Kisa ‘uchumba sugu’, mpenzi wa Wizkid atema nyongo!

Muktasari:
- Hatua ya mashabiki kuhoji hilo kwa Jada P kupitia mtandao wa X zamani Twitter, inakuja baada ya mshindani wa Wizkid kimuziki, Davido hivi karibuni kufunga ndoa ya kifahari na mpenzi wake wa kitambo Chioma
Nigeria, Kwa mara nyingine tena mpenzi wa Wizkid, Jada P ametema nyongo na sasa ikiwa ni baada ya kuandamwa mtandaoni na mashabiki wanaohoji ni lini ataolewa maana uhusiano wake na msanii huyo wa Nigeria ni wa miaka mingi.
Hatua ya mashabiki kuhoji hilo kwa Jada P kupitia mtandao wa X zamani Twitter, inakuja baada ya mshindani wa Wizkid kimuziki, Davido hivi karibuni kufunga ndoa ya kifahari na mpenzi wake wa kitambo Chioma.
Wizkid na Jada P walikutana kwa mara ya kwanza mwaka 2012, wakati mrembo huyo akiwa bado ni Meneja wa Chris Brown, walianza kufanya kazi pamoja 2014 kisha baadaye kuingia katika uhusiano ambao umeleta watoto wawili.
“Ni wangapi kati yenu mnaozingatia mada hii! wengi wenu mnaoandika hamna uzoefu, maarifa au ufahamu wa nini kinahitajika ili kuwa na furaha, ndoa yenye afya na mafanikio ambayo inadumu milele!..” Jada P aliwajibu mashabiki hao.
Ujumbe wa Jada P umezua mijadala mtandaoni ambapo baadhi ya mashabiki wameunga mkono msimamo wake na kusema ni muhimu kuwa na msingi imara kabla ya ndoa yenyewe.
Hata hivyo, hii sio mara ya kwanza kwa Jada P kujitokea hadharani na kutolea ufafanuzi baadhi ya mambo katika uhusiano wake na Wizkid, mathalani tofauti ya umri kati yao iliwahi kumuweka kitimoto mtandaoni.
Lakini Jada P, alitumia Insta Story kujibu hilo ambapo kukiri ni kweli amemzidi Wizkid umri kama miaka mitano hivi na sio kama ambavyo ilikuwa ikienezwa kwa lengo la kupotosha.
Jada P alizaliwa Marekani Oktoba 20, 1983, alisoma Shule za St. Saviour’s na St. Olave Uingereza na baadaye kupata shahada Chuo Kikuu cha Westminster, London. Kwa upande wake Wizkid alizaliwa mnamo Julai 16, 1990 huko Lagos, Nigeria.
Wakati wawili walipojaliwa mtoto wao wa kwanza, Zion Ayo Balogun aliyezaliwa London, Uingereza hapo Novemba 11, 2017, Jada alisema uhusiano wao ulianza rasmi msimu wa wapendanao (valentine’s) Februari 2017.
“Mimi sio mama mtoto wa Wizkid pekee, bali ni meneja anayefanya kazi kwa bidii sana kuinua na kusukuma harakati za muziki kimataifa ambazo zina maana kubwa kwetu.” alisema Jada P mwaka mmoja baada ya kuzaliwa Zion.
Akiwa kama meneja wa Wizkid, Jada P amemsaidia msanii huyo kusaini mikataba minono iliyomuunganisha na majina makubwa katika tasnia ya muziki duniani kama vile Drake, R Kelly, Chris Brown, Justin Bieber na Beyonce.
Jada P anajivunia kumpatia Wizkid tuzo ya kwanza ya Grammy mwaka 2020, huku akishinda tuzo nyingine kubwa kama BET (4), Soul Train Awards (3), Billboard Awards (3), iHeartRadio Music Awards (2), America Music Awards (1) n.k.
Ikumbukwe hapo awali Jada P alifanya kazi na kaka yake mwanamuziki Akon, Bu Thiam katika kampuni yake ya usimamizi chapa, Bu Vision, LLC, ambapo aliwakilisha na kusimamia baadhi ya wanamuziki wakubwa wa kimataifa kama Chris Brown na Pia Mia.