‘Valentine day’ na fursa za biashara

Dar es Salaam. Ni siku ya mavuno kwa wafanyabiashara, ndivyo unavyoweza kuielezea siku ya Valentine inayoadhimishwa na wapendanao.

 Siku ya wapendanao ambayo chimbuko lake ni karne ya tatu huko Roma, huadhimishwa Februari 14 ya kila mwaka ikiwa ni ishara ya wapendano kuthaminiana huku ikiambatana na shamrashamra za kila aina.

Mbali na kununuliana zawadi mbalimbali zikiwemo kadi na maua, baadhi ya wapendanao hutoka kimatembezi na kula vyakula kwenye migahawa na vinywaji mbalimbali ili kuimarisha mapenzi yao.

Hali hiyo imekuwa ikiibua fursa za biashara kwa wauza zawadi, mapambo na vyakula na vinywaji hivyo.

Kutokana na hilo wafanyabiashara wameonekana na nyuso za furaha, wengi wao wakisema huwa siku hiyo huja na fursa kemkem za kibiashara.

Akizungumza na Mwananchi, Mary Florance anayeuza maua eneo la Mbuyuni jijini hapa, alisema katika biashara ya maua fursa ya uchumi inaongezeka zaidi ikiwa inakaribia sikukuu ya wapendanao.

“Watu wengi wamekuwa na tabia ya kuagiza mzigo kabla ya siku husika, wanatoa hela kabisa na kusubiria maua yao yafike,” alisema.

Mary alisema kipindi cha Valentine amekuwa akiingiza fedha nyingi kutokana na mwitikio wa watu katika siku hiyo.

“Unakuta naweka mzigo wa maua mekundu ‘red flowers’ ambayo kwa kawaida huuzwa Sh7, 000 na watu wananunua mpaka yanakwisha,” alisema.

Mary pia anafafanua kuwa mbali na faida hizo za kiuchumi wanazozipata wafanyabiashara wa maua, kwa sasa maua hayo ‘fresh’ yameadimika.

“Maua kwa sasa yanapatikana Kenya, tofauti na zamani watu wengi wamekuwa wakiyafuata Kilimanjaro au Arusha, nafikiri Serikali iliangalie hili kwa jicho la tatu,” alisema.

Kwa upande wake, Miraji Jaffary ambaye ni mfanyakazi katika moaj ya migahawa jijini hapa alisema wakati wa sikukuu hupunguza bei ili wapate wateja wengi zaidi.

“Tunakuwa tunatoa ofa kwa mwezi mzima, jambo ambalo ndani ya mwezi wa pili tunajipatia fedha nyingi kwa kuwa wateja huongezeka,” alisema Jaffary.

Naye dereva wa teksi mtandao, Omary Shabani amesema inapokaribia sikukuu ya wapendanao, huwa anapata safari nyingi tofauti kwa kuwa watu hupenda kuwapeleka wapendwa wao sehemu tofauti.

“Kwa siku nalala hata na Sh200, 000 au 300, 000, kila ifikapo mwanzoni mwa mwezi wa pili, safari huwa ni nyingi, huwa nafurahi sana maana najua huo ndio mwezi wa kuongeza uchumi wangu,’’ alisema.

Neema Msella, mfanyabiashara wa kupeleka bidhaa kutoka sehemu moja kwenda nyingine, alieleza kwamba katika kipindi hicho huwa anapata oda tofauti ya bidhaa mbambali tofauti na miezi mingine.

“Kusema kweli huwa natamani sikukuu ziwepo mara kwa mara hususani hii sikukuu ya wapendanao...huwa napata oda zaidi ya 50,” alisema Msella.

Biashara pia huchanyanya kwa Grace Mzava, muuza kadi katika maeneo ya Buguruni aliyesema kila ifikapo Februari na na Desemba hupata wateja wengi wa kadi.

“Imekuwa ni kama desturi katika ofisi yangu watu wengi huja kuulizia kadi mwanzoni mwa mwezi wa pili na mwishoni mwa mwezi wa kumi na mbili,’’

Alisema,wakati anapoandika ripoti ya mauzo ya mwezi, kwa Februari huwa anakuta ameuza kadi za aina mbalimbali kutokana watu kutumiana ujumbe wa aina tofauti unaoonyesha ishara ya upendo kati yao.