Sh3 bilioni zatengwa kwa vyama 70 vya ushirika

Meneja Mkuu wa benki ya KCBL, Godfrey Ng'ura

Muktasari:

  • Zaidi ya vyama 70 vya ushirika mkoani Kilimanjaro vimetengewa Sh3.5 bilioni na benki ya ushirika ya KCBL kwa ajili ya ununuzi wa kahawa katika msimu huu wa mwaka 2021/22.

Moshi. Zaidi ya vyama 70 vya ushirika mkoani Kilimanjaro vimetengewa Sh3.5 bilioni na benki ya ushirika ya KCBL kwa ajili ya ununuzi wa kahawa katika msimu huu wa mwaka 2021/22.

Lengo la kuvikopesha vyama hivyo ni kuwapunguzia mizigo viongozi wa vyama hivyo wakati wa ununuzi wa Kahawa kwa wakulima katika msimu huu.

Hayo yamesemwa na meneja mkuu wa benki hiyo, Godfrey Ng'ura alipokutana na viongozi wa vyama hivyo vya ushirika.

"Benki ya KCBL itafanya biashara na vyama vyote vya ushirika vya Mkoa wa Kilimanjaro na tayari tumetenga Sh3.5 bilioni kwa ajili ya kuwasaidia wakulima wa Kahawa," amesema Ng'ura

Naye mrajisi wa vyama vya ushirika mkoani humo, Henjewele John amesema fedha hizo zitasaidia kuwaondolea usumbufu wa malipo wakulima hao.

"Utaratibu huu utawapunguzia mzigo viongozi wa vyama hivi vya ushirika na pamoja na usumbufu wa kuhangaika kutafuta mikopo ya wakulima," amesema