Dk Mpango: Toeni mikopo yenye riba nafuu

Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango.

Arusha. Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amezitaka taasisi za fedha nchini kutoa mikopo ya riba nafuu kwa makundi mbalimbali wakiwemo wachimbaji wadogo wa madini, wavuvi, wakulima na wafugaji hivyo kuinua uchumi.

Ameyasema hayo leo mei 19 jijini Arusha wakati akifungua semina kwa wanahisa wa Benki ya CRDB inayofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa AICC jijini Arusha.

Amesema kuwa, taasisi nyingi za fedha zimekuwa zikitoa mikopo ya riba kwa asilimia 9 na hivyo kuhamasisha punguzo la chini ya asilimia 9 ili kuwapa fursa wafanyabiashara wadogo na wananchi waliopo vijijini kuweza kupata huduma za mikopo yenye riba nafuu.

Aidha amezitaka taasisi za fedha kuongeza huduma vijijini ili kuwapa fursa wananchi waliopo maeneo hayo, kwani kwa sasa ni asilimia 8.6 ya wananchi waishio vijijini ndiyo wanaopata huduma hizo.

"Baadhi ya mabenki yanakopesha kwa asilimia 9 hivyo yanapaswa kupunguza zaidi ili kuwapa fursa wananchi wa kipato cha chini hasa vijana na wanawake kuweza kukopa na kujikwamua kiuchumi," amesema Dk Mpango.

Katika hatua nyingi, Makamu huyo wa Rais amezitaka taasisi hizo kubuni madirisha maalumu ya mikopo kwa vijana na wanawake ambayo ni sehemu kubwa ya nguvu kazi ya Taifa lakini bado kuchukuliwa ni soko gumu kwa huduma za fedha.

Dk Mpango amezitaka benki kuzingatia ufanisi katika utendaji kazi ikiwemo kuongeza gharama za uendeshaji katika matumizi ya Tehama, sambamba na kuhakikisha hakuna mikopo chechefu mipya na kuzingatia ukomo wa asilimia 5 uliowekwa na Benki Kuu ya BOT.

Naye Mwenyekiti  wa Bodi ya Benki ya CRDB, Dk Ally Laay ameomba serikali kupitia wizara ya elimu kuandaa mitaala maalumu wa kuwafundisha wanafunzi umuhimu  wa kuwekeza  katika Hisa ili kuwapa elimu ya fedha na matumizi  sahihi.

Dk Mpango ametoa wito kwa wananchi kuendelea kuwekeza kwenye hisa kwani kama Taifa kuna mwako mdogo sana ya uwekezaji katika masuala ya hisa

"Bado kuna ufahamu mdogo kwa jamii katika maswala ya hisa na uwekezaji , katika masuala haya, mapendekezo yetu  ni kuwa tuna haja ya kufundishwa  somo  la mitaala kwenye shule zetu  ili vijana wapate ufahamu wakiwa wadogo  jambo ambalo litaleta  fikra  chanya  katika uwekezaji wa maswala ya Hisa." amesema.

Awali Mkurugenzi  wa Benki ya CRDB, Abdulmajjid Nsekela amesema kuwa, semina hiyo ya leo ni utaratibu waliojiwekea kila  mwaka wa kutoa elimu ili kuhamasisha idadi ya wanahisa  ambayo  ni chache kwa mabenki mbalimbali hapa nchini kutokana na kutokuwa na elimu ya fedha ndio maana kumekuwa  na utaratibu  wa kutumia semina ya wanahisa.

"Watanzania  tupo zaidi ya milioni 60 lakini ukiangalia kwenye mabenki yote nchini wateja hawazidi  milioni 10  wenye akaunti na hiyo ni  kutokana na elimu ndogo ya fedha ndio maana benki hii imeamua kufanya maboresho ya kuwa na semina ya wanahisa jambo lililosaidia  kuongeza  idadi ya wateja wa  benki hiyo,"amesema.