Bongo Fleva ni nyumbani kwa P-Square kwa miaka 17 sasa!

Muktasari:
- Ndivyo tunavyoweza kusema kufuatia kundi la muziki kutokea Nigeria, P-Square pamoja na wasanii wake ambao ni pacha (Peter na Paul Okoye) kuendelea kufanya kazi na wenzao wa Bongofleva ikiwa ni miaka 17 tangu utaratibu huo kuanza
Dar es Salaam. Ndivyo tunavyoweza kusema kufuatia kundi la muziki kutokea Nigeria, P-Square pamoja na wasanii wake ambao ni pacha (Peter na Paul Okoye) kuendelea kufanya kazi na wenzao wa Bongofleva ikiwa ni miaka 17 tangu utaratibu huo kuanza.
Kwa sasa mwanachama wa kundi hilo, Rudeboy (Paul) anasikika sana katika Bongofleva baada ya kushirikishwa na Harmonize katika wimbo wake mpya, Best Couple (2025) uliyotayarishwa na Cukie Dady.
P-Square, wakali wa miondoko ya Afrobeat, R&B na Dancehall, walianza kuvuma Afrika baada ya kutoa wimbo wao, Senorita (2003), kisha albamu ya pili, Get Squared (2005) ambayo iliwapa nafasi ya kuwania tuzo za MTV EMAs.
Wengi waliwapenda P-Square kupitia nyimbo zao mahiri na maarufu kama Temptation, Do Me, Bizzy Body, Roll It, Personally, Gimme Dat, Ifunanya, Chop My Money, Alingo, Shekini, Bring it On, Beautiful Onyinye n.k.
AY, mwanachama wa zamani wa S.O.G. na East Coast Team, ndiye mwanamuziki wa kwanza kutoka Afrika Mashariki kulishirikisha kundi la P-Square, kisha wakafuata wengine kama Cindy Sanyu wa Uganda na Diamond Platnumz wa Tanzania.

Miaka 17 iliyopita P-Square walikuja Bongo kufanya show ndipo wakakutana na AY na kurekodi wimbo, Freeze (2008) ukitayarishwa na Hermy B kutokea B’Hitz, studio ambayo ilimtoa Vanessa Mdee kimuziki kupitia ngoma, Closer (2013).
Hata hivyo, AY alishindwa kutoa video ya wimbo huu mkubwa kwa sababu zilizokuwa nje ya uwezo wake. Mwaka 2015, AY alikiambia kipindi cha Mkasi kuwa kulifanyika makosa ya kutoa wimbo huo bila video ambayo ilipangwa kufanyika Lagos, Nigeria.
Kufikia Januari 2015, Diamond akiwa Lagos aliketi pamoja na P-Square kisha kuandika wimbo uliokuja kufanya vizuri, nao ni Kidogo (2016) uliotayarishwa na Shirko kutokea Tanzania huku V-Teck wa Nigeria na Laizer wa Wasafi Records wakifanya mixing.

Video yake ambayo ilifanyika Aprili 2016 huko Johannesburg, Afrika Kusini chini ya kampuni ya Godfather Production, hadi sasa imetazamwa YouTube zaidi ya mara milioni 57.8 ikiwa ni video ya 10 kutoka kwa Diamond kutazamwa zaidi katika mtandao huo.
Mwaka 2016, migogoro ilipamba moto ndani ya P-Square, hiyo ni kufuatia Paul (Rudeboy) kupitia mtandao wa X, zamani Twitter kuibuka na kudai ameandika asilimia 90 ya nyimbo za kundi hilo, kauli ambayo haikumpendeza Peter (Mr. P).
Hali ilikuwa mbaya kwani migogoro ya kibiashara ilikuja kuibuka, Peter hakukubaliana na kaka yake na aliyekuwa meneja wao, Jude Okoye kwa mambo mengi, hivyo alitoka hadharani na kutangaza kumfuta kazi, na kisha kujiondoka ndani ya kundi hilo.

Tangu hapo kila mmoja akaanza kufanya muziki peke yake ambapo Peter alitumia jina la Mr. P huku Paul akijitambulisha kama Rudeboy, na hii ikawa zama mpya ndani ya Bongofleva kwa wasanii hao sasa wakifanya kazi kama solo na sio kundi tena.
Vanessa Mdee a.k.a Vee Money, alifanikiwa kumshirikisha Mr. P katika wimbo wake, Kisela (2017) kutoka katika mikono ya EKelly wa Nigeria ambaye ndiye alitengeneza wimbo wa Vanessa, Cash Madame (2016).
Wimbo huo (Kisela) uliokuja kujumuishwa katika albamu ya kwanza ya Vanessa, Money Mondays (2018), unatoa hadithi ya mwanamke aliyekatishwa tamaa na mapenzi baada ya kugundua kile alichodhani ni uhusiano wa kweli, kilikuwa ni uhusiano wa muda mfupi tu!

Video yake iliyosimamiwa na Clarence Peters imeshatazamwa mara milioni 4 YouTube, huku Vanessa akisema kuwa Mr. P ni mfano halisi ya msanii bora kwa jinsi walivyoigiza hadithi ya mapenzi kwa hisia na uhalisia ndani ya video hiyo.
Baadaye staa mwingine wa Bongofleva kutokea Kings Music, Alikiba alimshirikisha mwanachama mwingine wa P-Square, Rudeboy katika wimbo wake, Salute (2021) uliyotayarishwa na Yogo Beats, huku video yake ikifanyika Lagos na director wa huko, Paul Gambit.
Wimbo huu ulitoka wiki chache kabla ya Alikiba kuachia albamu yake ya tatu, Only One King (2021) ambayo ilifanya vizuri kwa kiasi chake ikishinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) 2021 kama Albamu Bora ya Mwaka.

Mapokezi ya wimbo huo (Salute) ndani ya muda mfupi hasa katika majukwaa ya kidijitali ni kitu kilichomshangaza Rudeboy na kusema Alikiba ana mashabiki wa kweli ambao wanajua nini maana ya kumuunga mkono msanii wao.
Na kwa sasa Rudeboy amerejea tena katika Bongofleva kupitia kolabo hii mpya na Harmonize, Best Couple (2025), ni kitu kinachofanya jina la P-Square kwa ujumla kuendelea kuingia na kutoka kama sio kuishi ndani ya Bongofleva kwa miaka 17 sasa.
Mbali na P-Square, msanii mwingine wa Nigeria aliyejitoa sana kwa Bongofleva ni Davido ambaye ameshirikiana na wasanii watatu wa hapa, nao ni Diamond Platnumz - Number One Remix (2013), Joh Makini - Kata Leta (2017) na Dayna Nyange - Elo (2021).
Ikumbukwe P-Square ambao walikuwa wasanii wa kwanza Nigeria kuingia tano bora chati ya SNEP Ufaransa.