Wizara ya Maliasili na Utalii Tanzania yawatangazia fursa wafanyabiashara mkutano wa Sadc

Thursday October 17 2019

 

By Rehema Matowo, Mwananchi [email protected]

Geita. Wizara ya Maliasili na Utalii nchini Tanzania imewataka wananchi hususan wafanyabiashara katika sekta ya utalii kutumia fursa ya uwepo wa mkutano wa Mawaziri 16 wa sekta ya za Mazingira, Maliasili na Utalii kutoka nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika(Sadc) kutangaza biashara zao ili kupata masoko nje na ndani ya nchi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Oktoba 17, 2019 mjini Geita nchini Tanzania, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu amesema uwepo wa mkutano huo ni fursa kwa wafanyabiashara kutangaza bidhaa zao na kukutana na watu mbalimbali ambao watawasaidia kupata masoko kwenye nchi za Sadc na duniani kwa ujumla.

Kanyasu amesema mkutano huo wa siku tano wenye lengo la kuangalia mwenendo wa hali ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi unatarajiwa kufanyika katika ukumbi wa kituo cha kimataifa cha mikutano Arusha (AICC) kuanzia Oktoba 21 hadi 25, 2019.

Amesema mbali na kuangalia mabadiliko ya tabianchi pia mkutano huo wa utabainisha utekelezaji wa mikakati ya hifadhi na usimamizi wa mazingira kupitia mkakati wa Sadc wa uchumi wa bahari na kutathmini maendeleo katika sekta za misitu .wanyamapori na utalii.

Naibu Waziri amesema mkutano huo wa mawaziri utatanguliwa na mkutano wa wataalam wa sekta ya wanyamapori utakaofanyika Oktoba 18 na 19, 2019 na kufuatiwa na mkutano wa makatibu wakuu wa sekta za mazingira, maliasili na utalii utakaofanyika Oktoba 21 hadi 21, 2019.

Mkutano huo wa mawaziri utafunguliwa na makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan Oktoba 25, 2019 katika ukumbi wa AICC huku mkutano wa makatibu wakuu ikitarajiwa kufunguliwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla  Oktoba 21 ,2019 katika ukumbi huo.

Advertisement

Jumuiya ya Maendeleo kusini mwa Afrika ni moja kati ya jumuiya za kikanda katika bara la Afrika iliyoundwa kwa dhumuni la kuimarisha ushirikiano katika nyanja za uchumi, ulinzi, siasa na usalama.

 

Advertisement