Ommy Dimpoz na rekodi yake kwenye Bongo Fleva
Muktasari:
- Baada ya jina lake kuwa kubwa ndipo akaanzisha Poz kwa Poz (PKP) Entertainment, lebo iliyosimamia kazi zake lakini pia ikamsaini Nedy Music aliyetoka kupitia wimbo wake, Usiende Mbali (2016) ambao pia alimshirikisha Dimpoz mwenyewe.
Dar es Salaam. Je unafahamu kuwa Ommy Dimpoz ndiye msanii pekee Bongo kushinda TMA mara mbili mfululizo katika kipengele cha Wimbo Bora wa kushirikiana akishinda 2012 na 2013 kupitia ngoma zake 'Nai Nai' na 'Me and You' alizoshirikiana na Alikiba na Vanessa Mdee.
Baada ya jina lake kuwa kubwa ndipo akaanzisha Poz kwa Poz (PKP) Entertainment, lebo iliyosimamia kazi zake lakini pia ikamsaini Nedy Music aliyetoka kupitia wimbo wake, Usiende Mbali (2016) ambao pia alimshirikisha Dimpoz mwenyewe.
Kwa muda mfupi wimbo huo ukakamata chati za vituo vikubwa vya televisheni kimataifa kama MTV Base, Sound City, Trace Urban n.k, na hadi sasa ni wimbo wa tatu wa Nedy uliofanya zaidi YouTube ukiwa umetazamwa mara milioni 1.7.
Ila kufuatia Dimpoz kusainiwa RockStar Africa (2017) na baadaye Sony Music Entertainment Africa, huo ukawa mwanzo wa Nedy Music kuwa mbali na PKP na hatimaye kuachana nayo kabisa.
Tetesi za kuachana zilianza alipoachia wimbo, One and Only (2018) akiwa na Ruby, video yake ilitoka bila nembo (logo) ya PKP ndipo maneno yakaanza ila mwaka mmoja kabla Dimpoz alidai kuwa amemtafutia Nedy menejimenti nyingi.
Wimbo huo wa kwanza wa Nedy Music nje ya PKP ulifanya vizuri ukishinda All Africa Music Award (AFRIMA) 2018 katika kipengele cha African Fans Favourite, tuzo zilizofanyika nchini Ghana.