Wakosa nafasi JKT kwa kutojua kusoma, kuandika

Mkuu wa wilaya ya Chemba, Simon Odunga 

Dodoma. Athari za halmashauri ya wilaya ya Chemba kuwa miongoni mwa halmashauri za mwisho kwenye matokeo ya darasa la saba kitaifa zimejionyesha baada ya kushindwa kupata idadi kubwa ya vijana wa kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Akizungumza na Mwananchi, mkuu wa wilaya ya Chemba, Simon Odunga alisema kinachowakwaza vijana hao kupata nafasi JKT ni kutojua kusoma na kuandika.

Mwaka jana kwenye matokeo ya darasa la saba, halmashauri hiyo ilishika nafasi ya 186 kitaifa huku mwaka huu ikishika nafasi ya 183 kati ya halmashauri 186 nchini.

Pia, wanafunzi wote wa darasa la saba walirudia mitihani ya darasa la saba baada ya Baraza la Taifa la Mitihani kubaini udanganyifu katika mitihani hiyo mwaka jana.

Akifafanua zaidi kuhusu elimu katika wilaya hiyo, Odunga alisema katika matokeo ya mwaka huu halmashauri hiyo imefanya vizuri kwa kushika nafasi ya 183 ingawa bado iko katika kundi la halmashauri 5 za mwisho kitaifa na halmashauri ya mwisho kimkoa.

Alisema ufaulu umeongezeka ukilinganisha na halmashauri nyingine za mkoani Dodoma.

Odunga aliongeza kuwa kiwango cha ufaulu mwaka jana kilikuwa asilimia 37.7 lakini mwaka huu kimepanda kufikia asilimia 56.7.

Alisema kuongezeka ufaulu kumechangiwa kwa kiasi kikubwa na ushirikiano kati ya wazazi, walimu na bodi za shule pamoja na wakaguzi wa ubora wa elimu ambao walifanya kazi nzuri kuhakikisha wanakagua shule na kuhakikisha kuwa walimu wanaandaa vipindi na kufundisha.

Pamoja na dalili hizo njema kuanza kujionyesha lakini alikiri kuwa athari za matokeo hayo zimeanza kujionyesha baada ya idadi kubwa ya vijana wanaoomba kujiunga na jeshi kukosa sifa tatizo likiwa ni kutojua kusoma na kuandika.

“Mfano kuna nafasi 400 wanapatikana 50 tu wengine hawajui kusoma na kuandika, utampeleka wapi huyo sasa?” Anahoji.

Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Chemba, Dk Semistatus Mashimba alisema halmashauri hiyo ina upungufu wa walimu 812 katika shule za msingi.

Kwa upande wa vyumba vya madarasa, Dk Mashimba alisema kuna upungufu wa vyumba 915, nyumba za walimu 1,346, meza na viti 882. “Sasa hivi tumeanza kuvuna miti ili kukabiliana na upungufu huu,” alisema.

Utafiti wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) wa mwaka jana ulibaini mambo kadhaa yanayofanya Dodoma kufanya vibaya katika elimu.

Mambo hayo ni wazazi kushawishi watoto waandike madudu katika mitihani ya Taifa, ukosefu wa miundombinu, upungufu wa walimu na wanafunzi kutembea umbali mrefu kwenda shuleni ambapo kuna wanaotembea kilomita tano hadi 18 kwa siku.

Mmoja wa watafiti hao Dk Fransic William alisema walibaini kuna shule zina madarasa matatu tu, lakini wanafunzi wapo hadi darasa la saba na hivyo kulazimika wengine kusoma wakiwa wamekaa chini.

Anatoa mfano wa shule yenye walimu wawili lakini ina wanafunzi 700, hali inayomlazimu kuwa na vipindi 60 kwa wiki.

Alisema katika mojawapo ya shule pia kati ya watoto tisa waliokwenda kula chakula cha mchana nyumbani waliorejea walikuwa wanne kwa ajili ya vipindi vya mchana na wengine hawakuweza kurudi nyumbani kwa chakula cha mchana kwa sababu ya umbali.

“Ratiba ya wanafunzi wa shule za msingi kuwa na saa nyingi zaidi ya ile ya shule ya sekondari ambapo kwa sekondari ratiba ya masomo huisha saa 8.30 mchana wakati ya msingi humalizika saa 9.30 mchana,” alisema.