Mikakati ya kuzuia wamachinga kukimbizana na mgambo yaiva

Mgambo wakipakia mbao kwenye gari ambazo ni mabaki ya mabanda na meza za wafanyabiashara ndogo ndogo (wamachinga) katika eneo la Makoloboi jijini Mwanza juzi, ilipofanyika oparesheni ya kuwaondoa wafanyabiashara hao waliopo kwenye maeneo si rasmi. Picha na Michael Jamson


Dar es Salaam. Kwa miaka mingi nchini kumekuwepo mvutano usiokwisha wa wamachinga na mgambo wa halmashauri za wilaya, manispaa, miji na majiji, hali inayotishia ustawi wa biashara ndogo nchini.

Wajasiriamali hawa ni kundi kubwa la vijana, japokuwa wapo pia wachache wa rika tofauti, waliojiajiri katika biashara za uchuuzi likiunda takriban asilimia 60 ya vijana wote nchini.

Takwimu za Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara zinaonyesha wamachinga ni kati ya wajasiriamali milioni 3.1 wanaochangia asilimia 23.4 ya nguvu kazi nchini.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Zainab Chaula anasema wamachinga milioni 1.68 wanatakiwa kusajiliwa kupata vitambulisho vya kidijitali ili waingie kwenye mfumo wa kutambulika na kuanza kulipa kodi na kwamba hatua hizo zitakamilika muda wowote hivi karibuni.

Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya kiuchumi wanasema ukuaji wa kundi hilo kutoka kumiliki mitaji midogo kwenda kwenye mikubwa, unaathriwa na mambo makubwa matatu ya kisera na kimfumo.

Kwanza, ni mkwamo wa tafsiri ya wamachinga kwa kuwa hadi sasa Serikali na wadau hawajapata muafaka kuhusu vigezo vya kuwatambua wafanyabiashara hao, hivyo kuendelea kuibua migogoro kati ya Serikali na wajasiriamali hao, ambao wanaendelea kutengewa maeneo ya kufanyia biashara.


Machinga ni nani?

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wamachinga ni wafanyabiashara wadogo wanaoingiza mapato yasiyozidi Sh4 milioni kwa mwaka, sawa na wastani wa mauzo ya Sh11,000 kwa siku.

“Viongozi wetu wanasema itafsiriwe kwa mtaji usiozidi Sh4 milioni ili mapato yake yajulikane kwa mwaka. Badala ya kuangalia mapato, Serikali iliagiza tukae na TRA ili kukubaliana tafsiri ya pamoja lakini hadi sasa hatujaitwa,” anasema Steven Lusinde, makamu mwenyekiti wa wamachinga taifa.

Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo anasema hoja ya mjadala wa tafsiri uko chini ya wizara yenye dhamana na biashara na si TRA.

“Sisi hatuhusiki na wamachinga, tunahusika na waliopo kwenye mfumo rasmi,” anasema Kayombo.

Hoja ya pili ni ukosefu wa takwimu za wamachinga, huku Serikali ikifafanua kuwa changamoto hiyo inaathiri kundi na kusababisha lishindwe kutambuliwa na kuunganishwa na fursa mbalimbali za maendeleo.

“Ili kuondokana na changamoto hii, wizara inakamilisha uandaaji wa mfumo wa kielektroniki wa kuwatambua, kuwasajili na kutoa vitambulisho utakaosaidia kuwaunganisha na fursa mbalimbali za maendeleo zilizopo,” inasomeka sehemu ya taarifa ya Dk Chaula.

 


Siasa kikwazo

Profesa Humphrey Moshi, gwiji wa uchumi katika Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) anasema siasa ndiyo changamoto kubwa inayodumaza kukua kwa kundi la wamachinga nchini.

“Siasa imekuwa ikiathiri hata utekelezaji wa sheria, ukiwagusa utasikia waache wapigakura wangu. Matokeo yake hakuna uwazi wa mapato yao halisi na kodi inayotakiwa kuchukuliwa kwao,” anasema mchumi huyo.

Hoja ya tatu inaakisi kauli ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba aliyoitoa hivi karibuni akiagiza kusitishwa kwa mchakato wa usajili uliokusudia kukusanya kodi zaidi ya Sh5 bilioni kutoka kwa wamachinga 8,900 wa Soko Kuu la Kariakoo.

Katika ufafanuzi wake, Dk Mwigulu alisema msingi wa kodi hiyo ni maeneo mahususi ya biashara yanayopaswa kutumia mashine za risiti za kielektroniki (EFD) na kuwahusisha wamachinga.

“Ili kuwasaidia katika ukuaji ni muhimu kuwatambua kitakwimu, unaimarisha mazingira ya kufanyia biashara zao, mazingira yenye ushawishi na rafiki kufikika na kisha kuwatafutia mitaji ili wakuze biashara. Zamani walichangia Sh20,000 wakasambaa kila mahali, hiyo haifai,” anasema Profesa Moshi.


Wanatambuliwa

Kuhusu mtizamo huo wa kisiasa, Dk Chaula anasema jitihada za Serikali za kuwatambua na kuwarasimisha zinaendelea ili waweze kutambuliwa na kufanya biashara zao kwa uhuru na kuchangia pato la Taifa.

“Serikali inaendelea kuwaelimisha na kuwahimiza wamachinga wasitumiwe na wafanyabiashara wachache ambao wanataka kukwepa kodi. Mwitikio wao kwenye suala hili ni chanya na wanaendelea kuelimishana wao kwa wao kuhusu umuhimu wa kulipa kodi kwa maendeleo ya nchi yetu,” anasema Dk Chaula.

Kwa mujibu wa Lucas Katera,
mtafiti mwandamizi wa Repoa, wamachinga ni sehemu ya asilimia 30 ya sekta isiyo rasmi inayotakiwa kufikiwa na kutambuliwa ili kuongeza mapato ya Serikali kama ifanyikavyo katika nchi nyingine.

Dk Constantine George, mtafiti wa sekta isiyokuwa rasimi anasema miaka ya 2000 Rwanda ilianza kulitambua na kulirasimisha kundi hili kwa kutoa ujuzi na mitaji kwa vyama vyao kabla ya kuanza kukusanya mapato.

Anashauri zikusanywe takwimu za wamachinga ili kutambua mchango wao katika biashara.

Hata hivyo, wizara yenye dhamana ya makundi maalumu inaendelea kuweka misingi ya suluhisho la changamoto za mitaji, maeneo ya kufanyia biashara na wamachinga kutambuliwa rasmi kama wafanyabiashara wanaochangia pato la Taifa, huku ikiandaa uongozi kuanzia ngazi ya Taifa hadi wilaya.

Aidha, wizara hiyo pia inaendelea kufanya majadiliano na taasisi za fedha ili kuweka masharti nafuu ya kupata mikopo, kukamilisha mwongozo wa kuwaratibu pamoja na mpango wa matumizi ya Sh45 bilioni za mitaji ya miradi ya kiuchumi katika sekta za mifugo, kilimo, uvuvi, madini na nyinginezo.

Mikakati hiyo ni maboresho ya wazo la kuwapatia vitambulisho
vilivyosambazwa kwa zaidi ya wamachinga milioni 1.5 kote Tanzania.

Januari 25 mwaka jana, Rais Samia Suluhu Hassan aliagiza wamachinga wote kuwa sehemu ya makundi maalumu chini ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii inayoongozwa na Waziri Dorothy Gwajima na kuwapa vitambulisho baada ya kukamilika kwa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 pamoja na kuandaliwa kwa masoko mapya ya Jangwani, Karume na Kariakoo.