Usiyoyajua kuhusu Jose Mlavichwa anayekula kenge, panya

Muktasari:
- Ni Josephat Mmasi maarufu kama ‘Jose Mlavichwa’ ndiyo anayezungumziwa hapa. Kijana aliyepamba video za mastaa kibao enzi hizo. Akaonekana kwenye movie ya Vocha, kwenye tamthilia ya Nafsi Yangu na sasa amechukua sura mpya kwenye mitandao ya kijamii baada ya video zake kusambaa akiwa anakula nyama za viumbe mbalimbali kama vile kenge, panya na wengineo.
Dar es Salaam. Ukitazama kwa umakini kwenye video ya wimbo wa Diamond ‘Nataka Kulewa’ utamwona Video King aliyepamba video hiyo lakini ukirudi kwenye ‘Marry Me’ wimbo wa Rich Mavoko utagundua kuwa Video King uliyemwona kwa Diamond ndiyo huyo huyo ametumika kwenye video hiyo.
Ni Josephat Mmasi maarufu kama ‘Jose Mlavichwa’ ndiyo anayezungumziwa hapa. Kijana aliyepamba video za mastaa kibao enzi hizo. Akaonekana kwenye movie ya Vocha, kwenye tamthilia ya Nafsi Yangu na sasa amechukua sura mpya kwenye mitandao ya kijamii baada ya video zake kusambaa akiwa anakula nyama za viumbe mbalimbali kama vile kenge, panya na wengineo.

Akizungumza na Mwananchi Jose anasema jila la Jose Mlavichwa alipewa na mwongoza filamu nchini Leah Mwendamseke ‘Lamata’.
“Hili Mlavichwa nilipewa na Lamata director wa Jua Kali mwaka jana alikuja Tanga akataka nimchomee kichwa hapo akaanza kuniita hilo jina. Itakuwa ni muda mrefu watu wamenisahau nilishafanya movie na Lamata aliiongoza.
"Lakini pia nilikuwa nafanya Swahili Fashion na kuonekana kwenye video za wasanii mbalimbali kama vile Rich Mavoko, Diamond, Belle 9, Shetta na wengine. Nilikuwa nafahamiana na Rammy baada ya Kanumba kufariki yeye akawa anafanya The Great tukaanza kufanya kazi nikafanya movie ya Vocha.
“Soko la sasa limebadilika sana zamani tulikuwa tunafanya movie tunauza steps, lakini kwa sasa wanafanya series wanaingia mikataba na makampuni hii inalipa zaidi. Naona Vitu vya kubadilisha kwenye soko la filamu ni stori na production ukiangalia kwenye movie za wenzetu zina uhalisia zaidi. Na sisi waongozaji wasiwe na hali ya kubana bajeti ili wapate kitu chenye ubora,” anasema.

Alivyoanza kula panya
Jose anasema ameanza kula viumbe hao muda mrefu tangu akiwa shule lakini sasa ndiyo ameamua kuchapisha kwenye mitandao ya kijamii kama maudhui.
“Hivyo vitu nimezoea kula lakini kilichobadilika ni maamuzi ya kushea na watu sijaanza jana au leo nakula siku zote. Nikaona naweza kutengeneza maudhui watu wakaona na wakajifunza. Mfano kenge ukimtengeneza na kulia ugali anakuwa mtamu sana hata panya ana nyama tamu kuliko ya kuku.
“Hivi viumbe Mungu ameviumba kwa ajili yetu kwa hiyo tusiwe na machaguo tu kama kuku na ng’ombe pekee. Zamani wakati nasoma nyumba yetu ilikuwa pembeni, kulikuwa na pori nilikuwa naenda kuwinda na mbwa. Kwa hiyo walikuwa wakikamata mnyama yoyote nawatengenezea wanakula ile minofu na mimi nachukua nakula ikaendelea hivyo,” anasema.
Anasema alianza kula viumbe hao kwa namna hiyo huku akikumbuka kiumbe wa porini wa kwanza kumla ni kicheche.

Licha ya kuwa na mitazamo mbalimbali juu ya sumu inayoweza kupatikana kwa viumbe hao Jose anasema kawaida huhakikisha akisafisha nyama hizo kwa ustadi wa hali ya juu ili asipate madhara.
“Mamba ananyongo hatari sana wanasema ikiingia kwenye mto inaweza ikaua kijiji kizima, lakini bado analiwa. Hata nyongo ya kuku au mbuzi ikiingia kwenye nyama inakuwa chungu kwa hiyo ni kwenye maandalizi tu.
“Natoa vitu vya ndani vizuri naiosha inakuwa safi nakula. Haijawahi niletea shida kwa sababu mwili wangu nakula kila kitu.
Kwenye familia yangu mtoto wangu wa kiume anatumia vitu vyote ninavyokula lakini mke wangu hatumii ila yupo sawa na ninachokifanya,”anasema.
Anasema hadi sasa amekula nyama za aina nyingi lakini nyama tamu kushinda zote ni ya Kenge.

“Wapo watu ambao wananipa wakiingia kwenye mabanda yao, wananipigia simu kama nipo Tanga wengine nawapooza na pesa,” anasema.
Anasema kutokana na anachokifanya amewahi kukutana na changamoto ya kufungiwa akaunti yake ya Instagram baada ya kuchapisha maudhui ya kula Kenge.
“Changamoto niliyokutana nayo ni moja tu kufungiwa akaunti yangu kwa sababu ya kula Kenge. Lakini mimi siendi mbugani kuwawinda wanakuja wenyewe.
“Pia nina mpango wa kwenda maliasili ili nikafanye nao mazungumzo kama ninachofanya ni sahihi au sio sahihi ili nisije nikajikuta navunja sheria bila kujua sitaki kujithibitishia kuwa nipo sawa bila kuwaona wahusika,” anasema.
Aidha kutokana na mitazamo mbalimbali ya anachokifanya kama ni uvunjifu wa sheria au yupo sahihi Dk. Thomas Kahema, kutoka Shirika la Ustawi wa Wanyama Tanzania (TAWESO) anasema kwa mujibu wa sheria ustawi za haki ya wanyama kenge haimwingizi moja kwa moja.
“Kenge sio mnyama pori lakini, anakuwa amemwindaje kama mwindaji anatakiwa kuwa halali na kama ni risasi anapiga mara moja ndiyo inavyotakiwa kwa wanyama pori. Lakini kwa wanyama wanaofugwa sheria ni kali zaidi. Kama vile paka kwa wanyama wanaoliwa hayupo.

“Kwa usalama wa chakula nyama huwa zinakaguliwa ili kuepusha mlipuko wa magonjwa. Kwa sababu hakuna ukaguzi wa nyama ya paka hapo kula mnyama huyo ni tatizo na kinyume cha sheria. Kwenye mazingira ya ukamataji wa huyo paka hata uchinjaji pia umefanyikaje hilo nalo ni tatizo.