WHO yaitangaza corona janga la dunia

Muktasari:

WHO imesema kumekuwa na visa 98 katika mataifa mengine 18, ingawa hakuna vifo vilivyoripotiwa. Visa vingi vya wagonjwa hao vilitokana na watu waliosafiri kutoka mji wa Wuhan, eneo ambalo mlipuko wa ugonjwa huo ulianzia.

Geneva. Shirika la Afya Duniani (WHO) limevitangaza virusi vipya vya corona kuwa janga la dharura huku virusi hivyo vikiendelea kusambaa kwa kasi ndani na nje ya China.

"Sababu kubwa ya tangazo hilo si kwa sababu ya kile ambacho kinatokea China kwa sasa, lakini kile ambacho kinatokea katika mataifa mengine," alisema Tedros Adhanom Ghebreyesus, kiongozi mkuu wa WHO.

Kinachoangaliwa zaidi ni kuhusu ugonjwa huo kusambaa katika mataifa mengine huku kukiwa na mfumo duni wa afya, imeripoti BBC.

Watu takribani 213 wamefariki kutokana na virusi hivyo nchini China.

WHO imesema kumekuwa na visa 98 katika mataifa mengine 18, ingawa hakuna vifo vilivyoripotiwa. Visa vingi vya wagonjwa hao vilitokana na watu waliosafiri kutoka mji wa Wuhan, eneo ambalo mlipuko wa ugonjwa huo ulianzia.

Hata hivyo kuna kesi nane zilizosababishwa na maambukizi ya kati ya mtu kwa mtu huko Ujerumani, Japan, Vietnam na Marekani.

Akizungumza katika mkutano wa habari mjini Geneva, Uswisi, Dk Tedros alisema mlipuko wa ugonjwa ambao haujawahi kutokea awali na bado haujaweza kupata suluhu.

Dk Tedros alisifia hatua ambazo zimekuwa zikichukuliwa na serikali ya China katika kuzuia maambukizi yasienee na kuwa hakukuwa na sababu ya kuzuia watu wasisafiri au biashara zisiendelee.

"Lakini nataka kueleweka kuwa ,tangazo hili halimaanishi kuwa ni kura ya kutoiamini China".

Lakini nchi mbalimbali zimechukua hatua ya kufunga mipaka na kusitisha safari za ndege za nchini China, vivyo hivyo makampuni makubwa pia yamefunga maduka yao.

Ugonjwa huu umeanza mwezi mmoja tu mpaka sasa na tayari watu 7,736 zimethibitishwa kuugua nchini China na wengi zaidi wakiwa wanashukiwa kuwa na ugonjwa huo.

Kutangaza kuwa janga la dharura la dunia kutaweza kuruhusu WHO kuzisaidia nchi zenye kipato kidogo na cha katikati kujiandaa kukabiliana na virusi vya corona.

WHO huwa inatangaza kwa umma kuhusu dharura ya afya ya kimataifa kwa kuangalia tukio la mlipuko wa ugonjwa ambao si wa kawaida na kuna hatari kubwa ya maambukizi ya ugonjwa huo duniani.

Magonjwa mengine ambayo yaliwahi kutangazwa kwa njia hiyo ni mafua ya nguruwe (2009), polio, zika na Ebola.