Prime
Sakata la wasanii, mashabiki linavyozidi kuchukua sura mpya
Muktasari:
- Kwa mujibu wa Majizzo, kuna uwezekano kundi fulani la wasanii lilipitiliza au kujikwaa sehemu pindi walipochagua upande wa kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Dar es Salaam. Kutokana na kilichotokea kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu na Oktoba 29, 2025 kipindi cha uchaguzi mkuu kumesababisha mvutano na maoni mseto kati ya wasanii na baadhi ya mashabiki wao kudai kutengwa, kudharauliwa na wasanii, suala hilo likichukua sura mpya baada ya Mkurugenzi wa EFM Radio, Francis Ciza 'Majizzo' kujitokeza na kuwaombea msamaha wasanii.
Kwa mujibu wa Majizzo, kuna uwezekano kundi fulani la wasanii lilipitiliza au kujikwaa sehemu pindi walipochagua upande wa kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Hata hivyo, anaamini wasanii kuchagua upande na hata kushiriki kampeni sio kosa kwa sababu ni sehemu ya wao kujipatia kipato, hivyo mashabiki pale wanapohisi hawakutendewa sawa wasamehe ili kuikoa tasnia.
"Kwangu mimi naona ni msanii ambaye ameadhibiwa kwa kosa la kujitafuta riziki, kwa kukosa la kwenda kutafuta kipato chake. Kumbuka hawa wasanii walikuwa kwenye majukwaa ya siasa wanalipwa, kwa hiyo mtu ameenda kujitafutia riziki sisi tunamwadhibu," amesema.
"Kuna wakati wanakosea, wana maneno ya kukera na kuna wakati wanapitiliza. Kibinadamu ni vizuri kukiri mimi kama kaka, kama mshikadau wa sanaa nawaombea radhi kwa niaba yao ili tasnia isonge mbele," alieleza Majizzo.
Kauli yake imekuja baada ya kuwapo vuguvugu la mashabiki katika mitandao likidai halitaunga tena mkono kazi za baadhi ya wasanii nchini kwa kile wanachotaja kama kushindwa kutekeleza wajibu wao kwa jamii!
Huu umekuwa ni mjadala mkubwa ukihusisha mashabiki, wasanii na hata wadau, lengo likiwa ni kurekebisha na kuwa na hatima itakayozingatia maslahi mapana ya pande zote mbili.
Mkongwe wa Hip Hop nchini Mr II Sugu ambaye alianza kuvuma katikati mwa miaka ya 1990, akijibu maoni ya Majizzo alieleza kuwa suala la wasanii kukataliwa na mashabiki halipo kisiasa bali ni wao wenyewe kujisahau.
"Ieleweke, suala la hawa wasanii kukataliwa na jamii sio la kisiasa, ni suala la wao wenyewe kukosa uzalendo kwa Watanzania, ni zaidi ya itikadi za vyama... Vijana walijisahau sana, na hayo ndiyo madhara ya kutokujali historia," alisema Sugu na kuongeza.
"Tuliwaanzisha huu muziki kwenye mazingira magumu sana sana; hatukueleweka kabisa mwanzoni, tukihusishwa na uhuni na dawa za kulevya. Tukafanya juhudi kubwa na za makusudi kuukubalisha kwa jamii mpaka Watanzania wakaukubali na kuufanya kuwa muziki wao".
"Ukawa fahari ya Watanzania popote walipo duniani. Mpaka tunafika hapa, wasanii wasiojielewa wakautumia tena dhidi ya Watanzania kwa kuwadharau, kuwachamba, kuwabagaza na kuchangia kuwaumiza," alieleza.
Naye rapa Nay wa Mitego amedai ubinafsi wa baadhi ya wasanii kwa kujali maslahi yao pekee bila kutazama upande wa pili unaowapa hiyo nguvu ya ushawishi, ndio umefanya mashabiki kuchukiwa na kususiwa kazi zao.
"Mwaka huu mwanzoni niliwashauri wasanii wenzangu kujitoa kwa wananchi wetu hata mara moja tu kwa mwaka kuwasemea kwa sababu wao ndio mabosi wetu wa kwanza na wenye hatima ya nguvu, thamani na ushawishi tulio nao."
"Nilitoa mifano hai kabisa ya wasanii wa nje ya Tanzania na kwa majirani zetu jinsi wanavyosimama na wananchi wao yanapotokea ya kutokea. Tatizo kubwa la mastaa hapa nyumbani ni ubinafsi na kusahau kuwa mabosi zetu ni hawa wananchi".
"Sasa mabosi zetu wameamua kutuonyesha kwamba wao ndio wanaotupa jeuri, na maisha mazuri tuliyonayo ni kwa sababu yao. Mimi siwalaumu Watanzania; wana haki ya kuendelea na walichoamua hadi hasira zao zitakapoisha. Nadhani baada ya hapo somo litakuwa limetuingia sisi wasanii wote, na tutakuwa tunaongea lugha moja, wananchi na wasanii," alieleza Nay.
Kwa upande wake Harmonize, mwanzilishi wa Konde Music Worldwide, amesema anaona maoni ya mashabiki mtandaoni lakini huu sio wakati wa kumsaka mchawi ni nani kwa sababu hakuna aliyetegemea yaliyotokea.
"Naona baadhi ya watu wanasema 'hatutakuja kwenye show' sijui nini. Mimi nikiona watu wanalalamika hivyo najua tumefikia hatua ambayo kama taifa hatukuwahi kuifikia, kwa hiyo hatujui mchawi ni nani wa kumlaumu".
"Hivyo kilichotokea hakuna aliyekuwa anajua kitakuja kutokea, kwa hiyo kama taifa ni muda wa kuungana pamoja, na kilichotokea kila mmoja kimemfunza kwa namna yake," alisema Harmonize na kuongeza.
"Ni suala tu la kukaa kimya kila kitu kitarejea katika uhalisia wake, sio muda wa kukaa na kuanza kulaumiana. Mimi nikiona mtu anasema 'sitakuja kwenye show yako, sitasikiliza wimbo wako', nachukulia kawaida kwa sabubu hali iliyopo inachanganya," ameeleza.
Akizungumza na Mwananchi Mkuu wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa), Dk Herbert Makoye amesema siyo kosa msanii kushabikia chama chochote cha siasa kwani katiba inaruhusu.
“Katiba yetu inaruhusu kila mmoja kuamua, kwa hiyo mwananchi yeyote kasoro taaluma chache tu. Wasanii wanawalaumu bure ni kama hawafahamu haki zao kama raia hili litapita ni kawaida.
“Kila mtu ana haki yake awe mlengo gani kama mwananchi ilimradi asivunje sheria kukiwa kuna vyama vingi ni kuvumiliana tukitoka kwa wasanii watafuata wa taaluma nyingine mwisho inakuwa chuki,”amesema Makoye.
Mbali na hayo kwa upande wake mwanamuziki mkongwe nchini John Kitime akizungumzia hilo amesema haya yametokea kwa sababu upande wa serikali na wasanii wote wana matatizo.
“Kipindi cha nyuma hili halijawahi kutokea. Upande wa serikali una matatizo na upande wa wasanii uchawa umepitiliza. Enzi zetu hakukuwa na machawa ungeonekana mnafiki upande wa serikali walikuwa wanaheshimu wasanii wote.
“Sasa hivi unakuta kiongozi anaenda Songwe anachukua msanii kutoka Dar anaenda naye. Wakati hata Songwe kuna wasanii wa huko. Tulifanya utafiti tukakuta wanalalamika kuwa wasanii wanapendelewa,” amesema.
Amesema kutokana na hayo wasanii wanatakiwa kubeba hizo lawama kama ambavyo kuna upendeleo.
“Ukitaka kuwaambia jamii hadi wakuelewe ni lazima ufanye kitu. Haya ni matokeo ya kutengeneza kuwa na kundi maalumu kwa hiyo wanyamaze. Sanaa nyingine zitaendelea lakini Bongo Movie na Bongo Fleva inaweza kubadilisha watakuja wasanii maarufu wapya hakutakuwa na gap,” amesema Kitime.