Lucy Komba: Niliondoka Tanzania kwa sababu  ya mapenzi

Muktasari:

  • Filamu hizo zilipita mikononi mwa mwanadada Lucy Komba ambaye ndiye alimwaga wino katika uandishi, jambo lililofanya ajizolee mashabiki wengi waliojenga imani juu tungo zake.

Denmark, Ni ngumu kutaja filamu zilizofanya vizuri miaka ya 2000 na kuziacha Yolanda 1-2, Utata, Ama Zako Ama Zangu, na Vice Versa, ukali wa filamu hizi ulitokana na uwepo wa waigizaji makini na utunzi mahiri wa stori zake.

Filamu hizo zilipita mikononi mwa mwanadada Lucy Komba ambaye ndiye alimwaga wino katika uandishi, jambo lililofanya ajizolee mashabiki wengi waliojenga imani juu tungo zake.

                      

Lucy ambaye kwa sasa anaishi nchini Denmark aliliambia gazeti hili kuwa mapenzi ndiyo chanzo cha yeye kuondoka nchini Tanzania na kwenda nchini huko ambako anaishi sasa.

“Mapenzi yalinifanya niondoke Tanzania, nashukuru Mungu mume wangu ni mzungu raia wa Denmark tulikutana hukuhuku kwa sasa nina watoto wawili.

“Wa kwanza wa kiume yule niliyekuja naye niliyemzalia Afrika, wa pili wa kike ambaye nimemzalia huku wa mume wangu. Kwa hiyo na mtoto mweusi kama mimi na Afrikasti,” alisema Lucy.

Alivyomleta mjini mwigizaji Irene Uwoya
Wiki tatu zilizopita mwigizaji Irene Uwoya kupitia ukurasa wake wa Instagram alichapisha ujumbe wa kumshukuru Lucy kwa kumtambulisha kwa Watanzania. 

Aliandika: “Huyu dada ndiye mtu wa kwanza kuniona na kunipenda na kuniweka kwenye movie yake inaitwa Yolanda, Mungu akubariki sana natamani nikuone tena Lucy Komba,” aliandika Uwoya.

                       

Kutokana na chapisho hilo Lucy amesema lilimpa furaha kuona bado Irene anathamini mchongo wake.

“Irene alinishukuru na mimi nilifurahi kwa sababu niliona mchango wangu haujapotea, yaani haujafutika unajua ukifanya kitu hata kama miaka imeenda halafu akitokea mtu anasema amekumbuka mchango wako inafurahisha sana, namjua Irene huwa hana matatizo na mtu yeyote ni mtu wa shukrani sana,” anasema.

Mbali na hilo amesimulia kuwa kwa mara ya kwanza aliona picha ya Irene kwenye gazeti na ndipo alimpenda na kutamani atokee kwenye movie yake.

“Kuna siku nilikua nimekaa saluni natengeneza nywele karibu na nyumbani kwangu kipindi hicho Irene nakumbuka alikuwa anashiriki Miss Tanzania, kulikuwa na gazeti pale saluni, kuna dada msusi aliitwa Vero alikuwa anapenda kununua magazeti kila siku.

“Enzi hizo magazeti ya udaku kwa hiyo alinunua gazeti likionesha washiriki wa Miss Tanzania Tano Bora,  ziliwekwa picha zao na Irene akiwemo kipindi hicho nafikiri alikuwepo Wema Sepetu, Jokate Mwegelo, na Lissa lakini mimi jicho langu moja kwa moja lilienda kwa Irene Uwoya,” alisema.

Anasema baada ya kumuona Irene kwenye picha alivutiwa naye na ndipo akaomba apatiwe namba zake.

“Nikasema ningependa huyu msichana aje afanye filamu na mimi, ana mvuto nilivyomuangalia niliona  anajua, kuna dada mmoja akasema anamfahamu nikachukua karatasi nikampa namba nikamwambia ampelekee ili anitafute kwa hiyo mashindano yalivyoisha akanipigia tukakutana nikamwambia napenda acheze filamu yangu,” anasema.

Alivyotii ombi la mashabiki

“Watu wengi wanajua utunzi wangu na wamekuwa wakisifia filamu zangu ambazo nimekuwa nikizifanya Tanzania bado wananifuata kwenye Facebook DM wananiambia rudi sanaa ya Bongo imeharibika.

“Bado wananiulizia stori zangu za zamani kama vile Utata na Yolanda ndiyo maana nikaona nije kwa staili mpya ya ‘series’ ambayo asilimia 99 nimeandika mwenyewe,” anasema.

                       

Licha ya kuwa umepita muda mrefu tangu mwigizaji huyo kuachia kazi na kuonekana machoni mwa mashabiki, Lucy kwa sasa ameingia tena kwenye soko la Bongo Movie kwa kuungana na wasanii wengine waliopo Ulaya na kufanya filamu iitwayo ‘Malaika’ inayoruka kwenye mtandao wa YouTube.

Lucy alisema kilichofanya awe kimya kwa muda wote ni ubize hivyo ameona sasa ndiyo muda muafaka kwake kuachia kazi.

“Tangu nilipofika huku Denmark nilikuwa bize kusoma lugha, maana hawaongei Kiingereza muda mwingi nilikuwa shule nilikuwa napenda kufanya kazi ya sanaa na ilikuwa kwenye damu, nilikuwa najisemea kuwa nikitulia lazima nifanye series,”anasema.

Anaongeza kuwa  Malaika imekuja kwa ajili ya kuwashika watu kwani ndani yake ina stori ambayo ni ngumu kutabiri kinachotokea mbele.

“Series ya Malaika imekuja kuwashika watu, sitaki kuongea mambo mengi kuna kitu kipo ndani nataka waangalie wenyewe kwa sababu ukiangalia huwezi kujua kinachofuata kwa kifupi Malaika ni jina ambalo limekuwa likijulikana sana kwenye mataifa mengi,”anasema.

Waigizaji wa Tanzania wanaoishi Ulaya kuungana

Hata hivyo, katika filamu hiyo ya ‘Malaika’ wanaonekana waigizaji wengine wa Tanzania ambao hawajatokea kwenye filamu kwa muda mrefu kama vile Mohamed  Mwikongi ‘Frank’ na Issa Mussa ‘Cloud 112’

Lucy ameeleza kuwa alipata wazo la kuunganisha waigizaji wa Tanzania ambao wanaishi Ulaya kwa sababu wanaipenda sanaa ya Tanzania.

“Nilipata idea ya sisi wasanii ambao hatupo Tanzania kwa nini tusijikusanye kufanya sanaa, ili tusije tukapotea tuna vipaji na tunapenda sanaa ya Tanzania kwa hiyo tukarudi kwa sababu ya mapenzi”,alisema.

Njia aliyotumia kupata waigizaji kwenye Malaika
Filamu hiyo ya ‘Malaika’ imejumuisha wasanii mbalimbali wakiwemo kutoka Tanzania na waliopo nje ya nchi.

Lucy anasema alitumia mitandao kuwapata waigizaji hao kwa kutangaza kwenye mitandao ya kijamii na kisha kufanya mchujo hadi kupata wanaofaa.

“Kwa Watanzania nilitangaza Instagram pia nikaongea na Kilo Man akanisaidia kutangaza kwenye magrupu wakaja wasanii wengi tukafanya mchujo wakapatikana, wasanii wa Denmark ni watu ambao nawafahamu kwa ukaribu kama kuna mmoja huyo Selembe tuko naye alikuwa kwenye grupu huku Denmark,”anasema.

Wasanii kupigika na maisha Ulaya

Wapo wanaodai kuwa wasanii wengi nchini wakienda kwenye mataifa mengine, huishia kuishi maisha magumu kutokana na kukosa thamani kama wanayopata nchini kwani katika mataifa hayo huwa hawafahamiki.

Kwa upande wake Lucy ameeleza kuwa alivyofika Denmark alikuwa hajali lolote kwani watu walikuwa hawamfahamu hivyo hakuona ugumu wowote wa maisha.

“Sijui kwa wengine kama maisha ya Ulaya ni magumu kwa wasanii mimi nilikuwa sijali nilianza maisha chini bila kujulikana na mpaka sasa sijulikani, huku wananijua Waafrika nilikuwa nakutana na Wakongo, Watanzania ambao tayari wameona filamu zangu.

“Mwanzoni nilikuwa najitanua tu lakini mimi sioni kama kuna ugumu kwa mtu kutofahamika wakati sijaanza sanaa nilikuwa sifahamiki na nilikuwa naishi vizuri,”alisema.

Lucy ambaye kwa sasa ana zaidi ya miaka mitano tangu aondoke nchini ameeleza kuwa mwaka juzi alitua nchini kusalimia na kisha kurejea Denmark

“Mwaka juzi nilikuwa Tanzania sasa nina miaka miwili tu nikikaribia kuja Tanzania mtajua, namshukuru Mungu nilifurahi nilikula vyakula vyote vya Kiafrika sababu tunavikumbuka”,alisema.

Aidha ameeleza kuwa muda wote akiwa Denmark amekuwa akiikumbuka familia yake na marafiki ambao alikuwa nao Tanzania.

“Tanzania nakumbuka sana familia yangu, marafiki nawakumbuka ingawa wengine walinikimbia kwa maana ukiondoka nchini marafiki wanakimbia wanadhani mtu harudi lakini bado wapo ambao tunawasiliana kama vile Nikita, Koleta nawakumbka sana,”anasema.

Ombi lake kwa mashabiki

Lucy hakuacha kuzungumza na mashabiki wake kwa kuwaomba ushirikiano katika kipindi hichi ambacho amerudi kwenye gemu

“Mashabiki wangu sijui nawaambiaje wapo ambao wananipenda naona wapo ambao ni wanafiki lakini hawana chochote, wapo wanaosema wamekumbuka  filamu zangu lakini nimetengeneza unaona hakuna ambao wanakuja kuangalia, wanakuja lakini siyo kivile pengine ni kwa sababu walikuwa hawajui nilipo. Ninaomba sana ushirikiano wao nimerudi,”anasema.