Maajabu ya Dogo Paten na njia zitakazofunguka

Muktasari:
- Kabla ya hapo Dogo Paten hakuwa ametoa ngoma hiyo rasmi alirekodi vipande tu na kuvipakia kwenye mitandao ya kijamii hasa TikTok na Instagram ambako huko Zuchu alivutiwa nao.
Dar es Salaam. Nyota ya msanii chipukizi wa singeli, Dogo Paten inazidi kung’ara kila uchao tangu Zuchu alipomshika mkono.
Kwa sasa kila mitaa inapigwa ngoma ya Afande ambayo ni wimbo wa Dogo Paten akimshirikisha Zuchu.
Kabla ya hapo Dogo Paten hakuwa ametoa ngoma hiyo rasmi alirekodi vipande tu na kuvipakia kwenye mitandao ya kijamii hasa TikTok na Instagram ambako huko Zuchu alivutiwa nao.
Baada ya kuupenda msanii huyo wa WCB, akatangaza kufanya naye remix ili kumpa dogo huyo sikio kwa wapenda muziki.
Na kweli wakafanya ngoma hiyo na sasa ipo kwenye mtandao wa YouTube wa Dogo Paten yaani Zuchu alionyesha upendo wake kwa msanii huyo mwenye kipaji cha kuimba na kuandika mashairi ya singeli.

Kiufupi nyota yake iliendelea kung’aa pale tu Zuchu alipomtambulisha kuwa anatamani Watanzania wamsapoti kama alivyosapotiwa yeye kipindi anaanza muziki.
Kabla ya hapo Dogo Paten na mwenzake Dogo Sajenti walikuwa maarufu mwaka jana kupitia wimbo wa Salio wa Marioo walioufanyia remix na kuugeuza kwa upande wa singeli.
Wimbo huo uliendelea kupendwa na Watanzania wengi kama unavyojua singeli ni moja ya muziki unaopendwa nchini.
Kwenye remix hiyo ambayo Dogo Paten alidai kuwa yote aliiandika yeye na mwenzake alipita tu, Sajent alikitendea haki kipande kile kana kwamba aliandika yeye na akaenda mjini kuliko mwenzake.
Mambo yanakwenda kwa kasi sana na unaweza kusema wakati wa Mungu ni wakati sahihi, mwanzoni Sajenti alipewa sikio sana na sasa Paten amependwa haswa.
Maajabu ya Dogo Paten sasa wimbo wake wa Afande ndio umekuwa kama wimbo wa taifa na akipanda jukwaani anaondoka na kijiji.
Mwananchi imekuchambulia maajabu ya msanii huyo na njia zitakazofunguka kwenye muziki wake.

Matangazo
Kupitia umaarufu alioupata Dogo Paten ni wazi njia mbalimbali za rizki zitafunguka kutokana na ushawishi wake mitandaoni.
Kadri jina la msanii huyo linavyokua maarufu ndivyo nafasi za kujitangaza zinavyoongezeka.
Kazi moja tu ya Afande inaweza kumpa dili nono chipukizi huyo anayekuja kwa kasi nchini na kampuni zinaweza kumwona kama mfano mzuri wa kuwekeza kwake.

Shoo
Tangu apate umaarufu si chini ya shoo saba kubwa amefanya msanii huyo na bado anaendelea kupata kila uchwao.
Alialikwa na Billnass kwenye shoo ya Chuo kwa Chuo, alipokewa nyema na wanachuo hao, pia Zuchu alimpandisha kwa dakika tano kwenye jukwaa la Samia Music Festival pale Tanganyika Packers.
Ukiachana na hizo kwenye sherehe ya kutimiza mwaka mmoja kwa mtoto wa Marioo, Paten alikuwepo pia na kumpagawisha Paula na wasanii wengine waliohudhuria.
Kwa sasa shoo zote zipo mkononi kwa nyota huyo ni kama password ya simu kila sehemu ipo sehemu chache tu ndio utazikosa.
Kwa shoo hizo kubwa alizofanya na wasanii mbalimbali maarufu inamuhakikishia kuendelea kuitwa kwenye majukwaa.

Kolabo
Muziki sasa umekuwa biashara wawekezaji hawaangalia kipaji pekee bali ukienda kwa jamii utaleta matokeo gani na msanii anapata faida.
Kolabo moja alipata kwa Zuchu imempa umaarufu mkubwa lakini kuna wasanii wengine wataangalia fursa hiyo ili kuenda mjini.
Kwenye matamasha makubwa kuna mkusanyiko wa wasaniii mbalimbali mfano kwenye shughuli ya Marioo kulikuwa na Harmonize, prodyuza P Funk Majani, Nandy, Billnas na wengineo ambao anaweza kupata kolabo nao.