Siri iliyopo kwenye matamasha ya muziki
Muktasari:
- Kwa hapa nchini yapo matamasha mengi ambayo yamekuwa yakiinua wasanii na wakuwakutanisha na mashabiki wao kama lile la Fiesta Festival, Nandy Festival, Kizimkazi Festival, Wasafi Festival, Muziki Mnene, na hata Tulia Talent Competition
Matamasha ya burudani yanaonekana kuwa chachu katika tasnia ya muziki kwani yamegeuka sehemu ya mageuzi katika tasnia hiyo kwenye kuleta ushindani mkubwa na kutoa fursa za kipekee kwa wasanii kujipatia umaarufu, kujenga mtandao wa ushirikiano, kuonesha vipaji vyao na hata kuimarisha uhusiano kwa mashabiki wao.
Kwa hapa nchini yapo matamasha mengi ambayo yamekuwa yakiinua wasanii na wakuwakutanisha na mashabiki wao kama lile la Fiesta Festival, Nandy Festival, Kizimkazi Festival, Wasafi Festival, Muziki Mnene, na hata Tulia Talent Competition.
Kupitia matamasha hayo ambayo baadhi hufanyika kila mwaka, wasanii hujikuta wakipata nafasi ya kuonesha vipaji vyao kupitia majukwaa hayo. Na hapo ndipo huitumia sehemu hiyo kujitambulisha kwa mashabiki wapya na kuwavutia. Lakini hata kwa wasanii wapya huyageuza kama njia ya kukuza majina yao.
Aidha matamasha hayo ya muziki huwa ni sehemu ya kukutanisha wasanii na wadau mbalimbali, ikiwa ni pamoja na waandishi wa habari, waandaji, na hata wawekezaji. Mahusiano haya yanaweza kuwa na manufaa makubwa kwa wasanii kwani yanaweza kupelekea fursa za kufanya kazi na watayarishaji wengine, kuandaa mikataba ya kurekodi, au hata kupata udhamini kutoka kwa kampuni za biashara.
Pia yanatoa fursa kwa wasanii kujenga uhusiano wa karibu na mashabiki wao. Kwa kuwaona uso kwa uso na kuwasikiliza moja kwa moja, mashabiki wanapata uzoefu wa kipekee ambao hauwezi kupatikana kupitia redio au video za muziki. Hii inasaidia kuongeza mashabiki wa kudumu.
Katika matamasha hayo ya muziki yapo ambayo mara nyingi huandaliwa kwa madhumuni maalumu, kama vile kuchangisha fedha kwa ajili ya misaada, au kusherehekea. Hii inasaidia wasanii kuhusika katika shughuli za kijamii na kujenga picha nzuri kwa jamii.
Kupitia Taasisi ya Tulia Trust ambayo huandaa matamasha ikiwemo la Talent Competition hadi zaza limenufaisha zaidi ya vijana 200 kupitia matamasha mbalimbali na kuweza kukuza vipaji vyao.
Akizungumza na Mwananchi Ofisa Habari na Mawasiliano wa Taasisi hiyo Joshua Mwakanolo ametaja moja ya tamasha linalokutanisha makundi ya vijana ni pamoja na Tulia Talent Competition ambalo uratibiwa na kufanyika kila mwaka kwa lengo la kuibua vipaji mbalimbali vya wasanii.
“Tumeweza kuibua vipaji kwa vijana ambao wamepata nafasi ya kuchukuliwa na wasanii wakubwa na kupata fursa ya kujiajiri na kuajiriwa kupitia vipaji vyao.
“Kupitia matamasha hayo tumekuwa na mwitikio mkubwa wa ushiriki tangu tumeanza miaka kadhaa imepita tumeibua vijana zaidi ya 200 katika vipengele mbalimbali ikiwemo ngoma za asili,”amesema.
Mwakanolo amesema katika kuhakikisha wanafikia malengo yao wamekuwa wakiwafuatilia vijana hao kujua maendeleo yao na kutatua changamoto ikiwemo fursa za ajira na mbinu za kuwekeza kupitia vipaji vyao,” amesema.
Ameongeza kuwa msimu wa 2023 msanii Diamond Platnumz (Naseeb Abdul) alikuwa miongoni mwa wasanii walioweka kambi katika Tamasha la Tulia Street Talent competition 2023 na kuahidi kuchukua baadhi ya wasanii walioibuka kinara katika mashindano hayo.
Naye mmoja wa wanufaika wa mashindano hayo kwa mwaka huu 2022 Julias Nyandindi (J Fish) amesema alishiriki Tulia Talent competition 2022 na kuwa mshindi wa tatu.
Amesema baada ya hapo alianza kupata mwanga kwenye sanaa ya muziki na kupata mialiko mbalimbali ikiwemo kushiriki kutumbuiza kwenye VIP ya ukumbi wa Bunge.
“Kwenye sanaa awali nilikuwa kama naigiza baada ya kushinda kwenye tamasha hilo nimeweza kupata ‘connection’ kubwa zinazoniingizia kipato na kuweza kuendesha maisha yangu,”amesema.
Utakumbuka kuwa mwaka jana tamasha hilo la kuwatafuta vijana wenye vipaji lilihusisha washiriki zaidi ya 200 huku likidumu kwa siku tatu katika vipengele kama vila uchekeshaji, mitindo, uimbaji na unenguaji mmoja wa majaji waliokuwepo ni Kipepeo Mweusi ‘Mwasiti Almas’.
Ambapo baadhi ya washindi katika kipengele cha dansa walishinda Swax Dancers (Sh2,000,000),Waarabu Dancers (Sh1,500,000) na The Real Kings Dancers (Sh1,000,000) huku upande wa wachekeshaji walishinda Musa Piliton (Sh1,000,000) Eliah Mbilinyi (Sh 700,000) na Jebon Patrick (Sh 500,000).
Mbali na Tamasha hili mwanamuziki wa singeli ambaye amekuwa akionekana kwenye matamasha mbalimbali nchini akionesha umahiri wake kwenye muziki huo Aman Hasan ‘Man Fongo’ amesema kuwa matamasha hayo yanapaswa kuongezeka kwa wingi nchini kwani yanawakutanisha na mashabiki wao moja kwa moja.
“Matamasha yanatukutanisha na watu wetu ambao hatukonao karibu yanapokuwa matamasha mengi kama vile Muziki Mnene au Komaa Concert yanatukutanisha karibu na wadau wetu kukiwa na matamasha mengi yatatoa fursa kwa wasanii kwa ukubwa zaidi.
“Kawaida yamekuwa yakitunufaisha katika upande wa kujipatia kipato maisha yanaenda, siyo kama msanii anapata pesa nyingi lakini kikubwa kule ni kukutana na wadau na kupata kipato, faida ya kifedha kubwa wanapata waandaaji kama ikitokea nikiandaa tamasha langu nitapata faida kubwa kwa kuwa nitakuwa siyo mwalikwa ni muandaaji,”amesema mkali huyo wa singeli
Ikumbukwe Man Fongo ni kati ya wasanii waliotumbuza kwenye tamasha la Kizimkazi ‘Usiku wa Singeli’.Mbali na hayo kwa upande wa Nandy Festival mwanamuziki Nandy tayari amewaweka mashabiki wake katika mkao wa kula kulisubiri tamasha hilo kwa mwaka huu 2024 huku kauli mbiu yake ikiwa ‘Tupishe’
Kwa upande wa Wasafi Festival ilifanyika mwaka jana 2023 kwa 2024 mashabiki bado wanasubiri kuona ujio wao mpya.