Mandojo kutoka muziki hadi uwekezaji

Mwandishi wa gazeti hili, Imani Makongolo akifanya mahojiano na msanii Mandojo

Japo wengi walimfahamu kupitia muziki, wimbo wake wa ‘Nikupe nini mpenzi’ ukimtambulisha kwenye gemu miaka ya 2000, ndoto yake kubwa ilikuwa ni biashara, akalazimika kuanza kutafuta mtaji kwa kuuza maji kwenye toroli katika maeneo mbalimbali yaliyokuwa na shida ya maji jijini Dar es Salaam.

Huyu ni msanii Mandojo, ambaye jina lake halisi ni Joseph Francis Michael. Nyota huyo amezidi kuwa maarufu, hasa eneo la Mbande Kisewe, ambako ameanzisha mradi mkubwa wa soko ambao ukikamilika utamuingiza kitita cha Sh115,000 kila siku ambayo ni kama Sh4,800 kila baada ya saa moja hata akiwa nyumbani amelala.

Mwanamuziki huyu ambaye 'damu' yake na mapenzi yake ni biashara anasema alianza kuishi kwenye ndoto hiyo akiwa shule ya msingi, huko Manyoni, mkoani Singida ambako alikulia, kulelewa na kusoma akiwa na wazazi wake ambao wote wametangulia mbele ya haki.

“Nilifanya biashara ya kuuza maji nikiwa shule ya msingi, likizo zangu zote nilipokuwa nakuja Dar es Salaam kwa mmoja wa ndugu zangu, sikukaa kizembe, nilijishughulisha na kuanza biashara hiyo nikiuza maji kwa dumu, wakati ule moja liliuzwa Sh200 hadi Sh300,” anasema Mandojo, aliyezaliwa mwaka 1978.

Anasema alipata pesa nzuri kwenye biashara hiyo miaka ya 1990 ambazo zilimsaidia kununulia baadhi ya mahitaji ya shule bila kumtegemea mzazi na wakati mwingine hata nyumbani alisaidia.

“Nilifanya hivyo kila nilipokwenda likizo hadi nikahitimu kidato cha nne na kutoka Manyoni kuhamia Dodoma ambako nilijiunga na kidato cha tano na kuhitimu kidato cha sita katika Shule ya Jamhuri, lakini sikubahatika kuendelea na chuo.

“Kwa kuwa nilipenda kujishughulisha, nilikuwa na akiba ya Sh120,000 ambazo nilizipata katika biashara ya kuuza maji niliyokuwa naifanya wakati nasoma, nikaanzisha biashara nyingine ya kuuza vitu vidogovidogo stendi ya mabasi,” anasema Mandojo, ambaye sasa anamiliki biashara yenye mtaji wa Sh100 milioni nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

“Nilifungua kibanda changu Dodoma stendi na kuanza kuuza shampoo, biskuti, chocolate na vitu vingine vidogovidogo, nikiwauzia pia abiria kwenye mabasi,” anasema Mandojo, staa wa Bongofleva katika mahojiano maalumu na Mwananchi.

Mandojo, ambaye amekuwa na kombinesheni tamu jukwaani sanjari na Domokaya wakiwa na staili yao ya kutumia gitaa, walitamba na nyimbo zao kali ikiwamo ‘Wanoku noku watu wa kupakazia’ na ‘Nikupe nini mpenzi’ ambayo ndiyo iliwatambulisha kwenye Bongofleva.

Kutoka kanisani hadi kuimba Bongo fleva

Anasema kipaji chake kilianzia kanisani, akiwa miongoni mwa waimbaji kwaya ya Might Melody Brothers kilichokuwa kikundi cha Kanisa la Anglikana, ambako walitoa albamu mbili za injili.

“Nilianza muziki nikiwa darasa la saba, nikiimba nyimbo za dini kanisani ambako huko ndipo nilijifunza kutumia gitaa.

“Kipindi hicho ilikuwa ni ngumu kupata vyombo vya muziki isipokuwa kanisani, familia yangu ilikuwa ni waumini wa kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Rift Valey kule Manyoni, na mimi nilikuwa muumini wa kanisa lile tangu utotoni,” anasema Mandojo ambaye asili yake ni Mkoa wa Mara, baba yake akiwa Mkurya na mama Mjaluo.

“Mama yangu alikuwa akiimba kwaya, hivyo mara nyingi nilipenda kuimba naye hadi nilipojitambua mwenyewe pale kanisani nikaanza kujifunza kutumia gitaa, kulikuwa na wakaka wengine sita ambao nao walikuwa wanapiga gitaa, tukaanzisha kikundi chetu cha kwaya cha watu saba kilichoitwa Might Melody Brothers,” anasema.

Anasema walianzisha staili tofauti ya kwaya kanisani na iliyokuwa imezoeleka, waliimba kama Bongofleva, lakini ya injili na kutoa albamu mbili, ya kwanza iliitwa ‘Usitugonganishe’ na baadaye akiwa Arusha walimpitia na kwenda kufanya albamu ya pili jijini Nairobi Kenya, iliyoitwa ‘Neema za Mungu’.

Anasema akiwa Arusha ndiyo akajikita kwenye muziki wa kizazi kipya.

“Nilikwenda Arusha kwa kaka yangu, huko ndipo nilianzia Bongofleva, sikuhitaji kuomba ruhusa kwa wazazi ili kuingia kwenye huo muziki, japo ni kweli wakati ule kijana ukiingia huko ilionekana ni uhuni, hata hivyo wazazi wangu hawakufahamu hadi nilipokuwa maarufu na wao kupewa sifa tu.”

Anasema akiwa Arusha ambako alikwenda kwa ajili ya kufanya biashara ya vinyago ambayo aliifanya kwa kununua kwa wachongaji na wakati mwingine kwenda vijijini kutafuta miti na kuwalipa wachongaji gharama ya kuchonga na kuviuza kwa jumla na rejareja kwa watalii na wauzaji wa vitu vya asili, bado aliendelea kupiga gitaa na huko ndipo alikutana na Domokaya, ambaye alipenda pia kujifunza kupiga gitaa.

“Jirani na alipokuwa akiishi kaka yangu, Domokaya alikuwa na rafiki yake, mara kwa mara alikuwa akija kumtembelea ananikuta napiga gitaa, wakati huo akiwa mdogo mdogo akatamani kujifunza tukawa marafiki,” anasema.

Anasema hiyo ilikuwa ni mwaka 2000, wakajikuta tu wameanza kupiga gitaa pamoja na kutunga wimbo wa ‘Nikupe nini mpenzi’ ambao ilikuwa ni wazo walilolitoa kichwani.

“Hata hivyo tulitamani sana kukutana na kufanya kazi na P Funk Majani, wakati ule ukifanya kazi na prodyuza mwingine unaonekana bado.

Juma Nature awarahisishia

Anasema wakiwa hawafahamu watakutana vipi na Majani, siku moja wakasikia mkoani humo kuna shoo ya Juma Nature ambaye alikuwa akizindua albamu yake ya ‘Ugali’.

“Tulisikia na P Funk anakuja pia kwenye tukio hilo, tukajipanga ipasavyo kutimiza lengo letu, siku ya tukio kabla ya ile shoo mimi na Domokaya tukaenda pale hotelini walipofikia, tukiwa mapokezi akatokea Juma Nature, tukamfuata na kumueleza kuwa sisi ni wasanii, na tunatamani kuonana na P Funky. “Nature alitusikiliza, tukamuimbia na kupiga gitaa, akatukubali sana akatwambia anatupeleka kwa Majani mwenyewe, hivyo Nature akawa ameturahisishia njia,” anasema.

Anasema walipokwenda kwa Majani alipowasikiliza akawakubali, safari yao ya muziki ikawa rahisi tofauti na walivyotarajia kwa kuwa wakati huo ilikuwa ngumu kuingia kwa prodyuza huyo.

“Ilikuwa hadi uingie kwa Majani uwe msanii kweli, Bongo Records ilikuwa ina vichwa vingi vinajielewa kwenye muziki, hadi upate nafasi lazima uwe vizuri kwelikweli,” anasema.

Waibiwa kila kitu walipokuja Dar kurekodi

Anasema walipokuja Dar es Salaam kurekodi wimbo wao wa ‘Nikupe nini mpenzi’, waliibiwa kila kitu na ndipo walipopata wazo la kutunga wimbo wa ‘Niaje’.

“Ukisikiliza verse ya tatu ya huo wimbo, nasema tulipigiwa simu siku ya Alhamisi kwenda Dar kurekodi, lile ni tukio la kweli ambalo hatuwezi kulisahau, likasababisha tuishi kwa tabu mjini.

“Tuliibiwa kila kitu, tukiwa tunaelekea kwa baba mdogo Vingunguti na kusababisha kutembea mtaani na malapa halafu tuna gitaa kama machizi.

“Bahati nzuri, mwizi aliiba kila kitu lakini akaacha gitaa ambalo tulikuwa tumeliazima kwa mwanetu (rafiki yao) kama angelichukua na hili, maana yake angekuwa ametukata mikono,” anasema.

“Kesho yake tunaamka, tumeibiwa kila kitu, mdogo wangu (Domokaya) alikuja na dundo lake rangi ya kahawia nalo likaibiwa, ilituumiza sana,” anasema.

Pesa ya kwanza walinunua simu sare

Anasema baada ya kurekodi wimbo wa ‘Nikupe’ uliofanya vizuri, Ruge (sasa ni marehemu) aliwapa nafasi ya kwanza ya kufanya shoo. “Ilikuwa ni kwenye hoteli ya Movenpick (sasa Serena) ambako kulikuwa na uzinduzi wa albamu ya Q Chillah na Papii kocha. “Tulilipwa Sh600,000 kila mmoja, ilikuwa ni nyingi sana kwetu wakati ule ukizingatia tuko mjini, hatuna mchongo wa kushika hela, halafu mara laki sita ya shoo hii hapa, tulifurahi.

“Mimi nilinunua runinga, kipindi hicho ndipo simu zimetoka toka hapa kwetu, tukanunua sare sare na Domokaya.”


Safari za Ulaya zaanza



Anasema baada ya muda walianza kupata shoo nyingi za nje ya nchi, katika nchi za bara la Ulaya, japo ilikuwa ngumu kujulikana nchini kutokana na mazingira ya teknolojia wakati huo. “Teknolojia ilisababisha tutumie nguvu kubwa kutoboa, tofauti na sasa, nakumbuka mwaka 2005 tulienda Uingereza kufanya shoo kwa miezi miwili kwenye miji tofauti.

Anasema kwenye shoo inayofanywa na msanii kutoka Tanzania, japo wazungu wanakuwepo, lakini wengi wanakuwa ni Watanzania kutoka kwenye miji tofauti wanaoishi huko. “Walikuja Watanzania wengi sana kutoka kwenye miji tofauti, kwani kule shoo kama zile ndiyo sehemu ya wao kukutana kwa kuwa kule maisha yao ni tofauti.

“Hakuna mambo ya kutembeleana, watu wako bize na kazi, hivyo kwenye shoo kama zile ndipo wanakutana na kuhisi kama wako nyumbani, wazungu pia wanakuwepo kwa kuwa muziki wanaufurahia hata kama hawaelewi nini kinaimbwa,” anasema.

Anasema walipokewa kistaa, japo walifika na kushangaa shangaa maghorofa na kuona kweli wako Ulaya, lakini shoo hiyo ya kwanza Ulaya ilikuwa ni tukio jingine la kihistoria kwao, walifanya vizuri na kupata nyingine nyingi zaidi, hasa Uingereza.

Washawishiwa kuzamia Uingereza

Anasema katika safari zao za mara kwa mara Ulaya, baadhi ya marafiki zao waliwashawishi wazamie huko wasirudi Tanzania. “Tulishawishiwa sana, tuna marafiki zetu wengine wana miaka hadi 30 kule, walitushangaa kwa nini tumeshafika huko halafu tunarudi Bongo (Tanzania).

“Walituuliza tunarudi Bongo kufanya nini? Wakatushawishi na kutueleza wao wapo kule miaka kibao na maisha yanaendelea, mimi na mdogo wangu tukakataa. “Ukiangalia huku nyumbani sisi kwanza tayari ni mastaa, tuna vitu vyetu tunafanya, lakini ukizamia unaishi kinyume cha sheria, utakosa amani.

“Lakini kubwa kuliko, hata ukiishi Uingereza miaka 20 kwa kuzamia, siku ukikamatwa utachukuliwa wewe na nguo ulizozivaa, tukaona hakuna haja, kwani hata home (Tanzania) kuna maisha tena yanaweza kuwa mazuri ukijipanga kushinda ya kuwa mzamiaji, tukakataa hizo habari,” anasema

Kwa nini wameamua kutoa video hivi sasa

Miezi ya karibuni, Mandojo na Domokaya wametoa video ya wimbo wa ‘Nikupe nini mpenzi’, ambao waliufanya katika audio miaka zaidi ya 20 iliyopita.

“Zamani wengi tuli-heat na audio tu, ikiwamo sisi, ukiangalia albamu yetu ya ‘Taswira’ ambayo kuna wimbo pia wa Nikupe zote ni audio, wakati ule mambo ya video hayakuwa vizuri sana hivyo nyimbo zetu zote tulifanya kazi nusu.

“Nikupe imekuwa na mapokeo makubwa kwa kuwa imewakumbusha watu ‘moment’ tofauti za wakati ule,” anasema. Imetokea tu, halikuwa tukio kama nyimbo zetu nyingine nyingi ikiwamo ile ya ‘Wanoku noku’ ambayo ilitokana na tukio la maskani kwetu.

“Hii tuliitunga kutokana na tabia za jamaa mmoja maskani alikuwa mnoko, tukianza kuimba anatumaindi (hapendi) anasema ni makelele, basi tukawa tunamuimba kama utani bila yeye kufahamu hadi tukatunga wimbo.

“Baadaye Jide (Lady Jay Dee) ni mtu ambaye alikuwa karibu sana na sisi, mumewe Gadner alikuwa meneja wetu, alipousikiliza huu wimbo kwenye gitaa aliupenda akaomba mwenyewe kolabo.

“Kipindi hicho Jide alikuwa wamoto kwelikweli, tukafanya naye kolabo studio kwa Mika Mwamba akaitendea haki,” anasema Mandojo.

Itaendelea kesho akielezea uwekezaji wake.