Prime
Simulizi msanii wa Ramadhani Brothers alivyokosa 'Visa'

Mhariri wa burudani wa gazeti la Mwananchi, Christina Joseph akifanya mahojiano na kundi la Ramadhani Brothers
Februari 19, 2024, historia iliandikwa baada ya kundi la wasanii wa Sarakasi, Ramadhani Brothers, linaloundwa na vijana wawili Fadhili Ramadhani na Ibrahim Jobu kuwa Watanzania wa kwanza kushinda mashindano ya kusaka vipaji American Got Talents: Fantasy League nchini Marekani na kujinyakulia dola 250,000 (Sh milioni 637.5) pamoja na tuzo.
Vijana hawa ambao wanafanya sarakasi aina ya Acrobatic wameiambia Mwananchi kuwa wao siyo ndugu wa damu kama watu wengi wanavyodhani badala yake ni marafiki wa karibu.
Wakizungumza na Mwananchi wamesema kuwa safari yao ya kufanya kazi pamoja kwenye sarakasi ilianza mwaka 2017, baada ya kukutana Msasani Club kwenye kempu ya mchezo huo.
“Kuna siku nilisema ngoja niende Msasani nikaangalie vijana wenzangu wanafanya nini, siku ambayo nilifika ndipo nikakutana na mwenzangu Ibrahim, ilikuwa baraka na upendo, tukaona tukishirikiana tutafanya jambo kubwa siku za usoni, nikamwambia mwenzangu kwa mara ya kwanza tumekutana naona tutengeneze kitu ambacho kitakuja kuleta matunda baadaye, lakini kwanza tujikite kwenye mazoezi, basi kuanzia hapo tukaanza kufanya mazoezi pamoja”. Amesema Fadhili.
Fadhili aliendelea kusema kuwa michezo ya sarakasi ipo mingi lakini wao waliamua kufanya kitu cha tofauti ambacho kitawatambulisha ulimwenguni na ndipo wakapata wazo la ‘head to head balance’.

Balozi awapa mchongo
Wanaeleza kuwa walipata mualiko wa kwenda Marekani kwa ajili ya mashindano hayo mwaka 2021, baada ya American Got Talents (AGT), kuona video yao kwenye mtandao wa Facebook ndipo wakapewa nafasi ya kushiriki lakini hawakufanikiwa kwa sababu ya mmoja wao alikosa visa.
Matumaini ya kwenda Marekani yalirudi tena mwaka 2022, baada ya kukutana na Balozi wa Marekani nchini Tanzania wakati huo Don J. Wright katika tamasha moja walilotumbuiza Masaki na ndipo safari yao ya Marekani ikaanza hadi kunyakua ushindi.
“Kulikuwa na tamasha moja linafanyika maeneo ya Masaki watu wengi walikuja kuangalia, wakiwemo wakubwa kwa sababu siku hiyo wasanii wengi walikuwa ‘wanapafomu’ ikiwemo sisi, cha ajabu siku hiyo balozi wa Marekani alikuwepo alivyoona ‘pafomansi’ yetu alivutiwa sana akaomba kuonana na sisi kimaongezi.
Tukaenda tukamueleza tatizo letu ambalo tulikutana nalo siku tumeenda kuomba visa kwa mara ya kwanza mwenyewe alishangaa kwamba tunakipaji lakini tumekosa visa akauliza hicho ndiyo tumepanga kwenda kukionesha Marekani, akatupa ‘business card’ yake akasema tukienda ubalozi tumpigie simu, ilibidi twende tena bila maswali tulipatiwa visa safari ya kwenda Marekani ikaanzia hapo,” anasema Ibrahim.
Baada ya kufanikiwa kupata visa wanaeleza wakaambiwa tena Februari 2023, wanahitajika kwenda kwenye mashindano ya America Got Talent Season 18 ambapo walifanikiwa kushika nafasi ya tano kati ya washiriki zaidi ya 600.
Hata hivyo, mwaka 2024, katika mashindano hayo hayo wakiwa tayari wamejikoki upya kwa mashindano wakiwa na staili mbalimbali za mchezo huo kama vile, kupanda ngazi wakiwa wameziba macho iliwashangaza wengi na kufanya waibuke kidedea kwa kushika namba moja.
Kilichofanya mmoja kukosa visa
Wanasema mwaliko wao wa mwanzo Marekani ulikuwa mwaka 2021, licha ya kufanya mazoezi ya kutosha lakini walipofika ubalozi wa nchi hiyo, Ibrahim alikosa visa kutokana na kutokuwa na historia ya kusafiri nje ya nchi.
Wanasema baada ya kukosa visa ya Marekani walifanikiwa kupata mwaliko wa Australia ambako walienda kwenya mashindano ya Australia Got Talent huko hawakufanikiwa kushinda lakini walipata mialiko mingi baada ya watu wengi kuvutiwa na ‘pafomansi’ zao ambazo walizionesha hapo.
Ramadhan Brothers wanasema ishu ya kukosa visa, ilikuwa moja kati ya changamoto ambayo wamewahi kukutana nazo, huku changamoto nyingine wakizitaja kama vile misuli kukaza, kushtuka kwa viungo na uchovu.

Sarakasi ni rahisi kwa wanawake
Wanasema sarakasi wanayofanya wao ya kubebana kwa kutumia kichwa ni ngumu inahitaji umakini wa hali ya juu, akili na mazoezi. Lakini mchezo huo kwa wanawake wanasema unaweza kuwa rahisi zaidi kwa sababu ndiyo wabebaji wazuri wa ndoo kichwani tena wakiwa wameachia.
“Mchezo wa kubebana kwenye kichwa wanawake ni wachezaji wazuri kuliko sisi wanaume, kwa sababu wao ndiyo hubeba ndoo kichwani za maji na wanaachia, wanakuwa na balansi shida ni kwamba wanawake wengi huogopa kudondoshana lakini wao ndiyo wazuri kwa mchezo huu.”
Ngoma bado mbichi kwenye ushindi wao
Licha ya kuwa wakali hawa wamefanikiwa kuondoka kidedea kwenye mashindano hayo, bado wana mtihani mzito wa kutetea ubingwa wao na kuhakikisha wanalinda nafasi yao.
Wanasema huo ndiyo mtihani mzito walionao kwa sababu wanaenda kukutana na wababe wote waliowahi kushinda miaka kadhaa ili kumpata mbabe zaidi.
“Mwezi Septemba tunakwenda ‘kudifendi taito’ kwamba tumeshashinda, lakini sasa tunakwenda kushindana na washindi wengine ambao wamewahi kushinda haijalishi wanatoka wapi hapo tunatakiwa kugombania taji lisichukuliwe, yaani asitokee mtu mwingine akatushinda, sasa tukishinda hapo ndiyo tutakuwa tuna mtihani mkubwa zaidi huku mbele,” amesema Ibrahim.
Amesema wanatakiwa kufanya mazoezi makali na kubuni vitu vipya, ili kufanikisha vitu hivyo wanahitaji ‘sapoti’ kubwa kutoka kwa taasisi mbalimbali, serikalini na kwa watu binafsi, pamoja na kuweka rekodi ya dunia (Guinness World Records).