Matonya: Nimepitia changamoto nyingi, sitasahau hili
Muktasari:
- Kati ya majina hayo, huwezi kukosa la Matonya. Mkali wa nyimbo za kulalamika aliyeteka hisia za mashabiki ndani na nje ya nchi.
Dar es Salaam. Unapoutaja muziki wa Bongo Fleva kokote uendapo yapo baadhi ya majina ni ngumu kuyakwepa. Ni majina yaliyobeba maana halisi ya midundo ya muziki huo tangu kitambo ulipoanza kushika kasi.
Kati ya majina hayo, huwezi kukosa la Matonya. Mkali wa nyimbo za kulalamika aliyeteka hisia za mashabiki ndani na nje ya nchi.
'Vailet' na nyingine nyingi kama 'Anita', 'Siamini', 'Mapito', 'Tax Bubu', 'Spea Tairi' zilimpa mafanikio makubwa kwenye muziki na kuwa miongoni mwa wasanii wa Bongo wanaoingiza mkwanja mrefu kutokana na sanaa.
Ni mmoja wa wasanii walioshawishi wengine kuingia kwenye Bongo Fleva baada ya kuona inalipa na wakati wengi wakidhani amemalizana na kazi ya muziki, mwenyewe anasema yuko kama kawa na hivi karibuni alionekana na prodyuza S2Kizzy.
Msanii huyo mwenye makazi Dar es Salaam na Tanga aliposti picha yake akiwa na mwonekano tofauti na watu kudhani ana mvi kichwani na kwenye ndevu huku akiwa amenenepa. Baadhi walisema ameanza kuzeeka na ameupa mwili nafasi ya kunenepa na kuonekana amechakaa.
Mwananchi lilitaka kujua mengi kuhusu Matonya kuanzia mwonekano wake, kazi zake na maisha yake kwa jumla na alikotoka.
Kuhusu muonekano wake
"Mambo ndiyo yalivyo jamani, ni kweli nazeeka, kuzeeka umri akili inabaki palepale, umri lazima ukubaliane nao siwezi kuukwepa hata kidogo, hivyo sio tatizo kuambiwa nimezeeka au nimeota mvi."
Vipi kuhusu muziki?
"Mimi siko kimya, naendelea kufanya kazi yangu ya muziki kama kawaida, japo kuna shughuli zingine huwa nazifanya mbali na muziki ambazo siwezi kuziweka wazi kwa sababu hayo ni maisha yangu binafsi.
"Muziki wangu sana sana nafanya Nairobi, Kenya, kwa hapa Tanzania huwa nakuja pia kufanya shoo pale ninapohitajika, hivyo sitaacha kufanya muziki, na hivi karibuni nitaachia nyimbo zangu kadhaa ambazo zipo katika maandalizi na zingine zimeshakamilika."
Wimbo gani unaukubali katika nyimbo zako?
"Nyimbo zangu zote nazikubali kwa sababu nimezitunga na kuimba katika ubora mzuri sana na hisia, ila kuna huu wa 'Spea Tairi' ni wimbo ambao nikienda kwenye shoo lazima mashabiki zangu nao waombe kuimba zaidi ya mara mbili na ndiyo maana huwa nafungua nayo kwenye shoo zangu nyingi.
"Kuna kitu ambacho wengi hamkijui, kuna huu wimbo wa Vailet, ni wimbo ambao ulifika Marekani hadi Snoop Dogg katumia kwenye biti wimbo wake mmoja hivi, hii kwangu ni faraja sana.
Unawazungumziaje wasanii wakongwe?
"Nafasi hii naipeleka kwa maprodyuza wakongwe. Kwa kazi waliyoifanya kwenye huu muziki wa Bongo Fleva wanahitaji kuheshimiwa sana, kuna P Funky, Master J, Roy Ayers aliyenitengeneza wimbo wangu wa Vailet, sasa hivi marehemu, Marco Chali na wengine wengi. Huwezi kuitaja Bongo Fleva bila ya hawa watu, tuwape heshima yao na siyo kuwalinganisha nani na nani ni makali."
Makazi ni wapi kwa sasa?
"Nitaishi wapi mimi zaidi ya Dar es Salaam. Tanga ni nyumbani kwetu, ukiniona nipo nchi zingine jua nimeenda kufanya kazi ya muziki au shughuli zangu zingine."
Chanzo cha mafanikio
Anasema mafaniko yake yametokana na kujituma katika kazi na kusikiliza ushauri anaopewa na wadau wa muziki huo, hali inayofanya kuwa kioo kwa wasanii wengine.
Anasema kutokana na muziki, ametembea na kufanya muziki katika nchi mbalimbali za Ulaya, Afrika na kusaidia kumtangaza vyema.
"Niseme tu Matonya ni mmoja wa wasanii wenye mafanikio ambayo kwa njia moja au nyingine ni mfano wa kuigwa, licha ya kupata mafanikio haya, nimepitia changamoto nyingi, lakini nashukuru wadau wa muziki na mama yangu amekuwa msaada mkubwa katika kufikia mafaniko haya.
"Mara nyingi amekuwa akinishauri mambo mengi ambayo yananifanya kuwa katika mstari mnyoofu kwenye shughuli zangu za muziki, licha ya changamoto zinazojitokeza."
Kitu ambacho hawezi kukisahau
Matonya anasema kitu ambacho hawezi kukisahau ni kuhusu tuhuma zilizosambaa kuwa amekamatwa na dawa za Kulevya China.
"Hii tuhuma ukweli ilinisikitisha sana kipindi hicho na sio mimi tu hata mama na familia yangu kwa jumla, mama alikuwa akinipigia simu kila muda akitaka kujua kama ni kweli lakini ilikuwa ni uzushi tu," anamaliza Matonya.