Wafanyabiashara waitaka Tanzania kuridhia mkataba wa soko huria Afrika

Thursday September 12 2019

 

By Ephrahim Bahemu, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Wafanyabiashara nchini Tanzania wamesema Serikali inatakiwa kuridhia mkataba wa Soko Hurua la Afrika (AfCFTA) sanjari na kufanya kampeni a kuwaelewesha wananchi kuhusu fursa  wanazoweza kuzipata kupitia mkataba huo.

Hayo yameelezwa leo Alhamisi Septemba 12, 2019 katika mkutano wa wafanyabiashara ulioandaliwa na Taasisi ya Sekta binafsi nchini (TPSF) kujadili mustakabali wa Tanzania kuelekea katika mkataba huo.

Wafanyabiashara hao wamesema soko hilo lina fursa nyingi kuliko hasara.

Mwenyekiti na ofisa mtendaji mkuu wa kampuni ya Infotech Investment Group , Ali Mfuruki amesema Tanzania haina budi kuridhia mkataba huo bila hofu kwani kuna nchi kubwa na ndogo zimeuridhia.

Mtoa mada huyo kwenye mkutano huo amesema, “Mwaka jana Tanzania na nchi nyingine 44 za Afrika zilisaini mkataba huo lakini nchi chache ziliridhia kwa Afrika Mashariki bado Tanzania na Burundi.”

“Wafanyabiashara tunapaswa kusukuma hili kuhakikisha Tanzania nayo inaridhia ili wengine watakapoanza mwakani nasi tuweze kunufaika na soko hilo kubwa lenye watu zaidi ya bilioni 1.2.”

Advertisement

Mufuruki amesema Afrika inaweza kuendelea kwa kufanya ushirika ili sehemu kubwa ya biashara katika bara hilo ibaki Afrika.

“Ushirika siku zote ni kwa watu wasio lingana hivyo hakuna haya ya kuogopa kushirikiana kwa kigezo cha nchi kutolingana kiuchumi,” amesema Mufuruki.

Mkurugenzi mtendaji wa TPSF, Godfrey Simbeye amesema hata Tanzania isiporidhia Julai 2020 soko hilo litaanza na hakuna mbadala wa kutojiunga kama nchi nyingi zitakuwa tayari zimejiunga, ni vyema Tanzania ikajiunga.

“Manufaa ni makubwa biashara siku zote inakuzwa na soko, kama tunaweza kufanya biashara katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) wigo wa soko ukipanuka zaidi nasi tutakuza zaidi,” amesema Simbeye.

 

Advertisement