Bunduki za jeshi zatumika katika uhalifu Uganda

Muktasari:
- Polisi mjini Kampala jana wamesema silaha za jeshi zimekuwa zikitumika kufanya uhalifu karibu na Kampala na kusababisha vifo vya watu wengi katika wiki za hivi karibuni.
Uganda. Polisi mjini Kampala jana wamesema silaha za jeshi zimekuwa zikitumika kufanya uhalifu karibu na jiji hilo na kusababisha vifo vya watu wengi katika wiki za hivi karibuni.
Katika moja ya matukio ya hivi karibuni ya unyang’anyi wa kutumia silaha Juni 30 mwaka huu, askari mmoja kutoka kambi ya Jeshi ya Kikubamutwe iliyopo barabara ya Kayunga wilayani Mukono, alivamia duka la kubadilisha fedha katika eneo la Luzira, jijini Kampala na kuiba fedha za Uganda Sh72 milioni.
Msemaji wa polisi wa Kampala, SP Patrick Onyango, ameiambia mtandao wa Monitor kwamba maafisa wa eneo la uhalifu wamefanikiwa kupata bunduki aina ya AK47 ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda (UPDF) baada ya tukio hilo la Luzira.
Polisi wanasema askari huyo mhalifu ndiye chanzo cha bunduki zilizotumika katika matukio ya wizi ya hivi karibuni katika Wilaya ya Mukono.
Inasemekana mtuhumiwa huyo alipangiwa kazi ambayo ilimpa nafasi ya kuingia kwenye ghala la silaha katika kambi ya Kikubamutwe ambako alitoa silaha kwa ajili ya kuzikodi kinyume cha sheria. Mnamo Juni 30, watu wawili waliokuwa na silaha walivamia na kufyatua risasi hewani katika mahabusu moja huko Luzira na kusababisha Aggrey Bahati na Annah Nyamukulu waliokuwa wamewekwa mahabusu kutoroka.
Mhudumu wa eneo hilo, Betty Nakigudde, alijeruhiwa katika machafuko yaliyofuata huku Richard Ssenondo alipigwa risasi na baadaye kufariki kutokana na majeraha yake.
“Polisi wamefanikiwa kuwakamata watuhumiwa wawili, akiwemo afisa wa UPDF,” SP Onyango amesema, na kwamba watuhumiwa hao sasa wako chini ya ulinzi wa kijeshi.
Naibu msemaji wa jeshi, Luteni Kanali Deo Akiiki, hata hivyo, aliwatoa hofu wananchi huku akisema upelelezi unaendelea.
“Hilo ni kosa la kiraia, si kosa la utumishi. Polisi wanabaki kuwajibika. Iwapo yeyote kati yetu atafanya kosa la madai, basi taratibu za kawaida kwa polisi hufanyika, ingawa jeshi linavutiwa kuona uwezekano wa kuwashtaki maafisa kama hao katika mahakama ya kijeshi," alisema Akiiki.
Afisa wa upelelezi anayeendelea na uchunguzi wa mauaji ya Luzira ameiambia Monitor kuwa polisi wanachunguza madai kwamba askari huyo alifika eneo la tukio akiwa na bunduki mbili.
Askari wa upelelezi amesema mtuhumiwa huyo alipohojiwa alisema silaha moja ilikuwa ni ya askari mwenzake ambaye yuko mapumzikoni kwa sasa huku akisema alipata silaha kinyume cha sheria kutokana na kuwekwa kwake katika ghala la silaha la kitengo chake.
Afisa wa upelelezi alisema askari huyo pia alikiri kuwa kwamba amekuwa akikodisha bunduki za UPDF kwa majambazi katika wilaya za Mukono, Wakiso na Kampala.