Al Jazeera kupigwa marufuku Israel
Muktasari:
Israel imesema vyombo vyote vinavyoonekana kuwa na uhasama na Taifa hilo vitapigwa marufuku kwa mujibu wa sheria mpya iliyopitishwa na Bunge
Israel. Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, ameahidi kupiga marufuku Kituo cha Al Jazeera kurusha matangazo kukiita ni cha kigaidi.
"Chaneli ya kigaidi ya Al Jazeera haitatangaza tena kutoka Israel. Ninakusudia kuchukua hatua mara moja kwa mujibu wa sheria mpya kusimamisha shughuli za idhaa hiyo," AFP imemnukuu Netanyahu jana Aprili mosi 2024 kama alivyoandika kwenye X, zamani Twitter.
Hatua hiyo inakuja baada ya Bunge la nchi hiyo (Knesset) kupitisha sheria inayoruhusu Serikali kuvifungia vyombo vya habari vya kigeni.
Sheria hiyo pia, inampa Waziri Mkuu na Waziri wa Mawasiliano mamlaka ya muda ya kufunga mitandao ya habari ya kigeni inayoonekana kutishia usalama wa taifa kwa siku 45.
Aidha, Waziri wa Mawasiliano Shlomo Karhi amesema mashirika mengine ya matangazo ambayo inayaona kuwa yana uhasama kwa Israel katika kuripoti kuhusu mgogoro wa Gaza, pia yatazuiwa kufanya kazi nchini humo.
Kufuatia sakata hilo, Marekani imeonesha wasiwasi juu ya hiyo sheria huku Katibu wa Habari wa Ikulu ya White House, Karine Jean-Pierre akisema: "Tunaamini katika uhuru wa vyombo vya habari. Ni muhimu sana. Marekani inaunga mkono kazi muhimu inayofanywa na wanahabari duniani kote, hiyo inajumuisha wale wanaoripoti kuhusu mzozo wa Gaza. Ikiwa taarifa hizo ni za kweli, zinatuhusu sisi.”
Hata hivyo, Al Jazeera imesema hatua hiyo inakuja kama sehemu ya mfululizo wa mashambulizi ya Israel ya kunyamazisha shirika hilo.
(Imeandaliwa na Sute Kamwelwe)