Bashe aagiza kuundwa timu huru kuchunguza bei ya korosho

Muktasari:
- Kufuatia kuwapo sintofahamu kadhaa kwenye zao la korosho ikiwamo bei, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe ameagiza kuundwa timu huru ya kuchunguza changamoto za zao hilo msimu huu, ambayo itafanya kazi ndani ya siku 14.
Mtwara. Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe ameagiza kuundwa timu huru ya kuchunguza changamoto za zao la korosho zilizojitokeza katika msimu huu.
Malalamiko yaliyogubika zao hilo msimu huu ni soko la awali linalotajwa kuangusha bei ya korosho, zao hilo linapitishwa kwenye Bandari ya Mtwara bila kupimwa na kuwapo na madhara ya kusafirisha bidhaa hiyo usiku.
Agizo hilo lilitolewa na Bashe Novemba 27,2023 kwa kupiga simu kwenye kikao kilichokuwa kikiendelea kikihusisha vyama vikuu, waendesha maghala, warajis na wadau wengine wa korosho kutoka katika mikoa mitatu inayolima zao hilo kilichokuwa kinajadili mauzo ya korosho ghafi. Kwa maelezo ya kiongozi huyo alipiga simu baada ya kuona malalamiko hayo kwenye mitandao.
Amesema kuwa ameziona hoja tatu zilizotolewa na Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha MAMCU, Siraj Mtenguka zikiwamo soko la awali kuangusha bei ya korosho, Bandari ya Mtwara korosho zinapita bila kupimwa na kusafirisha korosho usiku kunaleta madhara.
“Kutokana na madai hayo Mwenyekiti huyo aliomba kuundwa timu ya uchunguzi, sawa naagiza hiyo timu huru iundwe na mwenyekiti wa MAMCU awemo ili tuone kama hayo malala,iko ndiyo yanasababisha kuanguka kwa bei ya korosho,”amesema Bashe.
Ametaja wanaopaswa kuwepo ndani ya timu hiyo kuwa ni Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), watu wawili kutoka wizarani, mwenyekiti wa Mamcu, huku akiwaagiza mbali ya kuangalia mambo hayo matatu pia waangalie suala la kulaza nje debe kama kunasababisha changamoto kwenye soko.
“Hii timu naipa siku 14 tu wakachunguze soko la awali, korosho zinazopita bila kupimwa Bandari ya Mtwara, madhara ya kusafirisha korosho usiku je, kunaleta madhara kama ya wizi ama kuchanganya na zenye ubora hafifu, kulaza debe kama kunaathiri bei sokoni. Wizarani nitamwambia katibu mkuu alete watu wawili,” amesema Bashe.
Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Masasi & Mtwara Cooperative Union (MAMCU), Silaj Mtenguka amesema, “Sisi tulishasema kuwa hatuliziki na utaratibu wa soko la awali na tulikuwa na mwongozo , lakini tumeletewa mwingine tena katikati ya msimu bila wadau kushirikishwa na ndio unasema tusafirishe korosho usiku.
“Mnada wa kwanza wanunuzi 42, mnada wa pili wanunuzi 50 baadaye wakashuka zaidi huu mwongozo ulibadilisha ambapo wanunuzi walipungua wakafika 20 tukajiuliza kwa nini? kumbe wale wanunuzi waliotoka nje ya nchi ndio wananunua korosho kupitia soko la awali hii ni kama kangomba iliyochangamka.
“Soko la awali limetushushia bei ya korosho haiwezekani mnunuzi amekuja Tanzania ananunua kwa wakulima korosho kwa Sh1300-1500 hata akienda mnadani hawezi kupandisha bei huku anapewa nafasi ya kusafirisha korosho usiku,” amesema na kuongeza.
“Hatujiulizi kwa nini mzani wa bandarini ulibadilishwa na umeanza kutumika jana kuna nini wakati korosho ikitoka ghala kuu inatakiwa kuhakikiwa sasa pasipo mzani tunahakikishaje,” amesema Mtenguka.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Francis Alfred amesema kuwa kikao hicho ni maalumu kwa ajili ya kufanya tathmini na mweneno wa soko la korosho ghafi unaonekana kushuka.