Selcom yainunua Access Benki Tanzania

Muktasari:

  • Kununuliwa kwa benki ya Access ni hatua inayolenga kuboresha utoaji wa huduma za kifedha kwa watu wenye kipato cha chini.

Dar es Salaam. Kampuni ya Selcom imeinunua iliyokuwa benki ya Access Tanzania ikiwa ni moja ya hatua za kutanua shughuli zake za biashara katika huduma za kifedha nchini.

Uwekezaji uliofanywa na Selcom ,sasa unaifanya benki hiyo kuwa na mtaji wa zaidi ya Sh8.6 bilioni, huku ikibeba malengo ya kuwa miongoni mwa benki kubwa tatu ndani ya muda mfupi.

Selcom ni kampuni ambayo imejikita zaidi katika teknolojia ya malipo ya huduma za fedha katika maeneo mbalimbali nchini.

Hayo yameelezwa leo Juni 4, 2024 katika hafla ya kutangaza jina jipya la benki hiyo iliyofanyika jijini hapa.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mwakilishi wa bodi ya wakurugenzi, Tusekile Kibonde amesema mabadiliko hayo yanalenga kuboresha huduma za kibenki kwa kuzingatia namna wanavyoweza kuwafikia watu wengi wa chini, kati na juu kwa ubora na gharama nafuu.

“Katika mipango yote, mojawapo ni kuhakikisha tunabadilisha jina la benki linalokuja na uwekezaji mpya, unaombatana na mambo mengi mapya ambayo mtayaona na kuyafaidi katika huduna zetu zitakazopatikana kirahisi zaidi nchini na ubora,” amesema.

Amesema wajasiriamali wanasaidia kupata pato la Taifa kwa asilimia 35, huku wakiajiri asilimia 40 ya watu nchini, jambo ambalo liliifanya benki hiyo kufanya maboresho kwa ajili ya kujenga taasisi.

Mkurugenzi mkuu wa benki hiyo, Julius Ruwaichi amesema lengo la kuanzishwa kwa benki hiyo ni kumpa Mtanzania wa hali ya chini fursa ya kufanya biashara na benki na kukuza biashara zake.

Amesema Selcom ina uzoefu mkubwa ndani na nje ya Tanzania kupitia tasnia ya malipo ya huduma na kuwa uwekezaji huo utasaidia benki kufikia melengo makubwa kwa haraka na ufanisi huku ikihakikisha mlaji anapata huduma nzuri za kibenki kwa wakati.

Amesema mchakato huo ulipitia taratibu zote zilizotakiwa hadi kupatikana kwa Selcom, akiwa miongoni mwa waliokuwa wameonyesha nia.

“Sisi tunaamini kuwa kupitia uwekezaji huu ndani ya miaka mitatu tutakuwa miongoni mwa benki kubwa nchini, tunayo nia na ari, katika teknolojia tutakuwa bora na hii utafanya huduma kuwa rafiki kwa mtu yoyote anayehitaji huduma za kibenki nyumbani au nje,” amesema Ruwaichi.

Amesema benki hiyo sasa itajikita zaidi katika kusaidia watu wa chini kati na juu lakini nguvu kubwa ikiwekwa kwa wateja wadogo.

“Mabadiliko haya hayataathiri shughuli zozote za kibenki na kila kitu kilichokuwa chini ya Access benki kitahamishiwa Selcom Microfinance kwa mujibu wa sheria,” amesema.

Uwekezaji huu na mabadiliko ya jina yanatangazwa ikiwa ni takribani miezi minne tangu mwanzilishi wa Benki ya Access duniani, Herbert Wigwe (57) kufariki dunia kwa ajali ya helikopta iliyotokea California, nchini Marekani Februari 10, mwaka huu.

Katika ajali hiyo iliyoondoa uhai wa Winge pia ilisababisha kifo cha mkewe, mtoto wake wa kiume na watu wengine watatu waliokuwa ndani ya helikopta 'chopa' hiyo.

Benki ya Access yenye makao makuu chini Nigeria ina matawi katika nchi za Tanzania, Congo, Ghana, Kenya, Uganda, Nigeria, Rwanda, Gambia, Guinea, Cameroon, Sierra Leone, Msumbiji, Botswana, Afrika Kusini, Zambia, Ufaransa na Uingereza.