Yara Tanzania kusambaza lishe ya mifugo nchini

What you need to know:

Baada ya kufanya vizuri katika uzalishaji na usambazaji wa mbolea, Kampuni ya Yara Tanzania inatarajia kuanza kuzalisha lishe ya wanyama na kuku hapa nchini, hatua inayotajwa kuwa italeta mapinduzi katika sekta ya ufugaji.


Dar es Salaam. Baada ya kufanya vizuri katika uzalishaji na usambazaji wa mbolea, Kampuni ya Yara Tanzania inatarajia kuanza kuzalisha lishe ya wanyama na kuku hapa nchini, hatua inayotajwa kuwa italeta mapinduzi katika sekta ya ufugaji.

Mkurugenzi Mtendaji wa Yara Tanzania, Winstone Odhiambo, anasema kuwa kampuni hiyo itaanza kuuza vyakula na virutubisho vya aina mbalimbali vya vyakula vya mifugo katika soko la ndani kama sehemu ya dhamira yake ya kuinua kipato cha mamilioni ya wafugaji.

“Yara International (Kampuni mama) inazalisha bidhaa lishe kwa wanyama ambazo sasa zitakuwa zinapatikana na kusambazwa hapa Tanzania. Tumefurahishwa na safari hii mpya na tunatazamia kufanya kazi kwa karibu na wafugaji ili kuboresha wingi na ubora wa uzalishaji wa maziwa na nyama nchini Tanzania,” Alisema Odhiambo.

Odhiambo alisema hatua hiyo ya kuanza kuuza lishe za wanyama na ndege wafugwao inaenda sambamba na dhamira iliyoonyeshwa na viongozi na washiriki wa mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika (AGRF) uliomalizika wiki iliyopita jijini hapa.

Mojawapo ya mada ya mkutano wa AGRF iliwataka wadau kuchukua hatua za haraka kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, upotevu wa chakula, na uhaba wa chakula kabla ya mwaka 2030. Mkutano huo ulitoa wito wa kufanya kazi kwa pamoja ili kubuni sera na programu shupavu zinazounga mkono mifumo endelevu, inayostahimili na inayojumuisha chakula.

Kwa Yara kuleta lishe hizo hapa nchini kutaifanya Tanzania kuwa nchi ya tatu barani Afrika baada ya Afrika Kusini na Kenya walioanza hivi karibuni. Na uzinduzi wa lishe hiyo unatarajiwa kufanyika Septemba 19, 2023 mkoani Iringa.

Dk Peter Mukua, Mtaalam wa Lishe wa Yara aliyeko Nairobi, Kenya, alisema wafugaji watarajie bidhaa bora za lishe ya mifugo yote na kuku.

Mshauri wa Kiufundi wa Yara upande wa lishe za Wanyama kutoka Afrika Kusini Nico Brink alisema ujio wa bidhaa hiyo nchini Tanzania utakuwa na manufaa makubwa kwa wafugaji wa ng'ombe wa maziwa, wafugaji wa kuku, malisho ya mchanganyiko, malisho ya madini, Wanyamapori na pia ufugaji wa samaki.