Cardi B: Kuachana na Offset hakuna uhusiano na kulala pamoja

Muktasari:

  • Wawili hao walisherekea pamoja mkesha wa mwaka mpya huko Miami Beach ambapo kila mmoja alikuwa na shoo yake, kufuatia picha na video zao kusambaa mtandaoni zikaibua hisia huwenda wamerudiana.

Ukishangaa ya Mussa, subiri kuona ya Firauni. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya rapa  Cardi B kukiri kulala na aliyekuwa mume,  Offset kutoka kundi la Migos usiku wa mkesha wa mwaka mpya, lakini ameweka wazi kuwa  bado hawajarudiana.

Amesema isiwashangaze mashabiki wake, kwani  wanashughulikia tofauti zao kama wazazi na bila shaka mambo yatakuwa sawa. Ila kwa sasa walikula bata la mwaka na kulala pamoja, hivyo havihusiani na kuachana kwao. wameachana na wanalishughulikia hilo.

Wawili hao walisherekea pamoja mkesha wa mwaka mpya huko Miami Beach ambapo kila mmoja alikuwa na shoo yake, kufuatia picha na video zao kusambaa mtandaoni zikaibua hisia huenda wamerudiana.

Utakumbuka Desemba 2023 Cardi B, 31, alitangaza kuachana na Offset, 32, kwa madai ya usaliti katika ndoa yao yenye miaka saba sasa, huku wakijaliwa watoto wawili, Kiari Cephus, 5, na Wave Set Cephus, 2.

Cardi B amesema wakiwa Miami Beach kila mmoja alikuwa sehemu yake, kutokana wao ni binadamu walijumuika pamoja usiku huo wenye baridi kali, kusherekea mwaka mpya na walilala pamoja ila ni mapema kusema wamerudiana.

"Tumekuwa kwenye ndoa kwa miaka saba ila sifikirii kama tumerudi kuwa pamoja, tunahitaji kufanyia kazi mawasiliano yetu, kuna mambo ambayo anahitaji kufanyia kazi, name yapo nitakayoyafanyia  kazi” amesema.

Staa huyo akizungumza Insta Live aliendelea kwa kusema kwamba anaamini bado wanapendana, lakini anatambua kuwa usiku huo mmoja waliokuwa pamoja hautoshi kusuluhisha mambo yao na isitoshe ulikuwa usiku wa kufurahia tu.

Hata hivyo, hii sio mara ya kwanza kwa wawili hao kuonekana pamoja baada ya kutangaza kuachana kwao, siku chache zilizopita mashabiki waliwaona katika Jiji la New York.

"Lakini nimekuwa nikiogopa, sio hofu bali sijui jinsi ya gani ya kuuambia ulimwengu kuhusu  jambo hili lakini nahisi kama leo umekuwa mwanzo mzuri. Nina hamu ya maisha mapya na mwanzo mpya," amesema Rapa huyo wa Bodak Yellow.

Cardi B alivuma kimuziki baada ya kuachia albamu yake ya kwanza, ‘Invasion of Privacy’ (2018) iliyofanya vizuri na kumfanya kuwa msanii wa kwanza wa kike kushinda tuzo ya Grammy katika kipengele cha Albamu Bora ya Rap, huku ikishika nafasi ya kwanza kwenye chati za Billboard 200.