Noti za Sh10,000 zaongezeka mitaani, wachumi, BoT watofautiana

Muktasari:

  • Ripoti ya Dondoo za Takwimu za Robo mwaka inayotolewa na BoT kuonyesha ongezeko la asilimia 43 la noti ya Sh10,000 kwenye mzunguko kati ya Desemba 2018 na Desemba 2023.

Dar es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema ongezeko la thamani na idadi ya noti za Sh10, 000 kwenye mzunguko kwa miaka sita mfululizo linatokana na kufunguka kwa uchumi, kauli inayopingwa na wachumi wakiwa na sababu tofauti.

Wachumi waliozungumza na Mwananchi wamesema ongozeko la noti za Sh10, 000 mtaani, ni ishara ya kushuka kwa thamani ya fedha za Tanzania na kuongezeka kwa mfumuko wa bei.

Tofauti hizo za kimtazamo zinakuja baada ya ripoti ya Dondoo za Takwimu za Robo mwaka inayotolewa na BoT kuonyesha ongezeko kubwa la thamani na mzunguko wa noti ya shilingi 10,000, ambayo ndiyo kubwa kuliko zote nchini.

“Desemba 2018, noti za Sh10,000 kwenye mzunguko zilikuwa na thamani ya Sh3.6 trilioni, mwaka 2019 iliongezeka hadi Sh4 trilioni, mwaka 2020 zikafika Sh4.2 trilioni.

“Desemba 2021 thamani za noti hizo katika mzunguko ziliongezeka hadi Sh4.8 kabla ya kuongezeka hadi Sh5.5 mwaka 2022 na kufikia Sh6.3 trilioni mwaka 2023,”inaeleza sehemu ya ripoti hiyo.

Vilevile ongezeko hilo la Sh10, 000 mtaani kwa Desemba 2023 sawa na asilimia 43 ikilinganishwa na hali ilivyokuwa Desemba 2018.

Hali hiyo inaelezwa na Profesa Humphrey Moshi kuwa ongezeko la noti hizo zenye thamani kubwa zaidi linamaanisha thamani ya fedha ya Tanzania inashuka na kuna ongezeko la mfumuko wa bei.

 “Hii inamaanisha vitu viwili, kwanza thamani ya sarafu yetu inashuka ukilinganisha na dola, kwa sababu uwezo wa fedha yetu kununua bidhaa  umepungua.

“Pili inamaanisha kuwapo kwa mfumuko wa bei, hii inaweza kuwa imesababishwa na vitu mbalimbali kama vita vya Urusi na Ukraine kwa sababu kuna bidhaa tulikuwa tunazitegemea kutoka katika nchi hizo kama vile ngano,” amesema na kuongeza Profesa Moshi ambaye mkurugenzi wa Kituo cha mafunzo ya Kichina Afrika (CCS.)

Kauli ya Profesa Moshi inaungwa mkono na Profesa mwenzake wa uchumi na mtafiti wa UDSM, Abel Kinyondo anayekazia kuwa kuongezeka kwa fedha hizo mitaani ni kiashiria kwa kupungua kwa thamani ya fedha yetu.

“Ukiona watu wanatumia fedha ya juu kabisa katika manunuzi yao, ujue thamani ya ununuaji wa fedha hiyo imeshuka na hii inasababishwa na mfumuko wa bei, vilevile inamaanisha unatumia fedha nyingi kununua bidhaa.”


Biashara zimefunguka

Hata hivyo, Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba amezipinga hoja hizo akisema kuongezeka kwa noti hizo kunamaanisha uchumi wa Tanzania umefunguka na biashara zinafanyika kwa wingi.

Loading...

Loading...

 “Ukifanya uchambuzi wa kiuchumi vizuri, hauwezi kusema hizo ni sababu kwa kuwa mfumuko wetu wa bei upo wastani wa asilimia 3, sasa hauwezi kusema mfumuko wa bei umesababisha kuongeza mzunguko wa higher denomination (fedha zenye thamani kubwa).

“Lakini pia kushuka kwa thamani ya fedha yetu nayo si sababu kwa sababu ukiangalia kwa miaka kama mitatu iliyopita depreciation (kushuka) ya shilingi ilikuwa kama asilimia 1 kwa mwaka, lakini kwa mwaka huu bado ipo wastani wa asilimia 8 licha uhaba wa dola, vita vya Ukraine, athari za Uviko-19 lakini bado shilingi yetu imekuwa stable (imara) kwa kiwango fulani,” amesema Tutuba.

Tutuba amezitaja sababu za hali hiyo kuwa ni kufunguka kwa uchumi kwa sababu Serikali imeweka mazingira wezeshi ya wafanyabiashara kuendesha shughuli zao za kiuchumi kwa uhuru na wanapata faida.

“Kutokana na hilo mzunguko wa fedha unakuwa mkubwa, sasa unapokuwa mkubwa katika uchumi ambao watu wanatumia fedha taslimu (cash), ndipo utaona hizo ishu za kuwepo kwa shilingi zinazunguka,” amesema Tutuba.


Wachumi washauri

Licha ya kuwa na mgongano wa hoja kati ya wachumi na BoT, Profesa Moshi ameshauri kuweka msukumo kwenye kilimo ili kuongeza uzalishaji na matumizi ya fedha za Tanzania katika biashara za kimataifa.

 “Tuweke msukumo katika kilimo ili uzalishaji uongezeke, ukiangalia bado sekta yetu ya kilimo ‘speed (kasi) yake katika ukuaji ni ndogo. Lakini pia tuanze kutumia fedha zetu katika biashara za kimataifa, tunavyonunua bidhaa,” ameshauri.

Vilevile Profesa Kinyondo ameshauri kuongeza uzalishaji ili uuzwaji wa bidhaa zetu nje ya nchi uongezeka.

“Tunachotakiwa kukifanya ni kuhakikisha fedha yetu iwe na thamani na njia rahisi kabisa ni kuongeza uzalishaji ili kupunguza mfumuko wa bei,” amesema.

Hata hivyo, Tutuba amesema wanaendelea kuhimiza ulipaji na matumizi ya malipo ya kidijitali kwa ajili ya kuongeza wigo wa mapato.

“Kwetu kuongezeka kwa mzunguko ni kama fursa na tunaendelea kuweka mazingira wezeshi ili watu wafanye biashara kwa uhuru zaidi, wapate faida na wawe formalized (wawe rasmi) ili walipe kodi, na sasa tumekamilisha mfumo ule wa TIPS (malipo ya papo hapo mtandaoni) ambao utazinduliwa hivi karibuni,” amesema Tutuba.


Mzunguko fedha nyingine

Mbali na kuongezeka kwa mzunguko wa noti ya Sh10,000 pia noti ya Sh2,000 imeongezeka kutoka Sh177.2 milioni Desemba 2018 hadi Sh230.8 milioni Desemba 2023 sawa na ongezeko la asilimia 15.

Noti ya Sh5,000 thamani ya mzunguko wake ilipungua kutoka Sh732.2 Desemba 2018 hadi Sh713.7 mwaka 2023 sawa na kupungua kwa asilimia 2.5.