Cardi B anachana anga tu ndani ya Spotify

Muktasari:
- Kwa matokeo hayo, Cardi B anazidi kung’aa ndani ya ‘Billions Club: The Series’ ya Spotify ambayo hujumuisha nyimbo zilizopata namba hizo katika jukwaa hilo liloanzishwa mwaka 2006, huku likiwa na watumiaji zaidi ya milioni 600 kila mwezi.
Rapa wa Marekani, Cardi B, 31, amefanikiwa kuwa na nyimbo nne ambazo zimesikilizwa (streams) zaidi ya mara bilioni 1 katika mtandao wa Spotify, huku akisema hatua hiyo inamfanya kuendelea kuwa na kiu ya kupambana.
Kwa matokeo hayo, Cardi B anazidi kung’aa ndani ya ‘Billions Club: The Series’ ya Spotify ambayo hujumuisha nyimbo zilizopata namba hizo katika jukwaa hilo liloanzishwa mwaka 2006, huku likiwa na watumiaji zaidi ya milioni 600 kila mwezi.
“Wanawake wanasema uongo, wanaume wanasema uongo, lakini namba hazifanyi hivyo. Nimefurahi sana kuweka muziki mpya katika hatua hii kubwa zaidi. Asanteni sana wote kwa kunisikiliza, hii ina maana kubwa sana kwangu,” anasema Cardi B.
Kauli hiyo inakuja baada ya wimbo wake, WAP (2020) akishirikiana na Rapa mwenzake, Megan Thee Stallion kufikisha ‘streams’ bilioni 1 Spotify ukiwa ndio wa nne tangu ametoka kimuziki.
Wimbo wa kwanza wa Cardi B kupata namba hizo ni Girls Like You ( 2018) aliyoshirikishwa na Maroon 5, kisha ukafuata I Like It (2018) akiwa na Bad Bunny na J Balvin, Taki Taki (2018) akishirikishwa na DJ Snake, Selena Gomez na Ozuna.
Cardi anafurahia mafanikio hayo baada ya Desemba 2023, Variety kuripoti kuwa Taylor Swift atapokea kitita cha Dola 104 milioni kutokana na mauzo ya muziki wake Spotify kwa mwaka huo ambao alikadiriwa kupata ‘streams’ zaidi ya bilioni 26.1.
Msanii mwingine wa kike mwenye rekodi kubwa Spotify ni Rihanna ambaye Julai 2023 aliandika rekodi kama mwanamuziki wa kwanza wa kike duniani kuwa na nyimbo 10 zenye ‘streams’ zaidi ya bilioni 10.
Nyimbo hizo ni Diamonds (2012), We Found Love (2011), Love on the Brain (2016), Stay (2012), This Is What You Come For (2016), Needed Me (2016), Four Five Seconds (2015), Work (2016), Umbrella (2007) na Love the Way You Lie (2010).
Ikumbukwe Cardi B alianza kuvuma kimuziki baada ya kuachia albamu yake ya kwanza, Invasion of Privacy (2018).
Albamu hiyo iliyotoka chini ya Atlantic Records na kuweka rekodi ya dunia ya Guinness kama albamu ya msanii wa kike iliyosikilizwa zaidi katika mtandao wa Apple Music ndani ya wiki moja.