Masele Chapombe anavyoibuka na staili mpya ya uchungaji

Muktasari:
- Wapo ambao upande huo wa pili bado unagusa sanaa na wengine umetoka nje kabisa ya sanaa. Katika hili ni ngumu kuacha kuwazungumzia baadhi yao kama Jokate Mwegelo ambaye awali alionekana kwenye u-Miss, uimbaji na uigizaji lakini kwa sasa amejikita kwenye siasa.
Dar es Salaam, Waswahili husema safari moja huanzisha nyingine, na hili limejionesha kwa baadhi ya wasanii nchini ambao walianza wakiwa katika upande mmoja wa sanaa na kisha baadaye kuonesha upande wao wa pili.
Wapo ambao upande huo wa pili bado unagusa sanaa na wengine umetoka nje kabisa ya sanaa. Katika hili ni ngumu kuacha kuwazungumzia baadhi yao kama Jokate Mwegelo ambaye awali alionekana kwenye u-Miss, uimbaji na uigizaji lakini kwa sasa amejikita kwenye siasa.
Emmanuel Mgaya ‘Masanja Mkandamizaji’, awali alitambulika kama mchekeshaji na mwimbaji lakini akaonesha upande wake wa pili kuwa mchungaji, Emanuel Mathias ‘Mc Pilipili’ naye ni miongini mwa wachekeshaji ambao wamedondokea upande huo wa uchungaji.
Mbali na hao sasa ni zamu ya mchekeshaji Chrispin Masele ‘Masele Chapombe’ ambaye aliiambia mwananchi kuwa yupo kwenye mpango wa kuwa mchungaji kwani ndani yake amekuwa akiusikia wito huo.
“Najinoa kabisa kuwa mchungaji ndani yangu nina wito, nipo kwenye mchakato wa kuanzisha kitu kinaitwa madhabahu inayotembea, kuna mchungaji pia nitakuwa naye nitakuwa natembea sehemu mbalimbali nawafuata walevi baa, makahaba, na watu wengine wanaotenda maovu kuwahubiria waachane na mambo hayo hata kama nitahubiri kwa njia ya vichekesho lakini nitahakikisha ujumbe unafika,” alisema Masele.
Aidha mchekeshaji huyo ambaye kwa saa amerudi kwenye gemu baada ya kukaa kimya kwa muda mrefu alisema familia na uuzwaji wa kazi zao kiholela ulifanya atulie kufanya kazi ya sanaa.
“Kuna wakati nilitulia kwa ajili ya kujitengeneza kuwa baba bora kwa ajili ya watoto wangu lakini kingine wakati ule kazi zetu zilikuwa zinauzwa kiholela tukawa kama tunafanya kazi kubwa lakini mafanikio hatuyaoni kwa hiyo ikawa inatupa changamoto nayo ilinisimamisha,” alisema
Masele ambaye kwa sasa anaonekana akifanya kazi ya vichekesho na wachekeshaji Stive Mweusi na Mjeshi Kikofia ‘Ndaro’ alieleza kuwa alilazimika kuwatafuta wachekeshaji wao ili afanye nao kazi kwani ni kati ya wachekeshaji wanaofanya vizuri.
“Siku zote kwenye sanaa lazima ukubali wale wanaofanya vizuri Stive, Ndaro, na Chumvi Nyingi ni kati ya wachekeshaji ninaowakubali wanafanya vizuri lakini mimi nikaona nifanye kitu tofauti kwamba wasanii wengi wenye majina kuwasogelea hao vijana huwa wanaona ni dharau.
“Ukiangalia kwenye mitandao kuna watoto wanapata pesa lakini sisi enzi zetu tulichelewa tulikuwa hatutaki hela za kusubiri kwa hiyo wasanii ambao walichipukia kwenye mitandao walikuwa wavumilivu ili wafikie lengo ili ufanye kitu kizuri lazima kushirikiana wale ni wadogo zangu nikaona kwa nini tusifanye kitu nikawatafuta,” alisema Masele.
Ili kwenda sambamba na soko la kidijitali Masele alisema amejipanga kwenda na dunia ya sasa kwani ni ngumu kubishana nayo.
“Wakati wa nyuma mitandao ilikuwa haina nguvu lakini baada ya simu za ‘tachi’ imefanya dunia ibadilike hatuwezi kubishana nayo inavyotaka lazima twende nayo, mimi sitatumia nguvu nyingi kwa sababu tayari wananijua kwa hiyo watanipata tu kirahisi mitandaoni. Mitandao inataka juhudi na ubunifu,”alisema.
Mkataba ilifanya aondoke Mizengwe
“Nilifaya kazi vizuri pale Mizengwe, ITV sikuondoka kwa ubaya mimi mwenyewe nilikuwa na mawazo chanya nikaona kwanini nisijaribu kutafuta wigo mwingine, nilikuwa napenda kufanya kazi na watu tofauti tofauti, nilivyokuwa ITV nilikuwa na mkataba nilikuwa hata siwezi kwenda mbali lazima nifanye kipindi,”alisema.
Utakumbuka kuwa Masele alikuwa akifanya vichekesho kwenye runinga kipindi kiliitwa Mizengwe kilichokuwa kikirushwa ITV.
Siri ya kutendea haki uhusika wa ulevi
Alisema aligundua kuwa anaweza kutendea haki uhusika wa ulevi baada ya kuona kila akiigiza kama amelewa watu wanafurahi.
“Kuna siku nikiwa shule nilijifanya nimelewa nikashangaa watu wanacheka wakajua nimelewa kweli baadaye nikawaambia sijalewa hawakuamini wakaniambia nachekesha basi nikaona hii niishi nayo,” alisema.
Aidha alisema wachekeshaji wengi wa sasa ambao wanaigiza kama walevi wanakwama sehemu kwani wanashindwa kufanya inavyotakiwa. Ambapo kwa upande wake alidai kabla ya kuuvaa uhusika huo alifanya tafiti na kuielewa pombe.
“Mimi nimeingia kwa undani kujua pombe ni nini kabla ya kuigiza ulevi nilifanya ‘research’ kujua pombe ni nini nikapata mtaalamu mmoja akanielekeza akaniambia unapokunywa bia ‘alcohol’ yake inazunguka kwenda nyuma yaani mlevi yeyote wa bia huwa anakosa ‘balance’ ya nyuma, waangalie wengi wanadondoka kwa kukaa,”alisema.
“Mlevi wa pombe kali ‘alcohol’ inazunguka kwenda mbele hana ‘balance’ ya mbele, ndiyo maana wengi wana makovu usoni lakini mtu anayechanganya anakosa ‘balance’ zote ndiyo unakuta kashikiliwa au anabebwa kwa hiyo na mimi nikajua jinsi ya kuyumba kutokana na chupa ya pombe niliyoshika,”alisema.
Anayokutana nayo mtaani kisa uhusika wa ulevi
Masele alisema yeye siyo mlevi kama watu wanavyodhani, licha ya kuwa uhusika huo umekuwa ukifanya watu wengi waamini yeye ni mlevi
“Mimi siyo mlevi lakini, mimi ni binadamu naweza nikanywa nikijisikia sipo sana kwenye ulevi lakini napenda kukaa na watu wanaokunywa pombe kwa sababu maneno mengi yapo baa, watu wananiita baa wananinunulia, ili nisiwaangushe nawadanganya natumia dawa.
“Mwaka huu kuna mtu alinialika kwenye sherehe ya kumbukumbu ya kuzaliwa mtoto wake ili nikamchekeshe nilienda lakini wale watu walidhani mimi mlevi wakaninunulia kreti tatu za bia aisee ilibidi nidanganye natumia dawa hata wao walishangaa kuona nakataa pombe”, alisema.
Hata hivyo, mchekeshaji huyo hakuacha kugusia wachekeshaji wanaovaa matambara na vinyago ili wachekeshe watu.
“Mimi uchekeshaji wangu sijawahi kuvaa matambara kwa sababu watu wanachotaka kucheka siyo nguo zako mimi naweza nikaitwa ata hapa nikaondoka kama nilivyo watu wanamtaka Masele siyo nguo yake je siku ikiibiwa?
“Kuna siku nilimwambia Pembe rungu analotumia litamchosha kwa sababu kuna wakati hakutakuwa na wawindaji watu watatumia bunduki, juzi kati nilifurahi kumuona Senga kavaa macheni kamzidi hadi Harmonize na Diamond, nikasema safi sana tusipende kukariri dunia ya sasa inataka kucheka, uwe mbunifu hawangalii nguo unazovaa, ”alisema.