I&M Holdings PLC yainunua Orient Benki Limited ya Uganda

Muktasari:

  • Kampuni ya I&M Holdings PLC imetangaza kuichukua Benki ya Orient Limited (OBL) kwa asilimia kubwa kutoka kwa 8 Miles LLP na Morka Holdings Limited.

Dar es Salaam. Kampuni ya I&M Holdings PLC imetangaza kuichukua Benki ya Orient Limited (OBL) kwa asilimia kubwa kutoka kwa 8 Miles LLP na Morka Holdings Limited.

 OBL ni benki ya biashara ya 12 kwa ukubwa iliyosajiliwa na inafanya shughuli zake nchini Uganda.

I&M Holdings PLC na Orient Bank zilisaini makubaliano Julai 2020 ili I&M Holdings PLC kuchukua asilimia 90 ya hisa katika taasisi hiyo iliyopo nchini Uganda.

Mchakato huo ulikamilika  Aprili 30, 2021 baada ya kupokea vibali muhimu kutoka Benki Kuu ya Kenya, Benki Kuu ya Uganda, mamlaka ya masoko ya mitaji Kenya na Mamlaka ya Ushindani (Comesa).

Hatua hiyo inakazia nia ya I&M Group ya mkakati wake wa kukua na kujitanua ndani ya Afrika Mashariki, ambapo Uganda ilikuwa ni kiungo kipya katika jitihada za kimkakati za I kuanzisha uwepo wake katika nchi zote za Afrika Mashariki.

Lengo kuu la mkakati huu ni kutafuta fursa za kuwekeza katika ngazi za ndani na za kikanda ili kuiwezesha benki kuhudumia mahitaji ya wateja wote, ikiendelea  kukuza mtiririko wa biashara ndani ya kanda.

Maendeleo hayo yanasaidia kukua kwa biashara ya I&M Group kupitia upanuzi wa vyanzo vya mapato kwa kuingia katika masoko mapya na kupanua kampuni, biashara, benki binafsi pamoja na ufumbuzi wa hazina na biashara fedha kwa wateja wake wote nchini Uganda.

Akizungumza kuhusu ununuzi wa hisa hizo, mkurugenzi mtendaji wa I&M Group, Sarit Raja Shan amesema, “I&M inakusudia kuwa mdau mkuu wa ukuaji wa kifedha Afrika Mashariki. Ununuzi wa OBL unaipa fursa Benki ya I&M kukuza mtaji na uchumi katika eneo la Afrika Mashariki, na hivyo kuongeza thamani ya mwanahisa.”

“Ununuzi wa hisa hizi, unatarajiwa kuipa I&M Group uwezo mkubwa wa kukua kwa faida kupitia kupanua mtandao wetu kwa wateja wetu wa ukanda huu. Pia, inaonyesha jukumu letu la uongozi katika tasnia ya Benki Afrika Mashariki”, amesema.

Dk Ketan Morjaria, mwanachama mwanzilishi, mwanahisa na mkurugenzi wa OBL amesema, “ununuzi huu ni hatua kubwa katika historia ya Orient Bank. Tunajivunia kuunganishwa katika kampuni ya kikanda ya I&M Holdings PLC na ushirikiano huu utasaidia wateja wetu kufaidika na bidhaa za benki zilizo bora huku tukiendeleza utamaduni wetu wa uaminifu.”

Kumaran Pather, mkurugenzi mtendaji wa OBL amesema, “ununuzi wa OBL kuwa mali ya I&M Holdings PLC utasaidia taasisi hii kupanua soko letu na upatikanaji wa huduma. Uongozi wa OBL una furaha kuwa sehemu ya I&M Group, taasisi inayokua kwa kasi, na tumejipanga kuwahudumia wateja waliopo na wapya kwa bidhaa bora, majukwaa ya kidijitali na huduma za kikanda.”
Kupitia ununuzi huu, I&M Group imepata ziada ya mkopo wa mali wa Sh7.7 bilioni ya Kenya amana ya Sh18.2 bilioni ya Kenya, idadi ya wateja inayokaribia 70,000, wafanyakazi 340 na mtandao wa matawi 14 na mashine za kutoa fedha (ATM) 22 kote.

Mpango wa kuunganisha OBL umeendelezwa na kupitia utekelezaji wake I&M Group inatarajia kupata ushirikiano wa kibiashara na uendeshaji.

I&M Group imefanya uwekezaji mkubwa katika miundombinu yake imara kama sehemu ya mageuzi katika safari yake ya kidijitali.

Akifafanu  zaidi  Shan amesema, “Uganda imefanya maendeleo makubwa katika kuboresha upatikanaji wa huduma za fedha nchini kote. Ushirikiano na Orient Bank Limited umekuja muda muafaka kwani I&M Group inajipanga kushiriki kikamilifu kukuza sekta ya benki nchini Uganda, kama ilivyofanya katika masoko mengine ya Afrika Mashariki.”