Vigogo wa sheria UDSM waichambua Sadc

Saturday August 24 2019

Profesa Khoti Kamanga wa kitivo cha sheria,

Profesa Khoti Kamanga wa kitivo cha sheria, UDSM akiwasilisha taarifa ya uchambuzi wa Sadc jana wakati wa semina ya uelewa kwa wahadhari wa kitivo hicho.  Picha na Kelvin Matandiko. 

By Kelvin Matandiko Mwananchi [email protected]

Dar es salaam. Nguli wa Sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) nchini Tanzania, wametumia saa mbili kuchambua Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi 16 za Kusini mwa Afrika (Sadc) katika muktadha wa kisheria.

Katika mjadala uliofanyika Kitivo cha Sheria chuoni hapo jana Ijumaa Agosti 23, 2019, jijini Dar es Salaam wanazuoni hao wamepitisha mapendekezo kadhaa ikiwamo kuanza kutafsiri machapisho mbalimbali ya uelewa wa kisheria kwa lugha ya Kiswahili kuhusu Sadc.

Mjadala huo umefanyika ikiwa ni siku sita zimepita tangu Mwenyekiti wa Sadc, Rais wa Tanzania John Magufuli afunge mkutano Mkuu wa 39 wa wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya hiyo, uliofanyika jijini Dar es salaam.

Akiwasilisha matokeo ya uchambuzi wa ripoti ya uelewa kuhusu Sadc kisheria, Profesa Khoti Kamanga alisema pamoja na mafanikio makubwa chini ya mtangamano huo, yako masuala yanahitaji kufanyiwa marekebisho.

" Sekretarieti ya Sadc ni chombo kinachoendesha majukumu ya kila siku, ila kinapaswa kiwe na nguvu ya kufanya maamuzi, kuchukua hatua katika masuala mazito lakini haiwezi," alisema Profesa Kamanga.

"Kwa mfano kufuatilia nchi mwanachama iwapo haitatekeleza majukumu, lakini badala yake mamlaka yako kwa wakuu wa nchi na Serikali, hili linaweza kutazamwa upya."

Advertisement

 

 

Pamoja na mahitaji mapya katika mtangamano huo, Profesa Hamudi Majamba, Mkuu wa kitivo hicho alisema mahitaji ya soko la Kiswahili ni fursa wanazofuatilia kwa karibu.

"Tutaanza kuandaa na kutafsiri machapisho mbalimbali kwa lugha ya Kiswahili kuhusu Sadc, wananchi waelewe ili waanze kufuatilia fursa Jumuiya hiyo," alisema Profesa Majamba.

Hoja zilizoibuliwa katika muktadha wa kisheria ni pamoja na uhalali wa mwanachama mmoja kuwa sehemu ya mtangamano mwingine kama vile Comesa na Jumuiya ya Afrika Mashariki

Pia, wamehoji vigezo vya mwanachama kujiunga na kujiondoa, malengo, mkataba wa kuanzishwa kwa Sadc, ikionekana kisheria baadhi ya masuala yako sawa na yameleta manufaa.

Jambo lingine ni changamoto ya maslahi binafsi kwa nchi mwananchi kuchelewa kuridhia Itifaki zilizosainiwa na wakuu wa nchi hizo, ikionekana kuwa dosari.

Semina hiyo ni sehemu ya ratiba za kitivo hicho, ambayo huandaliwa kulingana na mahitaji ya mjadala au tukio linalojitokeza kwa wakati husika.

 

 

 

Advertisement