Moni kuisaka Shahada ya Uzamili ndani ya Bongo fleva

Msanii wa hip-hop Bongo, Moni Centrozone

Muktasari:

Msanii wa hip-hop Bongo, Moni Centrozone amesema bado ana ndoto ya kurudi darasani kusomea Shahada ya Uzamili, licha ya muziki kumpatia fedha tangu alipohitimu Shahada mwaka 2015, katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).

Msanii wa hip-hop Bongo, Moni Centrozone amesema bado ana ndoto ya kurudi darasani kusomea Shahada ya Uzamili, licha ya muziki kumpatia fedha tangu alipohitimu Shahada mwaka 2015, katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).

Kauli ya Moni inakuja baada ya hivi karibuni kusema yupo mbioni kutoa albamu yake ya kwanza kisha ataacha muziki na kuendelea na mambo mengine, ikiwemo kurudi darasani kuongeza maarifa.

Rapa huyo alianza kuchukua usikivu wa wengi akiwa na kundi la Centrozone kutokea Dodoma, ingawa kazi zao nyingi zilitoka chini ya Tongwe Records jijini Dar es Salaam ambapo rekodi lebo hiyo iliwasaini. 

 Katika mahojiano na Mwananchi, Moni Centrozone, ambaye ni mwanzilishi wa Majengo Sokoni Music amefunguka mengi kuhusu safari yake ya muziki, elimu, familia na kipi kinakuja kutoka kwake kwa mwaka huu.

Chuo na ajira

Moni anasema kwa miaka zaidi ya nane aliyokuwa kwenye muziki ndiyo ilikuwa ajira yake rasmi, tayari ameelewa mfumo mzima wa ufanyaji kazi na biashara iliyopo ndani yake, hivyo anaona kuendelea kusoma siyo jambo ambalo linashindikana.

 “Pale UDOM nimesoma Geography and Environmental Studies kuanzia mwaka 2012 hadi 2015 nilipomaliza shahada, sasa nataka kuendelea mbele, napenda kujifunza zaidi. Ni moja ya ndoto zangu kufanya Shahada ya Uzamili, Mungu akitujalia uhai lazima vitu vyote tuvikamilishe,” amesema Moni.

Licha ya kutaka kuongeza elimu, Moni anasema bado akili yake haijafikiria kuajiriwa, bado anaona kwenye muziki kuna fursa nyingi ambazo zinaweza kuendesha maisha yake kama ilivyokuwa kwa kipindi chote.

“Tangu nakua ndoto yangu ilikuwa ni muziki, ila kwenda shule na kuhitimu ni kitu ambacho wazazi wanapenda, kwa hiyo nilichokuwa nimehakikisha cha kwanza ni kutimiza ndoto zangu kama msanii, lakini pia kufuata mfumo wa kielimu kama kijana na siyo kwa ajili ya kuajiriwa tu, bali kwa maisha ya kila siku,” anasema.

“Kwa hiyo kipaumbele haikuwa katika kutafuta ajira kwa sababu wakati nasoma tayari nilikuwa natengeneza njia zangu za kuja kuwa mwanamuziki. Hivyo nilianza kurekodi siku za nyuma na kutafuta nafasi nikijua kabisa nitakapomaliza chuo hiki kitu ndicho nitakachokifanya,” alisema Moni.

Alisema muziki una mafanikio kama vitu vingine ambavyo zinaweza kumpa mtu kipato na kuendeleza maisha na watu kuamini wanaweza kufika mbali, ukizingatia sasa hivi kuna biashara ya kuuza muziki mtandaoni, hiyo ni fedha ya msanii ambayo anatakiwa kuifanyia kazi tu.

 “Kwa hiyo kuna sehemu unapata na inatia moyo wa kuendelea kufanya ukiamini kuna nafasi ya kuja kupata zaidi, muziki ni moja ya sehemu ambazo zina mchango mkubwa kwa vijana kwa kweli,” alisema Moni.

Kupata mtoto akiwa UDOM

Moni anasema moja ya mambo yaliyompa nguvu ya kupambana na muziki ni kitendo cha kupata mtoto akiwa bado yupo chuo, ni changamoto iliyomtengeneza Moni huyu tunayemuona hii leo katika Bongo Fleva.

 “Ndiyo nina mtoto wangu nampenda sana, amezaliwa mwaka 2015, ilikuwa ni moja ya mambo yaliyonipa nguvu ya kupambana sana, hali kama ili inavyokukuta wewe kama kijana lazima upambane kuhakikisha kuna kuzaliwa kwa mtoto na malezi yake.

 “Kwa hiyo ni hali iliyotokea na sisi tukawa tumeipokea na kubarikiwa kupata mtoto na baadaye mimi kuja Dar kufanya kazi zangu, kwa hiyo namshukuru Mungu mpaka sasa hivi mtoto amekua na anasoma,” alisema Moni.

Licha ya yeye na mzazi mwenzake kuhitimu masomo vizuri, kwa sasa hawapo pamoja katika uhusiano. Moni anasema ilitokea tu ila kikubwa wanashirikiana katika malezi ya mtoto, amani ipo na ni mambo yaliyopita na sasa wanaganga yajayo.

Safari ya muziki

Rapa huyu safari yake ya muziki ilianza akiwa sekondari ya Dodoma, pamoja na wenzake wawili wakaunda kundi la Centrozone mwaka 2009 na miaka sita mbeleni Moni akaanza kufanya kazi peke yake baada ya kuhamia Dar es Salaam.

 “Kundi la Centrozone limeanza tukiwa bado tupo sekondari na marehemu Langa ndiye alitupa hilo jina, wakati huo alikuwa anakuja kusoma CBE Dodoma, kwa hiyo ndiyo alikuwa ametuona tukiwa mtaani akatuleta pamoja tukawa kundi.

 “Tulibahatika kurekodi na Langa, wimbo mmoja ulikuwa unaitwa ‘Too Real’ na tulifanya pale Tongwe Records na ulitoka mwaka 2010, lakini Ngwea hatukuweza kufanya naye kazi, kipindi anafariki bado tulikuwa tunajitafuta,” alisema Moni.

 Moni anasema kundi lao lilikuwa linakuja Dar es Salaam kurekodi Tongwe Records kisha kurudi Dodoma kuendelea na masomo, baada ya kumaliza shule ndipo nyimbo zikaanza kutoka rasmi redioni.

 “Tulikuwa pale Tongwe Records kama ‘lebo’, ndiyo maana unaona kazi zetu zilianza kutokea pale, baadaye tukaenda studio nyingine lakini Tongwe nimekuwa nikirudi kufanya kazi kwa sababu ni nyumbani kabla hata sijakutana na S2kizzy na Mr. T Touch.

 “Mwaka 2015 nikaanza kutoa kazi zangu baada ya kuona wenzangu wanatamani kuendelea kufanya vitu vingine nje ya muziki, mimi ndiyo nilichagua kufanya kama kazi yangu kabisa, hivyo kila mmoja alishika njia yake ila bado ni familia,” alisema Moni.

Kuacha muziki?

 Je, ni kweli ataacha muziki baada ya kutoa albamu kama alivyosema? Moni anasema amebadili mtazamo wake baada ya ushauri wa watu wengi, anaona bado anaweza kuendelea na muziki na akaendelea na masomo yake.

 “Nafikiri kutokana na hali ambayo imejitokeza juzi bado nitaendelea kuwepo kwenye muziki sababu ya maoni ya watu, wanataka kusikiliza hiyo albamu na kuona kazi zaidi zinakuja, hivyo nitajipa muda zaidi wa kuendelea kufanya kazi.”

Anasema kwa kipindi chote hakuweza kutoa albamu kutokana na kukosekana usambazaji mzuri, ila sasa kuna majukwaa ya kidijitali ya kuuza muziki, hivyo ni wakati wake sahihi wa kuachia albamu.

 “Mwaka huu albamu inatarajiwa kutoka na tayari tunafanya maandalizi kuona itatoka kwa utaratibu gani kama uzinduzi au hafla ya kusikiliza (listening party) kwanza. Rooftop Entertainment na Majengo Sokoni Music zinashirikiana katika kazi hiyo,” alimalizia Moni.

 Utakumbuka miongoni mwa nyimbo za Moni zilizofanya vizuri hadi sasa ni pamoja na ‘Usimsahau Mchizi’ & Roma, ‘Yeah’ ft. Marioo, ‘Lamoto’, ‘My Life’ ft. Jux, ‘Mihela’, ‘Maelekezo Chapter One’ ft. Lil Dwin, ‘Malume’, ‘Cha Mbunge’ ft. Rosa Ree & Kusah na ‘Hold On’ ft. Conboi Cannabino.