Waziri Mwakyembe amwita Diamond Jamafest Taifa

Muktasari:

Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan leo Jumapili Septemba 22,2019 anazindua Tamasha la Utamaduni la Afrika Mashariki (Jamafest) linalofanyikia Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Tanzania.

Dar es Salaam. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo nchini Tanzania, Dk Harrison Mwakyembe amemtaja msaani maarufu nchini humo, Diamond Platnumz kuwa miongoni mwa wasanii watakaoiwakilisha Tanzania katika tamasha la utamaduni la Africa Mashariki (Jamafest).

Tamasha hilo linalofanyikia Uwanja wa Uhuru Dar es Salam nchini Tanzania, linazinduliwa leo Jumapili Septemba 22, 2019 na Makamu wa Rais wa nchi hiyo, Samia Suluhu Hassan.

Waziri Mwakyembe amesema tayari wamefanya mawasiliano na Diamond ambaye alikuwa mkoani Iringa kwa ajili ya Tamasha la Wasafi na leo moja kwa moja atafikia uwanja wa Uhuru unapofanyika uzinduzi huo.

“Tulimpigia akasema yupo Iringa yaani haiwezekani niko na makatibu wakuu wa nchi za Afrika mashariki na manaibu waziri halafu yeye awe yupo Iringa, njoo huku utetee taifa."

“Atakuja na ndege ya asubuhi na ninafikiri itabidi aje na kipaza sauti moja kwa moja aje kwenye tamasha awaburudishe vijana,” amesema Waziri Mwakyembe

Waziri huyo amesema, "Kuna vijana wa Burundi wameingia na ngoma kichwani wanapiga bila kuangalia, wakaja mabinti wa Rwanda wanacheza kama wanaruka angani hapana lazima na sisi tuwaonyeshe vijana wafurahie."

Tamasha hilo lililoanza jana Jumamosi litahitimishwa Septemba 28, 2019 ambapo katika siku ya tamasha hilo shughuli mbalimbali za kiburudani zitaonyeshwa.

Nchi hizo za Afrika Mashariki zinazoshiriki ni Kenya,Uganda, Rwanda, Burundi, Sudani ya Kusini na mwenyeji Tanzania.