Ndani ya boksi: Zamani tulitekwa na bata la 'Lidazi Klabu '
Muktasari:
- Sina habari, natazama kilofalofa totozi zinazokatiza. Kwa miguu, kwa bodaboda, kwa ndinga. Ili mradi tu! si unajua tena mitaa ya Sinza, ilifunga ndoa ya kikristo na pisi mtambuka. Sinza ndiyo sehemu kuna pisi hazina kabila wala asili.
Dar es Salaam, Miaka kadhaa nyuma. Ilikuwa Jumapili. Nipo zangu mitaa ya Sinza, naunguza ini kama siyo maini kwa kumiminika kikali. Mezani jivu jingi, fegi haibanduki kwenye papi za midomo, na mimi ni mtu jamani, nimepitia ujana.
Sina habari, natazama kilofalofa totozi zinazokatiza. Kwa miguu, kwa bodaboda, kwa ndinga. Ili mradi tu! si unajua tena mitaa ya Sinza, ilifunga ndoa ya kikristo na pisi mtambuka. Sinza ndiyo sehemu kuna pisi hazina kabila wala asili.
Zile pisi ambazo wazazi wao walikutana bar. Wakalewa bila kujuana na wakalala pamoja ‘gesti’ bila kutambuana kwa jina wala kazi. Na asubuhi wakaagana freshi. Dada anajikuta ana ujauzito na hajui wa yule wa Kumekucha au Mapambano.
Picha linaanza wengi wao nyakati zile walikuwa wanaishi ‘gesti’. Mara mimba hiyo na dem anakomaa nayo. Mwisho wa siku anapatia uchungu akiwa tungi bar. Mtoto anazalia kwenye taksi ya Mangi wakati anawahi hospitali.
Hapo ndipo anazaliwa mtoto asiye na kabila wala asili. Juu kwa juu na wala siyo kesi. Na mtoto naye anachukua na kujimilikisha tabia za mama yake. Naye anakuwa bidhaa mpya ya wateja, yaani kata mti panda mti. Ndiyo dunia ilivyo wala siyo ajabu.
Basi naendelea kupitisha kooni kinywaji changu. Ghafla simu inaita, kuangalia hivi jina la mpigaji ni mwanangu Guda. Ananichana kwanini nimekaa kibwege Sinza wakati kila kitu kwa mchana ule ‘kinahapeni’ kule ‘Lidazi’? Dizaini kama napata unyonge hivi.
Mwana ananihakikishia usalama upo wa kutosha. Siyo usalama wa kulindwa na watekaji. Hapana! usalama wa kupiga tungi la uhakika na kusepa na totozi za geti au za kona.
Sikutaka kujiuliza zaidi nikalala ubavu. Nikamlipa kisenti chake dada wa pale ‘grosare’ nikasepa. Dakika sifuri naingia zangu ‘Lidazi’. Kutazama hivi mbuga yote ina pundamilia walionana na kuvutia kwa kila kitu. Twanga Pepeta ndiyo ‘wanatesti’ vyombo.
Wakati napiga hatua hivi, nikapigwa na ganzi. Ganzi ya namna hii huwa napata nikiona kitu chenye upekee sana. Kitu kinachoweza kuhamisha hisia zangu kutoka Kimara Bonyokwa mpaka kwa Waefeso kwenye milima ya mizeituni.
Mtoto flani hivi mfupi wa kimo. Rangi ya upekee na lips zenye unyevunyevu muda wote. Yupo na wasanii wenzake, lakini ni yeye peke yake ninayemuona kwa muda ule. ‘Imejini’ Uwoya, Wema, Wolper na Kuku nao wapo, lakini nikamuona yeye tu.
Niliendelea kujipa moyo kuwa nitamuoa mpaka leo ana watoto kadhaa. Siwezi kumtaja kwa sababu ni mali ya mtu tena ya halali, siyo kama Mondi na Zuchu. Na ‘Lidazi’ wakati huo inawaka.
‘Taim’ ambayo Bongo Movie ilikuwa na utawala wake. Waigizaji hawashikiki kwa kila kitu, kuanzia pesa, mikoko, kutafuna pisi kali na wale wa kike wakitafuna pesa za ‘madon’ wa ‘tauni’ kikatili. Walikuwa ‘madikteta’ wa ‘gemu’ na waliweza kwa kiwango cha juu.
‘Gemu walilidikteti’ likawa linafuata kile wanachofanya. Tafrija, na mitoko ya bata bila wao haikuwahi kunoga. Wakati ule waliiteka Kariakoo, waliteka vibanda vya video. Kule Harmonize alianzia kumuona Kajala akiwa rafiki wa Wema.
Waliteka vyombo vya habari na mitaani. Kila bishoo alitamani kuwa Kanumba, Ray, Mlela au Hemed Phd. Kila ‘sista duu’ kitaani ‘aliwishi’ ‘laifu’ la Wema, Uwoya, Johari, Wolper.
Wao walikuwa kielelezo cha ‘Maisha bora kwa kila Mtanzania’. Magogoni pale kukiwa na Jakaya. Wakati Bongo Movie hii leo hutamani ule ‘U-Diamond’. Zamani Bongo Fleva walitamani ‘U-Kanumba’. Ni kwamba waigizaji walikuwa kioo halisi cha kujitazama kama wewe ni bora.
Kuna wakati ‘Lidazi’ ilikuwa Macca ya wasanii. Waigizaji wa filamu, wanamuziki wa dansi na Bongo Fleva. Ungetaka kumuona staa yeyote wa filamu ama wa muziki. Basi ungetimba ‘Lidazi’ Klabu na kumuona kirahisi sana. Nyakati zinaenda kasi kuliko SGR.
Leo ukitaka kumuona msanii kirahisi nenda kwenye ‘peji’ yake insta. Hakuna makutano yao tena. Ikitokea pindi wamealikwa Ikulu ndiyo utawaona kwa pamoja.
Wamesambaratika kama nywele za Bush Man, yule staa wa filamu ya ‘Godi Masti Bii Krezi’. Wasanii wana umoja kweli kwa mmoja mmoja, siyo kama nyakati zile.
Wikiendi iliyopita eneo hilo walilokutana kwa ajili bata zamani. Wamekutana kwa ajili ya kumbukizi ya waliokuwa wanakutana nao pale pale kwa ajili ya bata. Wenzao wametangulia mbele za haki. Ni jambo zuri sana wamefanya na ikiwa inafanyika kila mwaka itakuwa vyema zaidi.
Nilifika pale wikiendi iliyopita. Na mwana yule yule, lakini safari hii siku haikuwa njema kwetu baada ya kuoana na picha na Albert Mangweha. Kumbukizi yetu iliturudisha nyakati zilezile za kizazi kile cha bata hakuna kulala. Ilikuwa ‘ishu’ flan hivi tamu sana. Wametisha.