Wajasiriamali biashara ya mazao ya kilimo kushikwa mkono

Kutoka kushoto, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa; Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dk Benson Ndiege; Mtendaji Mkuu wa Tume ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB), Asangye Bangu na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Bidhaa Tanzania (TMX), Godfrey Malekano wakisaini mkataba wa ushirikiano wa kuwainua wakulima na wajasiriamali wadogo wa sekta ya kilimo katika hafla iliyofanyika mwisho mwa wiki makao makuu ya Benki ya CRDB.

Muktasari:

Watakaonufaika zaidi ni wanawake na vijana

Dar es Salaam. Katika kuwainua wakulima na wajasiriamali wa biashara ya mazao ya kilimo, Taasisi ya CRDB Bank Foundation imesaini mkataba wa ushirikiano na Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC).

Mkataba huo pia umesainiwa na Tume ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) na Soko la Bidhaa Tanzania (TMX).

Akizungumza wakati wa kusaini mkataba huo, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa amesema mchango wa kilimo ni mkubwa kuanzia kwenye uzalishaji wa chakula hadi utoaji wa ajira hasa kwa wanawake na vijana.

Amesema azma ya taasisi hiyo ni kusaidia kuongeza ujumuishi wa kiuchumi, kuboresha maisha, na kukuza ustawi wa jamii.

Ili kufikia malengo hayo amesema taasisi hiyo hubuni na kutekeleza programu za uwezeshaji kama vile Imbeju ambayo imewafikia wanawake zaidi ya 125,000 na kutoa mitaji wezeshi zaidi ya Sh5 bilioni.

Amesema watashirikiana na mdau yeyote anayelenga kuwakomboa kiuchumi vijana na wanawake kuwapa nafasi ya kuujenga uchumi wa Taifa.

“Ushirikiano huu unajielekeza zaidi kwenye sekta ya kilimo inayotoa ajira kwa zaidi ya asilimia 75 ya Watanzania na kuchangia asilimia 26 kwenye Pato la Taifa, huku kikituhakikishia chakula kwa asilimia 95,” amesema.

Mkurugenzi huyo amesema katika wilaya wanatarajia kuzifikia Amcos (vyama vya ushirika) 10 ambazo zitawezeshwa kwa kati ya Sh1 milioni hadi Sh30 milioni au zaidi kulingana na mahitaji yatakayokuwapo.

Amesema CRDB Bank Foundation itatoa elimu ya fedha, ujasiriamali na mtaji wezeshi, huku TCDC itaratibu upatikanaji wa vyama hai vya ushirika, na WRRB itahakikisha uhifadhi makini wa mazao ya kilimo na TMX itawakutanisha wakulima na wanunuzi wa mazao.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa TMX, Godfrey Malekano amesema jukumu lao ni kuhakikisha mkulima anapata bei nzuri ya mavuno yake.

Tangu mwaka 2018 soko hilo lilipoanzishwa, amesema wameshayasajili mazao ya ufuta, dengu, korosho, mbaazi na mazao ya mifugo, huku wakikamilisha utaratibu wa kuingiza madini.

Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa TCDC, Dk Benson Ndiege amesema kuna zaidi ya vyama 7,000 vya ushirika nchini ambavyo sasa vitaanza kunufaika na mkakati uliowekwa na wadau wanaoenda kuutekeleza.

Mtendaji Mkuu wa WRRB, Asangye Bangu amesema huu ni mwendelezo wa kuwainua wakulima nchini.

“Nguvu za kila mmoja wetu kwenye ushirikiano huu ni kubwa. Tunaenda kuyatekeleza yote tuliyokubaliana hapa kumnufaisha mkulima wa Tanzania,” amesema.