Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ongezeko mauzo ya bustani nje ya nchi na athari zake kiuchumi

Kuimarika kwa uhusiano wa kidiplomasia, uwepo wa sera wezeshi katika sekta ya biashara na miundombinu zimetajwa kuwa sababu za kupaa kwa mauzo ya mazao ya bustani nje ya nchi, ikiwemo mbogamboga na matunda.

Mauzo hayo yameongezeka karibu mara mbili zaidi kutoka Sh747.9 bilioni Januari mwaka 2023 hadi Sh1.05 trilioni kufikia Januari mwaka 2024. Hii ni kwa mujibu wa ripoti ya Mapitio ya Uchumi ya kila mwezi (MER – Januari 2024) inayotolewa na Benki Kuu (BoT).

Kuhusu ongezeko hilo, Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk Hashil Abdallah anasema mafanikio hayo yanatokana na sera wezeshi, hususan kwenye sekta ya mazao ya kilimo cha bustani.

“Uwepo wa ndege ya mizigo yenye vifaa vya ubaridi na teknolojia ya uhifadhi iliyopo na inayoendelea kujengwa bandarini ni sababu nyingine ya kuongezeka kwa mauzo,” alisema.

Akielezea, mkulima wa zao la pilipili na maharage marefu kutoka Arusha, Yasinta Manyata anasema mabadiliko ya uuzaji nje ya nchi yapo, hasa mwaka 2023 hadi sasa.

“Kimsingi nimeanza kuuza kwa uhakika moja kwa moja nje ya nchi mwaka jana mwishoni na mabadiliko yapo. Nimekuwa na wateja kutoka nchi mbalimbali za Ulaya.”

Lakini pia changamoto hazikosekani kama alivyobainisha katika upande wa mchakato wa kilimo na usafirishaji, anasema jambo lililopo ni utunzaji kutokana na vigezo vya wanunuzi wanavyotaka.

“Changamoto iliyopo ni utunzaji wa zao ili liwe katika hali nzuri na likubalike sokoni, hii ni kutokana na kuwa soko la Ulaya linachagua sana. Mkulima ana uelewa wa kutunza zao lakini mnunuzi na yeye ana maelekezo yake, hivyo inatupa changamoto, hasa ikizingatiwa bado hatuna uwezo mkubwa,” alisema.

Yasinta anasema kwa upande wa usafirishaji kuna changamoto ya ndege: “Kwa wenzetu wa Kenya kuna baadhi ya kodi na tozo walizitoa kuanzia uwanja wa ndege, hivyo wanasafirisha kwa urahisi kwenda sokoni tofauti na sisi.

“Kuna wakati ndege inaweza kuahirisha safari, hapo ni hasara, kwani hatuna uwezo wa kutunza mazao. Hivyo ni rahisi wateja wetu kuhamia mataifa mengine, wanatuona hatuna uhakika,” amesema.

Hata hivyo, anasema hatua ya Serikali kuwapatia mbolea za ruzuku ambayo wananunua kwa wastani wa Sh70,000 kwa mfuko kutoka Sh150,000 imeleta nafuu kubwa na kuchochea biashara.

“Pia maofisa ugani wamepewa mwongozo watembelee mashambani waone watu tunavyolima, hii inatusaidia,” ameongeza.


Nini faida ya ongezeko hilo

Mhadhiri wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Lutengano Mwinuka anasema uzalishaji ukiongezeka unakuwa na maana nyingi, ikiwemo kuongezeka kwa tija.

Walioongeza uzalishaji wanapata mapato na kwenye mifumo ya uzalishaji kuna watu wamejiajiri na walioajiriwa wanapata mapato.

“Tukiangalia kwa jicho la ajira isiyo rasmi hapa kuna watu wanapata ajira, wanapata mapato kwa kupata fedha za kigeni ambazo watazitumia kufanya manunuzi hata kwa bidhaa za nje,” alisema

Dk Mwinuka anaongeza kuwa suala hilo lina faida kwa kuanzia wahusika wanaozalisha na Serikali kwa kupata kodi.

“Jambo la kufanya hapa kuwe na mipango kama ya kutunza vyanzo vya umwagiliaji ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya mbogamboga na matunda ambayo kwa kiasi kikubwa kinategemea miundombinu ya umwagiliaji.

“Kuhusu kuwajenga vijana na wanawake ambao katika eneo hili wana mchango mkubwa zaidi, programu mbalimbali ziendelee maeneo mengi ili kuongeza ufanisi,” alisema.

Naye Mhadhiri wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Humphrey Moshi anasema suala hilo linatoa sura kwamba lazima tubadilike na kujikita huko kwa kuwa tuna uwezo na fursa.

Anasema kuna haja ya kuongeza ufanisi kwenye eneo la usafirishaji ili mnyororo mzima kuanzia uzalishaji hadi usafirishaji uongezeke thamani.

Ikumbukwe mwezi uliopita jijini Arusha, Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (Fao), lilisaini makubaliano ya awali na Kituo cha Utafiti wa Mbogamboga na Matunda cha Kimataifa na kukipatia Dola 650,000 za Marekani (Sh1.6 bilioni) kwa ajili ya kuboresha benki ya mbegu iliyopo kituoni hapo.

Ilikuwa Machi 5, 2024 ambapo Katibu wa Usimamizi wa Mikataba ya Kimataifa wa Fao, Uhifadhi wa Vinasaba vya Mbegu, Dk Kent Nnadozie wakati wa utiaji saini makubaliano hayo yaliyofanyika katika ofisi za kituo hicho eneo la Tengeru, alisema lengo la Fao kukabidhi fedha hizo kwa kituo hicho ni kukuza na kuboresha kilimo cha mbogamboga hapa nchini na Afrika kwa jumla.

Vilevile, Juni mwaka jana jijini Mbeya, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Ushirika ilitenga zaidi ya Sh500 milioni kwa ajili ya kusaidia wakulima wa mbogamboga na matunda ili kuongeza tija.

Hadi sasa tume hiyo imefikia mikoa saba ambayo ni Songwe, Mbeya, Njombe, Iringa, Manyara, Arusha na Kilimanjaro, ikitoa mafunzo ya kuwajengea uwezo na jinsi ya kukabiliana na changamoto mbalimbali.

Mratibu wa mafunzo kutoka Tume ya Taifa ya Ushirika, Deogratias Bendera alisema mafunzo hayo yalilenga katika kujifunza matumizi ya fedha pamoja na kuwajengea uwezo wa jinsi ya kupata masoko, mitaji, sehemu za kuhifadhia mazao na utunzaji wa mahesabu.


Nafasi ya Serikali

Kwa mujibu wa hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Kilimo ya mwaka 2023, uzalishaji wa mazao hayo kwa mwaka 2021/22 ilikuwa tani milioni 7.7.

Kati ya hizo, tani milioni 2.2 ni za mbogamboga, tani milioni 5.4 za matunda , tani 1,350.8 za maua na tani 101,627.9 za viungo.

Akisoma bajeti hiyo Bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alisema Wizara kwa kushirikiana na wadau imeendelea kutoa mafunzo kuhusu uendelezaji wa mazao ya bustani hadi kufikia Aprili, 2023.

“Wizara kwa kushirikiana na Peace Corps imetoa mafunzo kuhusu kuibua na kuendesha miradi ya bustani za mbogamboga na matunda kwa walimu 150 wa shule za msingi na walimu 75 wa shule za sekondari kutoka Mikoa ya Dodoma, Iringa, Singida, Mtwara, Njombe, Rukwa, Lindi, Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Tanga, Mara na Tabora ili kuimarisha lishe na kipato,” alisema.

Aidha, alisema mkakati wa kuendeleza Tasnia ya Mazao ya Bustani (horticulture) mwaka 2021-2031 pamoja na mwongozo wa kuendeleza zao la parachichi umeandaliwa. Hatua hizo ziliwezesha kuongeza mauzo ya nje ya zao la parachichi kutoka tani 9,978 mwaka 2020 hadi tani 29,031 mwaka 2022.

Pia alisema, Wizara kupitia mradi wa AGRI - Connect itajenga vyumba vya ubaridi (cold rooms) vinne na vituo vitatu vya kukusanyia matunda na mboga, katika Mikoa ya Iringa, Njombe na Mbeya kwa lengo la kupunguza upotevu, kuboresha masoko na kuimarisha usalama wa chakula na lishe.

Kwa upande wa Wizara ya Viwanda na Biashara, hotuba ya bajeti 2023/24, ilisema imekamilisha usanifu wa teknolojia ya kisasa ya kuhifadhi mazao ya matunda na mbogamboga kwa kiwango cha mkulima mdogo.

Waziri Dk Ashatu Kijaji alisema wamewezesha wafanyabiashara wa Tanzania 859 kupata fursa ya kutangaza bidhaa zao kupitia maonesho, misafara ya kibiashara na makongamano ya kibiashara yaliyoratibiwa na TanTrade kwenye mataifa mbalimbali duniani, ikiwemo China, Saudi Arabia, Kuwait, Qatar, Kenya, Rwanda, Burundi, Comoro, Oman na Marekani.