Wanawake 15 ‘wanaojiuza’ Dodoma watupwa jela miezi sita

Kamanda wa polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto

Muktasari:

  • Wanawake 15 mkoani Dodoma ambao walikuwa wanajihusisha na biashara ya kuuza miili yao wamefungwa jela mie sita.

Dodoma. Polisi mkoani Dodoma nchini Tanzania limewakamata na kuwafikisha mahakamani wanawake 15 ambapo wamehukumiwa kifungo cha miezi sita kila moja baada ya kupatikana na hatia ya kujiuza.

Jeshi hilo lilifanya msako Septemba 2,2019 saa tatu usiku mtaa wa Uhindini na kuwakamatwa wanawake 15 wakifanya biashara ya ukahaba huku wakidaiwa kuhatarisha amani na utulivu katika mtaa huo.

Akizungumza na wanahabari leo Alhamisi Septemba 5, 2019 Kamanda wa polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto amesema kitendo hicho ni kinyume na kifungu 176 (a) (f) (g) cha kanuni ya adhabu sura ya 16 kilichofanyiwa marejeo 2002.

“Washtakiwa walifikishwa mahakamani, walisomewa mashtaka na ushahidi dhidi yao ulitolewa na kuhukumiwa kifungo cha miezi sita gerezani kila moja bila kulipa faini.”

“Walikuwepo pia wanaume wanne waliosadikiwa kuwa ni wateja wao na waliachiwa huru baada ya kukosekana kwa ushahidi,” amesema Muroto.

Amesema makahaba hao waliona fursa ya kuja kufanya matukio ya kujiua kitendo ambacho hakikubaliki na kuwa msako huo ni endelevu.

“Sasa hivi wako gerezani Isanga wamepokelewa kwa ajili ya nguvu kazi, wataponda kokoto na kufanya kazi nyingine, watu hao ni Suzana Onesmo (27), Mariam Omary (29), Maimuna Issa (38), Bhoke Chacha (30), Swaumu Bakari (26),  Rahma Abdi (28), Magreth Humphrey (27),  Wema Saidi (25),  Jeniffer Wilson (33), Lydia Kilale (30),  Manka Richard (21),  Mwasuma Hassan (26),  Angel Joseph (29), Zaina ramadhani (30) na Tatu Saidi (27),” alisema.

Katika tukio lingine Jeshi la polisikwa kushirikiana na askari wa wanyamapori kutoka mkoa wa Iringa alikamatwa John Gabriel (53) akiwa na silaha aina ya Gobole yenye namba DA 827-08 akiwa anaimiliki kinyume cha sharia na akiitumia kinyume cha sharia kwa uwindaji haramu wa wanyamapori.

Amesema mtuhumiwa atafikishwa mahakamani upelelezi utakapokamilika.

Amesema katika msako dhidi ya wavunjaji, wezi, wanaohifadhi mali za wizi, wamekamatwa watuhumiwa wanne kwa makosa hayo

Katika tukio lingine kamanda  Muroto alisema Agosti 18, 2019 Mtaa wa Mazengo Kata ya Zuzu jijini hapa, jeshi hilo lilimkamata Baraka mgomochi (24), mkazi wa Nkuhungu akiwa na silaha aina ya bastola muundo wa bereta yenye namba AR- 3648-1981 yenye usajili wa TZC 68344 ikiwa na magazine ambayo haina risasi.

Alisema mtuhumiwa alifukia  silaha hiyo pembeni ya karo la choo na uchunguzi ulifanyika na kubaini silaha hiyo iliibiwa Kurasini Jijini Dar es salaam baada ya watuhumiwa kuvunja nyumba na kuiba.

Alisema mtuhumiwa atafikishwa mahakamani pindi upelelezi utakapokamilika.