Namna ya kumaliza uhaba wa maji maeneo ya vijijini

Muktasari:
- Wilaya hiyo, yenye wakazi 107,117 kwa mujibu wa ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) waliogawanyika katika vijiji 93, ni miongoni mwa wilaya kame katika Mkoa wa Mtwara ambazo wakazi wake hulazimika kutembea umbali mrefu kusaka huduma ya maji.
Ni zaidi ya kilomita 70 kutoka katika Wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara kufika katika Mto Ruvuma, moja ya vyanzo vya uhakika vya maji vinavyotegemewa kumaliza uhaba mkubwa wa maji unaowaathiri wakazi wa vijijini.
Wilaya hiyo, yenye wakazi 107,117 kwa mujibu wa ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) waliogawanyika katika vijiji 93, ni miongoni mwa wilaya kame katika Mkoa wa Mtwara ambazo wakazi wake hulazimika kutembea umbali mrefu kusaka huduma ya maji.
Hadi sasa ofisi ya maji Mkoa wa Mtwara inakadiria kuwa ni theluthi tu (asilimia 34.8) ya wakazi wote wa wilaya hiyo ndiyo hufikiwa na huduma ya majisafi na salama kutoka kwenye bomba na visima.
Uhaba wa maji si tu umeathiri wanawake kwa kutumia muda mwingi kutafuta maji kwa matumizi ya nyumbani badala ya kuzalisha mali, bali sekta ya elimu, afya na shughuli za kimaendeleo.
Wakazi wa wilaya hiyo hawawezi kuwa na kilimo cha umwagiliaji na hata shughuli za ujenzi kama vile nyumba zinaathiriwa na tatizo hilo. Wakazi wanaeleza kuwa gharama za ujenzi zinapanda kutokana na ukosefu wa maji ambapo ndoo ya lita 20 huuzwa kwa bei kati ya Sh1, 000 hadi Sh2,000 wakati wa kiangazi kikali.
Hata wale wanaoishi kandokando ya Mto Ruvuma wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya kushambuliwa na mamba mara kwa mara kutokana na kukosekana majisafi na salama.
Mtaalamu wa Maji wilayani humo, Mhandisi Rejea Ng’ondya anabainisha kuwa tatizo la wilaya hiyo linasababishwa na jiolojia ambapo hakuna vyanzo vya maji vya kudumu na maji hupatikana umbali mrefu ambayo hata pale yanapopatika hudumu kwa muda na hukakuka.
Hata hivyo, wananchi wanaona tatizo lao linaweza kusuluhishwa iwapo Serikali itawekeza fedha za kutosha kujenga mradi wa maji kwa kuyatoa Mto Ruvuma hadi Nanyumbu kama ambavyo imefanywa katika maeneo mengine.
Ally Nassoro mkazi wa kaya ya Chipuputa anasema kuna wakati wanalazimika kununua maji yanayotoka Mto Ruvuma, nayo hayakidhi mahitaji kutokana na kipato chao.
“Maji ya Mto Ruvuma yanafaa kwa matumizi lakini bei yake ni kubwa hata tunapowaomba wauzaji wapunguze bei wanalalamikia gharama za kukodi gari, pia wachotaji wa maji mtoni na wenyewe wanakuwa wanahatarisha maisha yao sababu ya mamba.

“Ili kumaliza tatizo hili Serikali na wadau watujengee mradi kutoa maji Mto Ruvuma kuyaleta kwa wananchi kama walivyofanya Mto Ruvu,” anasema Nassoro.
Ng’ondya anasema tatizo hilo litamalizwa kwa kutekelezwa kwa mradi mkubwa wa kutumia maji ya Mto Ruvuma ulioanza mwaka 2015 ambao kukamilika kwake kutategemea upatikanaji wa fedha na kwa sasa mradi huo unafanyiwa upembuzi yakinifu pekee.
Mradi huo kwa mujibu wa Ng’ondya utahusisha vijiji 29 pamoja na mji wa Mangaka ambapo wananchi wapatao 61,000 watanufaika.
Mkakati mwingine ni uchimbaji wa mabwawa makubwa matano kuanzia mwaka 2017 hadi 2021 yatakayowanufaisha watu 37,000.
Mikakati hiyo ya Serikali inaweka picha za matumani kwa wakazi hao hata hivyo swali linabaki ni lini utekelezaji huo utakamilika? Je, katika kipindi hicho chote wananchi hao watatumia vyanzo gani vya majisafi na salama ili kujiepusha na magonjwa ya tumbo na kutumia muda wao vema katika uzalishaji.

Mkazi wa Kijiji cha Mbambakofi wilayani Nanyumbu, Mtwara, Hamis Namanje akionyesha kisima wanachotumia kuhifadhi maji yanayowasaidia wakati wa kiangazi.
Wananchi wengi wanaitupia mzigo halmashauri kwa kushindwa kutatua kero yao. Hata hivyo, wengi hawajui kuwa kiwango cha bajeti kinachopangwa kutokana na mapato ya ndani kwa ajili ya kutatua tatizo hilo ndani ya halmashauri hiyo kinapungua mwaka hadi mwaka badala ya kuongezeka.
Mwaka 2015/16 halmashauri ilitenga bajeti ya Sh257.9 milioni hata hivyo kiasi kilichopelekwa kwenye maji ni Sh188.9 milioni. Angalau mwaka wa fedha uliofuatia walipata kidogo kiasi cha Sh241.8 milioni kati ya Sh246 milioni zilizokuwa zimepangwa.
Hata hivyo, katika mwaka wa fedha unaoendelea walitenga Sh80 milioni pekee pungufu mara tatu ya zile zilizotengwa mwaka 2016/17 na hadi sasa hakuna kilichotolewa licha ya robo ya kwanza ya mwaka wa fedha kwisha.
Wadau wa maendeleo wanasema kwa sasa utatuzi wa kero ya maji upo nje ya uwezo wa halmashauri hiyo hivyo jitihada za nje hususan Serikali Kuu zinahitajika kwa haraka kuwaokoa wakazi wa eneo hilo.
Mratibu Mtendaji wa shirika lisilo la kiserikali la Faidika Wote Pamoja (Fawopa), Komba Baltazari anasema yanapokosekana maji yanaathiri shughuli nyingi za maendeleo hivyo ni vyema sasa Serikali na wadau wakaangalia uwezekano wa kuongeza bajeti ya maji kwa Wilaya ya Nanyumbu.
Anasema watoa uamuzi kama baraza la madiwani na wabunge wanapaswa kuhakikisha wanapigania ongezeko la bajeti ya maji ili kuwaondolea wananchi wa wilaya hiyo kero ya kusaka maji katika umbali mrefu.
“Kama tunavyojua tatizo hili kwa kiasi kikubwa linakwenda kumuathiri mwanamke ambaye ndiye kwa kiasi kikubwa kwa desturi zetu ndio mwenye jukumu la kutafuta maji. Pia, tukumbuke wanawake ndio wenye majukumu mengine ya kijamii hasa kufanya shughuli za nyumbani,” anasema Komba.
Mratibu huyo anaeleza kuwa uhaba wa maji unawaathiri hadi wanafunzi wanaopoteza muda mwingi wakitafuta maji na huenda wakapata magonjwa kwa kuwa ni watumiaji wa maji mengi hasa msalani na huduma nyinginezo za shuleni.
“Mbali na mamlaka za kiserikali zinazohusika na kushawishi Serikali kuongeza bajeti kwenye sekta ya maji pia mashirika yasiyo ya kiserikali yaliyo na uwezo wa kuchangia bajeti ya maji ni vizuri wakafanya hivyo,” anasema.
Mzee Said Said, mkazi wa Wilaya ya Newala anasema ni vyema wananchi wa maeneo yote yanayokabiliwa na tatizo la upatikanaji wa maji wakapewa elimu namna ya kuvuna maji ya mvua ili kukabiliana na tatizo hilo.
Anasema baadhi ya watu wamechimba visima kwa ajili ya kuvuna maji, lakini wengi wao hawajui namna ya kuvitunza na ndio sababu inayosababisha baadhi yao kuhangaika zaidi wakati wa kiangazi.
“Maeneo ya vijijini baadhi yetu tumeweza kuchimba visima ambavyo tunavuna maji ya mvua. Mtu akiwa na uwezo anaweza kuchimba kisima kirefu na kukijengea ndani na nje ambapo kitatunza maji yasiishie ardhini lakini walio wengi wanajenga visima lakini unakuta kinavuja na wakati mwingine kiko wazi hivyo maji yanapungua kwa kukaushwa na jua la kiangazi,”anasema Said.
Ikumbukwe kuwa Nanyumbu hata kama una fedha za kutosha bado kwa wakati wa kiangazi kikali unaweza kukosa maji. Si kwa sababu watu hawahitaji fedha la hasha, bali hawajui wapi watapata maji zaidi ya kwenda Mto Ruvuma ambao ni zaidi ya kilomita 70.

Wakazi wa wilayani Nanyumbu Mkoa wa Mtwara wakichota maji kwenye moja ya vyanzo vichache vya maji vinavyopatikana wilayani humo.
Wakati huo kwa mujibu wa wenyeji maji hata yenye chumvi hupatikana umbali hadi kilomita 20 kutoka maeneo ya makazi na hivyo kuwa kero kubwa.
Katika kipindi hicho ni kitu cha kawaida kwao kushinda siku mbili hadi tatu bila ya kuoga.
“Mkeo ametoka saa 11 alfajiri kwenda kisimani na anarudi saa 8 mchana na ndoo moja ya maji hivi unapata wapi huo ujasiri wa kuoga,” anahoji Yusufu Uledi mkazi wa Mangaka.
Kauli ya mbunge
Mbunge wa Nanyumbu, Duwa Nkurua anabainisha kuwa halmashauri yake imenunua mtambo wa kuchimba visima ili kurahisisha kazi ya uchimbaji visima, lakini mtambo hauonekani kuwa na tija kwa sababu kila wanapochimba hawapati maji au maji hudumu kwa muda mchache na kisha kukauka.
Pia, kukauka kwa mito ya msimu inayokatiza ndani ya halmashauri hiyo kunaweza kuwa kielelezo cha uharibifu wa mazingira na kushindwa kuhifadhi vyanzo vya maji.
Wenyeji wanasema katika mji wa Mangaka miaka 25 iliyopita kulikuwapo na chanzo cha maji cha Mkeweni, lakini kutokana na uhifadhi hafifu kwa sasa kimekauka na chanzo cha maji cha Ndwika ambacho nacho kimekufa.
Ni vyema sasa kukaanzishwa kampeni maalumu ya kuhifadhi vyanzo vya maji kwa sababu hata kama yatajengwa mabwawa bado yanaweza kukauka kama yalivyokauka baadhi ya mabwawa ikiwemo la Maneme.
Mito ambayo chimbuko lake lipo ndani ya wilaya hiyo ni mingi ukiacha Mto Masyalele ambao chimbuko lake ni katika Kijiji cha Mara ambao uliwahi kuwa mto wa kudumu miaka 30 iliyopita, Mto Mangaka na Mto Kalipinde ambayo yote vyanzo vyake vinajulikana.
Mkazi wa Kata ya Sengenya, mzee Shaibu Dadi anasema wilaya hiyo ilikuwa na vyanzo vya maji vya kuaminika, lakini kwa sasa vimekauka kutokana na uharibufu wa mazingira na hivyo hutiririsha maji pindi mvua kubwa inaponyesha basi.

Wananchi wa Kijiji cha Mnunia Kata ya Kilimanihewa wilayani Nanyumbu, Mkoa wa Mtwara wakiwa kwenye foleni ya kuchota maji kisimani.
Anasema miaka ya zamani kulikuwa na mto unaojulikana kama Mto Masyalele uliokuwa ukitoa maji yaliyowasaidia wananchi kwa ajili ya matumizi yao, lakini baadhi ya wananchi waliamua kufanya shughuli za kijamii kando ya mto huo ukakauka.
“Miaka 30 iliyopita tulikuwa na mto uliotiririsha maji, lakini siku hizi umekauka hauna faida yoyote, na hii yote ni sababu ya watu wasiokuwa na uelewa wa mazingira kuendesha kilimo kwenye maeneo ya mito siku hadi siku tumeshtukia umekauka maji tunayafuata mbali,”anasema Dadi
Aidha anasema pia, kulikuwa na mito mingine kama Mangaka na Kalipinde iliyopo Kata ya Kilimanihewa, lakini yote imekauka baada ya watu kushindwa kuitunza.
Anadai wakati mito hiyo ikiwa hai baadhi ya wafugaji waliitumia kama sehemu ya kunywesha mifugo yao maji licha ya kuwa maji yake pia yalitumika kwa matumizi ya nyumbani.
“Unakuta mtu ana mifugo yake anaielekeza mtoni kunywa maji badala ya kuiandalia mazingira ambayo yatafaa kwa wanyama kupata maji na matokeo yake mifugo iliharibu mazingira. Watu wengine wasiokuwa waelewa walikwenda mbali zaidi wakaanzisha kilimo cha umwagiiaji jirani na vyanzo vya maji,”anasema mzee Dadi
Mkazi wa Mnunio Kata ya Kilimanihewa Zainabu Mkate anasema uharibifu wa mazingira katika wilaya hiyo ndio umesababisha kuathiriwa zaidi na tataizo la maji kutokana na elimu duni juu ya utunzaji wa mazingira.
“Watu wangekuwa na elimu ya kutunza mazingira wala tusingekuwa tunapata shida kama msimu huu wa kiangazi. Watu waliendeshea shughuli zao kwenye mito na hakukuwa na mtu wa kuwazuia lakini kwa sasa adha ya maji inatuumiza kiu na mto mkubwa uliobaki uko mbali kwetu hapa tabu tu mto Kalipinde tuliokuwa nao umebaki kukaa nyoka na wadudu,”anasema Mkate.
Wakazi hawa wanajua chungu ya ukosefu wa maji, hivyo wakihamasishwa kutunza vyanzo vya maji kwa sasa watakuwa tayari kwa nguvu zote kulinda vyanzo vya maji na mazingira badala ya kusubiri maji ya Mto Ruvuma ambayo nao unaweza kukauka endapo hautahidhiwa vyema.
Iwapo jitihada hizo zitazingatiwa wilaya ya Nanyumbu inaweza kuandika historia tatizo la maji ambalo kila uchao linaonekana kukuwa huku jitihada za kulipatia ufumbuzi zikisuasua na kuondoa matumaini ya wananchi kuwa huru na kero hiyo.