Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Shabiki afufua kesi, amshtaki Cardi B kwa kumpiga na maiki

Muktasari:

  • Cardi B, mkali wa kibao, I Like It (2018), mnamo Julai 2023, video iliyosambaa mtandaoni ilimwonesha akirusha kipaza sauti chake kwa shabiki aliyemmwagia kinywaji wakati akiimba wimbo wake, Bodak Yellow (Money Moves) (2017).

Marekani. Rapa wa Marekani, Cardi B (32) ameshtakiwa kwa kosa la shambulio la kupiga kufuatia tukio la kumpiga na kipaza sauti (maiki) mwanamke mmoja miaka miwili iliyopita kwenye show yake iliyofanyika katika ukumbi wa Drai’s Beachclub huko Las Vegas.

Cardi B, mkali wa kibao, I Like It (2018), mnamo Julai 2023, video iliyosambaa mtandaoni ilimwonesha akirusha kipaza sauti chake kwa shabiki aliyemmwagia kinywaji wakati akiimba wimbo wake, Bodak Yellow (Money Moves) (2017).

Tukio hilo liliripotiwa kwa polisi wa eneo hilo na uchunguzi mfupi wa jinai ulifanyika lakini waliamua kutofungua mashtaka yoyote.

Sasa mlalamikaji ambaye ni mkazi wa Cleveland, Ohio, anayetumia jina la bandia katika shauri hilo akitambulika kama Jane Doe, ameibuka.

Kwa mujibu wa nyaraka za kisheria, Doe anadai kuwa rapa huyo hakuwa na sababu ya kukasirika kiasi hicho aliporusha kinywaji chake sababu ndiye aliwaomba mashabiki wammwagie maji ili kumsaidia kuupoza mwili kutokana na joto kali.

“Washiriki kadhaa wa show hiyo walijibu ombi hilo kwa kumwaga na kurusha vinywaji kuelekea jukwaani, vingi vikiwa vimefika kwa Cardi B na maeneo ya karibu ya jukwaa.” Waliandika mawakili wa Doe na kuongeza.

“Mlalamikaji, kwa kuzingatia mazingira yaliyowekwa kwa maneno ya Cardi B pamoja na vitendo vyake, na kwa namna ile ile kama mashabiki wengine, alimwagia sehemu ndogo ya kinywaji chake kuelekea kwa Cardi B. Kwa ghadhabu na bila onyo lolote, Cardi B alirusha kwa nguvu kipaza sauti chake moja kwa moja kwa mlalamikaji.”

Doe anasema alipata majeraha ya kimwili na kiakili kutokana na kupigwa na kipaza sauti hicho, na alikumbana na unyanyasaji na aibu baada ya tukio hilo kusambaa mtandaoni. Msongo huo ulizidi baada ya kipaza sauti kilichotumika kumuumiza kuuzwa kwa Dola 90,000.

Pia mwanamke huyo anaishtaki Drai’s Beachclub kwa uzembe, akidai walishindwa kuzuia au kutuliza hali hiyo. Anadai uongozi wa ukumbi huo ulipaswa kujua Cardi B anaweza kuleta vurugu kwa kuwa tayari alikuwa amemtupia DJ kipaza sauti kwenye tukio lingine usiku wa jana yake.

Mwakilishi wa Doe anasema wanatumia jina la bandia kwa sababu mlalamikaji anapitia changamoto za afya ya akili zinazotokana na tukio hilo na hataki kutambulika kwa kuogopa mashambulizi zaidi kutoka kwa umma.

Mwanamke huyo mwenyewe amesema katika tamko lake kuwa anatafuta haki kwa nia ya kumwajibisha Cardi B kwa vitendo vyake, kwa kuwa hakuna mtu maarufu aliye juu ya sheria.

Hata hivyo, timu ya mawakili wa Cardi B wamepuuza shauri hilo na kulielezea kama jaribio la wazi na la kusikitisha lenye lengo la kutaka fedha kwa njia ya hila.

“Polisi wa Las Vegas pamoja na Ofisi ya Mwendesha Mashtaka huko Clark walishafunga kesi hii zamani kutokana na ukosefu wa ushahidi wa kutosha. Lakini inaonekana fursa ya kutaka kupata fedha kutoka kwa mtu maarufu ni kubwa mno kwa baadhi ya mawakili walio tayari,” amesema wakili wa Cardi B, Drew Findling.

Hayo yanajiri wakati albamu ya pili ya Cardi B, Am I the Drama? (2025) imepangwa kutolewa Septemba 19, 2025 chini ya Atlantic Records baada ya kusubiriwa kwa muda mrefu.

Hata hivyo, albamu hiyo yenye nyimbo 23, itajumuisha vibao vilivyotangulia kutoka hapo awali kama WAP na Up, pamoja na wimbo wake mpya alioutoa hivi karibuni, Outside.

Cardi B alianza kuvuma kimuziki baada ya kuachia albamu yake ya kwanza, Invasion of Privacy (2018) iliyofanya vizuri na kumfanya kuwa msanii wa kwanza wa kike kushinda tuzo ya Grammy katika kipengele cha Albamu Bora ya Rap.

Mnamo Mei 2023, Cardi B alifanikiwa kuwa na nyimbo nne ambazo zimesikilizwa (streams) zaidi ya mara bilioni 1 katika mtandao wa Spotify, hivyo kuendelea kung’aa ndani ya ‘Billions Club: The Series’ ya Spotify, ikiwa ni rekodi yake nyingine kubwa.