Nchi za SADC kutia mguu Nanenane Mbeya

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera (katikati) akizungumza wakati wa kikao cha maandalizi ya sherehe za Nanenane kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanal Laban Thomas.

Muktasari:

  • Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amesema maonesho hayo ambayo yamezoeleka kuwa ya kitaifa, mwaka huu yatakuwa ya kimataifa kutokana na nchi kutoka mataifa mbalimbali zikiwamo za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuonyesha nia ya kushiriki.

Mbeya. Zaidi ya mataifa tisa yanatarajia kushiriki maonesho ya Nanenane yanayotarajia kufanyika kitaifa jijini Mbeya, huku Halmashauri zinazodaiwa bili za maji zikitakiwa kulipa ifikapo Mei 24 ili kutoathiri shughuli hiyo itakayoshirikisha nchi mbalimbali.

 Maonyesho hayo yanatarajia kufanyika kwa siku nane kuanzia Agosti 1 huku maandalizi yake yakianza rasmi leo kwa kuwakutanisha viongozi mbalimbali wa Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.

Akizungumza leo Mei 19 kwenye kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Juma Homera amesema maonesho hayo ambayo yamezoeleka kuwa ya kitaifa, mwaka huu yatakuwa ya kimataifa kutokana na nchi kutoka mataifa mbalimbali zikiwamo za Jumuiya ya maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuonyesha nia ya kushiriki.

Amesema hadi sasa maandalizi yanaendelea vizuri huku akizitaka Halmashauri zinazodaiwa bili za maji kulipa haraka ifikapo Jumatano ya wiki ijayo ili kurahisisha ufanisi wa shughuli hiyo muhimu.

"Naomba Mamlaka ya maji kufungua bomba zote za maji wakati Halmashauri zinazodaiwa zikiendelea na mchakato wa kulipa nataka hadi Jumatano madeni hayo yawe yamelipwa, hatutaki kuanza kurudi nyuma wakati shughuli zinaendelea, ukizingatia hili ni jambo la kitaifa na kimataifa hatutaki aibu" amesema Homera.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Maendeleo ya mazao kutoka Wizara ya Kilimo, Nyasebwa Chimagu amesema wizara hiyo imejipanga kuhakikisha maonesho hayo mwaka huu yanakuwa bora kwa kushirikisha wadau mbalimbali.

"Hadi sasa vikao vya ndani vinaendelea na tumejipanga mwaka huu maonesho haya kuwa bora, tunapokea pia ushauri wa kuboresha zawadi kwa washindi tofauti na mwaka jana" amesema Chimagu.

Naye mwenyekiti wa sekretarieti ya maandalizi ya maonesho hayo, Jeremiah Sendoro amesema hadi sasa tayari wamewaandikia wadau zikiwamo kampuni mbalimbali zipatazo 145 huku mchakato wa kuwafikia wengine ukiendelea.

"Mbiu ya mwaka huu katika maonesho haya ni vijana, wanawake ni msingi imara wa mifumo ya chakula na usalama wa chakula, japokuwa tumepokea maoni kuweza kuboresha kauli mbiu hii," amesema Sendoro.