Sheria za kodi, huduma mbovu kikwazo kwa wafanyabiashara

Baadhi ya wafanyabiashara wakiwa katika mkutano wa Jukwaa la Kodi na Uwekezaji 2024, jijini Dar es Salaam leo, Februari 26, 2024. Picha na Sunday George

Muktasari:

  • Baadhi ya wafanyabiashara wameendelea kulia juu ya kodi wanazotozwa, sheria za kodi zinazowaumiza, wakitaka baadhi ziondolewe au kupunguzwa.

Dar es Salaam. Ikiwa leo ni siku ya pili ya Jukwaa la Kodi na Uwekezaji mwaka 2024, vilio vya kodi kubwa, sheria za kodi na kupata huduma mbovu katika ofisi za halmashauri vimetawala katika jukwaa hilo.

 Mkutano huo unafanyika ukiwa ni maandalizi ya bajeti ya Serikali ya mwaka 2024/25.

Wakizungumza katika jukwaa hilo, leo Februari 28, 2024 katika ukumbi wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIC) jijini hapa, wafanyabiashara hao wametaka sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kupitiwa upya hususan katika sekta ya utalii wa uwindaji, wakisema uwepo wake umefukuza wageni.

Akizungumzia hilo, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kampuni za Kuongoza Uwindaji wa Kitalii Nchini (TAHOA), Suleiman Masato amesema kabla kufanyika kwa mabadiliko ya sheria ya VAT, watalii zaidi ya 1,500 walikuwa wanakuja nchini kwa ajili ya uwindaji, lakini sasa imeshuka hadi 450.

"Tumehangaika kwa miaka mitano hatujafanikiwa, tufanye marekebisho ya sheria ya VAT ikiwapendeza ipungue au iwe sifuri kwa sababu watalii hawa wanapokuja kuwinda na kusafirisha kwenda nje tunatengeneza fedha za kigeni," amesema Masato.

Amesema kampuni za uwindaji wa kitalii ziko 32 pekee, lakini mchango wake katika pato la Taifa ni karibu sawa na ule unaoweza kupatikana katika kampuni nyingine 100 hadi 200.

Akiunga mkono hoja hiyo, Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Wafanayabiashara ya Utalii (TCT), Latifa Skyes amesema utalii una nafasi ya kuleta fedha nyingi za kigeni nchini, lakini baadhi ya mabadiliko ya sheria yamekuwa changamoto.

"Kuna maboresho yanatakiwa kufanyika, utalii ni sekta ya kimkakati tunaomba kukaa na Serikali kwa ujumla, ili tuwaonyeshe ni vipi tunaweza kufanya ili kukuza uwekezaji katika eneo hili," amesema Skyes.

Kwa upande wake, mdau wa utalii, Leopord Kabendera ameitaka Serikali kuangalia upya mfumo wa utalii, ili ulete manufaa zaidi kwa nchi.

Mbali na VAT, pia wafanyabiashara wamepaza sauti juu ya sheria ya ukaguzi wa kodi ya miaka mitano na sheria inayoipa uwezo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kushikilia akaunti za mteja na kuzitumia.

Innocent, kutoka Iringa naye ameeleza kuwa wazawa wanaofungua kampuni za utalii nchini wanapata changamoto nyingi zinazowafanya wafilisike kwa haraka kutokana na sheria zilivyo.

Amesema nchi ina nafasi ya kutengeneza fedha nyingi za kigeni kupitia utalii kwa sababu ya uwepo wa vivutio, lakini kampuni za wazawa zimekuwa zikishindwa kukua kutokana na sheria zilivyo.

"Mfano sheria ya ukaguzi wa kodi ya TRA ile ya miaka mitano inaumiza sana watu, kuna wakati Rais alisema ifutwe lakini bado ipo.

“Nina rafiki zangu walikuwa na kampuni ya kitalii, walilipa kodi vizuri kila mwaka, lakini ulipokuja ukaguzi wa miaka mitano waliambiwa wanadaiwa zaidi ya Sh1 bilioni, kampuni ilifungwa," amesema Innocent.

Amesema kichaka hicho cha ukaguzi wa hesabu za nyuma kilichotengenezwa na TRA kinafanya mitaji ya watu kukatika na kuirudisha nyuma.

Akizungumzia suala la TRA kushika akaunti za wateja na kuhamisha fedha zilizomo, ameshauri liangaliwe na ikiwa sheria ipo, ibadilishwe na kila linalofanyika liwe kwa amri ya mahakama.

"Kama kuna mgogoro kati yangu na TRA, basi uende mahakamani kabla ya kushika akaunti yangu. Jambo hili linaumiza sana watu kwa sababu unaweza kuwa unadaiwa Sh60 milioni akaunti ikashikwa ina fedha zaidi ya hiyo," amesema Innocent.

Uwepo wa kodi kubwa ulimuibua pia mwenyekiti wa shule binafsi na vyuo nchini, Makulu Mlingo aliyesema utitiri wa kodi hususani katika vituo vya afya umekuwa ukiongeza gharama kwa wagonjwa.

Amesema huduma za afya zilipaswa kuwa bora kwa kiwango cha juu, ili kuhakikisha wafanyabiashara wanaandaliwa mazingira mazuri kwa ajili ya wananchi wakaazi na wageni, lakini imekuwa kinyume.

Amesema kinachotatizo ni kulipishwa kodi hadi kufanya watu kuingia gharama kubwa wanapohitaji huduma, huku waendeshaji wakipata shida.

"Hili linaenda sambamba na kwenye elimu, ukitaka kufungua chuo cha afya unatakiwa kuwa na madaktari wabobezi 80 kiwango cha chini 40, ukiwatafuta nchini huwapati, ukitaka kuingiza kutoka nje haiwezekani.

"Mazingira haya yanatengenezwa kwa hoja ya kulinda ajira, unalinda ajira ipi wakati unajua nchi ina shida ya wabobezi?

“Unachokifanya si kibaya kwa sababu unataka kuanzisha vyuo vya madaktari ambao hawa watu wanaweza kutoa huduma nzuri, lakini unabaki nyuma," amesema Mlingo.

Kutokana na suala hilo, ametaka kuwapo kwa mabadiliko ikiwemo kuangalia namna ya utozaji wa kodi hasa katika sekta ya afya na elimu, kwani kinachoonekana ni watu kutozwa kodi mara mbili.

“Kwa sababu baada ya mtoa huduma kulipa kodi, pia wanaohitaji huduma ikiwemo wagonjwa wanapopewa huduma hukatwa pia asilimia fulani ya kodi na hata wanafunzi wanapolipa ada pia hukatwa kodi,” amesema.

Mkurugenzi wa kiwanda cha Union Metat Group, Mariam Ng'hwani amesena ni vyema elimu ya uwekezaji ikatolewa hadi ngazi ya halmashauri, ili wajue namna nzuri ya kufanya kazi na wawekezaji.

 "Ngazi za chini kama halmashauri hawaelewi dhana hii, jambo linaofanya wawekezaji wafanye kazi kwa ugumu. Ni vyema walau kuwe na kikosi kazi cha kusimamia uwekezaji ili kunapokuwa na shida kitengo hicho kiongee na mwekezaji," amesema Mariam.