Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Shangwe China ikifungua mipaka bila karantini

Beijing, China. Kwa mara ya kwanza, raia wameanza kuingia nchini China bila kulazimika kukaa karantini ikiwa ni miaka mitatu tangu amri hiyo ilipowekwa ili kukabiliana na janga la uviko-19 lililoanzia nchini humo mwaka 2019.

Hivi karibuni, Serikali ya China ilitangaza kuondoa ulazima huo na jana abiria wa kwanza waliwasili nchini humo wakitua katika viwanja vya ndege vya miji ya Guangzhou na Shenzhen.

Abiria 387 kutoka Singapore na Canada hawakufanyiwa vipimo vya Uviko-19 walipowasili na hawakulazimika kukaa karantini kama ilivyokuwa awali huku Serikali ikisema ongezeko la maambukizi ya Uviko-19 halina hatari yoyote na wahudumu wa afya wanaweza kulimudu.

Rais wa China, Xi Jinping amewakumbusha wataalamu hao kufanya kila kinachowezekana kuokoa maisha ya yeyote atakayebainika kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo.

Tangu Machi 2020, abiria wote waliokuwa wanaingia China walilazimika kukaa karantini kwa wiki tatu lakini kwa sasa, pale itakapobidi basi itakuwa ni siku tano tu.

Miezi miwili iliyopita, yaliibuka maandamano yaliyopinga sheria hiyo nchini China kiasi cha kuwalazimu askari polisi kutumia nguvu kuwatawanya waandamanaji huku wakiwakamata baadhi yao.

Maelfu ya watu waliandamana wakilalamikia masharti makali ya kuzuia kuenea kwa virusi vya Uviko-19 chini ya sera ya Serikali kutaka kutokuwa na maambukizi ya ugonjwa huo kabisa. Maandamano hayo yalifanyika katika miji ya Beijing na Nanjing yakihusisha hasa wanafunzi wa vyuo vikuu.

Waandamanaji waliochukizwa na masharti ya kuwekwa karantini walijitokeza pia Shanghai wakikitaka chama tawala kuondoka madarakani.

Maandamano hayo yalifanyika siku chache baada ya watu 10 kufariki dunia kutokana na moto uliozuka katika jengo la ghorofa lililokuwa likikaliwa na watu mjini Urumqi.

Kuna wasiwasi kwamba huenda masharti ya watu kutoondoka nyumbani kwao ililizuia Jeshi la Zimamoto nchini humo kwenda kuwaokoa watu hao jambo lililpandisha hasira za wananchi.

Urumqi umekuwa chini ya amri ya watu kutotoka nyumbani tangu Agosti 2020 na ripoti zilieleza karibu kila siku kulikuwa na maambukizi mapaya 100 ya Uviko-19.

Mwaka 2020 China ilitangaza kuzuia wageni wote kuingia nchini humo hata kama wana viza au vibali, lengo likiwa kudhibiti maambukizi ya Uviko-19.

China pia iliagiza ndege za nchi hiyo na zile za kigeni kufanya safari moja tu kwa wiki na hazitakiwi kujaza watu kwa zaidi ya asilimia 75.

Zuio hilo lilikuja baada ya China kubaini wagonjwa 55 wenye maambukizi ya Uviko-19, kati yao 54 walikuwa ni wageni kutoka nje ya nchi hiyo.

Wizara ya Mambo ya Nje ya China ilisema inasitisha kwa muda watu kutoka mataifa mengine kuingia nchini humo kutokana na maambukizi hayo.

Zuio hilo liliwahusu watu wenye viza na wale wenye vibali vya ukazi lakini halikuwahusu wanadiplomasia na wahudumu wa ndege na wote wenye viza daraja C.