Sintofahamu bei kuku wa nyama ikipaa

Muktasari:

Kupanda kwa gharama za uzalishaji kumesababisha kupanda kwa bei ya kifaranga cha kuku kwa Sh300 kutoka Sh1,800 hadi 2,100, hivyo kutishia mustakabali wa wafugaji.

Dar/Moshi. Kupanda kwa gharama za uzalishaji kumesababisha kupanda kwa bei ya kifaranga cha kuku kwa Sh300 kutoka Sh1,800 hadi 2,100, hivyo kutishia mustakabali wa wafugaji.

Inaelezwa ongezeko hilo la bei lilianza kushuhudiwa tangu Juni, hali inayowaweka wafugaji katika wakati mgumu kiasi cha baadhi yao kufikiria kuacha kufuga.

Wakati wafugaji wakieleza hayo, kampuni za utotoleshaji vifaranga zinasema ongezeko la bei za nafaka na virutubisho vingine muhimu ni miongoni mwa sababu zilizochangia kupanda kwa bei ya vifaranga.

Bei ya nafaka zinazotumika kuandaa chakula cha vifaranga imeongezeka kati ya asilimia tisa hadi asilimia 49 katika miezi sita iliyopita, taarifa za Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara inaonyesha.

Gunia moja la mahindi la kilo 100 lililokuwa linauzwa kwa wastani wa Sh71,304 Mei sasa linapatikana kwa Sh106,305, wakati lile la mchele linauzwa Sh290,594 kutoka Sh213,125 na maharage nayo yakipanda kwa Sh97,471 na kuuzwa Sh296,000, huku gunia la mtama likipanda kwa Sh10,577 na kuuzwa Sh127,500.

Hata hivyo, Serikali imewataka wafugaji kutokata tamaa na kwamba bei ya nafaka ikishuka, vyakula vya kuku vitapungua, hivyo kushusha gharama za uzalishaji. Bei ya kifaranga imesema itafika Sh 1,700.

Jesca Mbwana, mfugaji wa jijini Dar es Salaam alisema bei ya kifaranga kuwa juu inazidisha gharama za uendeshaji, akitolea mfano mfugaji wa kuanzia kuku 400 atatakiwa kuwa na zaidi ya Sh2 milioni.

“Kifaranga kikiuzwa Sh2,100 kuku akikua atauzwa kuanzia Sh6,000 hadi Sh6,500 kwa bei ya jumla. Muda mwingine tunapata hasara ukiwa na kuku wengine bandani halafu mnunuzi wa jumla anataka kuwachukua chini ya bei uliyompangia na unakuwa huna jinsi inabidi uwauze,” alisema.

Wakati Jesca akieleza hayo, Stanley Gomezulu wa Himo mkoani Kilimanjaro alisema kifaranga cha siku moja kimepanda bei kutoka Sh1,500 hadi Sh2,200.

“Tulikuwa tunanunua kifaranga kwa kati ya Sh1,500 hadi Sh1,800 lakini sasa hivi tunapata kwa Sh2,000 hadi Sh2,200 kutegemea kampuni, hali ikiendelea hivi tutashindwa kufuga, maana hata bei ya chakula ipo juu. Gharama za maisha zimepanda, hii imesababisha kila kitu kupanda bei, maana chakula cha kuku, hasa vifaranga kilo moja ni Sh2,400 hadi Sh2,500 wakati tulikuwa tukinunua kwa Sh1,500 hadi Sh1,800,” alisema.

Hata bei ya vifaranga wa kuku chotara, Mary Kavishe alisema imepanda pia. “Wakati vifaranga wa kuku wa nyama wakipanda hadi Sh2,200, wale wa chotara wametoka Sh1,300 hadi Sh1,500,” alisema Mary.

Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Organia, Albert Sokotra alisema bei imepanda kutokana na kuongezeka kwa ngarama za uzalishaji ila hakuna upungufu wa vifaranga sokoni.

“Gharama ya nafaka kama mahindi imeongezeka kutoka Sh450,000 kwa tani moja hadi Sh1.1 milioni, soya ni Sh2.3 milioni hadi Sh2.4 milioni kutoka kati ya Sh1.4 milioni hadi Sh1.5 milioni,” alisema Sokotra.

Ramadhani Said alisema kama mfugaji alikuwa unatumia Sh4 milioni, sasa atatakiwa kuwa na Sh6 milioni kufuga idadi ileile ya kuku, hivyo kuwa ngumu kupata faida maana kuna kuku wengine watakufa kabla ya kukua.

Muuzaji wa chipsi eneo la Mabibo jijini Dar es Salaam, Hassan Juma kupanda kwa bei ya kuku kumepunguza faida yao.

“Bei ilipokuwa chini ya Sh6,000 tulikuwa tunapata faida hadi Sh4,000 lakini sasa hali imekuwa ngumu. Kuku anajulikana huwezi kupunguza kipimo wala kupandisha bei. Ni hasara kwani unatakiwa kulipa umeme, kodi na wafanyakazi,” alisema Hassan.

Meneja Uendeshaji wa kampuni ya Kibo Poultry, Vaileth Edward alisema kabla ya Juni walikuwa wanauza kifaranga kimoja kwa Sh1,800, lakini sasa ni Sh2,100.

“Malighafi za kuandalia chakula cha kuku wazazi zipo juu, kilo ya dagaa imepanda hata virutubisho vinavyotumika kuchanganyia chakula navyo vimepanda. Virutubisho vinatoka Urusi, lakini sasa upatikanaji wake umekuwa mgumu na bei yake ipo juu,” alisema.

Ili kuwahakikishia soko nchini, Vaileth alisema “tunaiomba Serikali iwape kipaumbele wazalishaji wa vifaranga wa ndani kwa kupunguza uingizaji wa vifaranga kutoka nje ya nchi.”

Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Profesa Hezron Nonga alisema zaidi ya asilimia 90 ya chakula cha kuku kinatengenezwa kwa kutumia nafaka ambazo bei zake zimepanda pia.

Hata hivyo, aliwahakikishia wafugaji na wazalishaji kwamba bei ya nafaka itashuka hivi punde na gharama za uzalishaji zitapungua hivyo bei itarudi.

“Wakati wa mlipuko wa Uviko-19 vifaranga vilikuwa vinauzwa hadi Sh2,800, lakini sasa hivi uhaba wa nafaka ndio unasababisha kupanda kwa bei, ni hali ya kawaida katika biashara na itatengamaa.

“Biashara ya kuku inabadilika mara kwa mara kulingana na hali na wakati, sasa hivi ni kiangazi na upatikanaji wa nafaka ni mgumu, wasiwe na wasiwasi, neema inakuja na kila kitu kitakuwa sawa,” alisema Profesa Nonga.

Profesa Nonga pia alizitaka kampuni hizo kuzalisha vifaranga vingi na wasiutumie mwanya huo kupandisha bei.