Bautista afunguka kilichofanya akonde
Muktasari:
- Akiwa kwenye mahojiano na ‘Chris Van Vliet’ alieleza kuwa awali uzito wake ulikuwa mkubwa sana, kutokana na filamu iitwayo ‘M. Night Shyamalan’ aliyokuwa akiigiza ilimbidi kupunguza uzito
Marekani, Baada ya kusambaa kwa picha za mwigizaji na nyota wa WWE, Dave Bautista zikimuonesha kapungua mwili tofauti na alivyokuwa awali, hatimaye mwigizaji huyo amefichua sababu za kupungua kwake.
Akiwa kwenye mahojiano na ‘Chris Van Vliet’ alieleza kuwa awali uzito wake ulikuwa mkubwa sana, kutokana na filamu iitwayo ‘M. Night Shyamalan’ aliyokuwa akiigiza ilimbidi kupunguza uzito.
“Nilianza kupunguza uzito kwa sababu maalumu. Kwanza, nilianza kupunguza kwa sababu nilikuwa nimejaa mafuta tu, nilikuwa mkubwa sana kwa ajili ya jukumu fulani na ilikuwa kubwa kupita kwenye Knock at the Cabin. Nilikuwa na karibu pauni 315 na nilipata uzito kwa haraka sana,” amesema Bautista.
Hata hivyo, aliongezea kwa kubainisha kuwa kutokana na muandaaji wa filamu hiyo kumtaka aonekane kama mtu mkubwa na siyo mnyanyua vyuma ilimbidi kula viazi vya kukaanga na Pancakes ili kuongeza uzito haraka.
Aidha aliwatoa hofu mashabiki wake waliokuwa wakihofia kuhusu afya yake katika mitandao ya kijamii kwa kueleza kuwa alikuwa na uzito mkubwa usio wa kawaida uliokuwa ukiathiri baadhi ya kazi zake kutokana na kuchoka haraka.
Bautista aliulizwa na mwandishi ni kitu gani amekitumia mpaka kikamkondesha kwa haraka na kujibu ni kufanya mazoezi na kuacha vyakula ambavyo vingemfanya anenepe.
Mbali na hayo aliwataka mashabiki kuuzoea mwili wake wa sasa kwani anampango wa kuendelea kufanya mazoezi ili apungue zaidi kwani kufanya hivyo kunamfanya ajisikie mwepesi (mwili kuwa mwepesi).
Utakumbuka kuwa picha za mwigizaji huyo zikimuonesha amepungua zilianza kusambaa kupitia mitandao ya kijamii mapema wiki hii, zilipingwa katika tamasha la Kimataifa la Filamu la Toronto ‘The Last Showgirl’.
Bautista alianza kujizolea umaarufu kupitia mieleka mwaka 2002 hadi 2019, na kuamua kujikita katika uigizaji rasmi ambapo ameonekana katika filamu kama ‘My Spy’, ‘The Killer's Game’, ‘Knock at the Cabin’, ‘Escape Plan’ na nyinginezo.