China kuchukua jukumu la upatanishi mgogoro wa Niger

Muktasari:

  • Mwanadiplomasi huyo ameyasema hayo katika mahojiano Jumatatu usiku kwenye televisheni ya taifa ya Niger, mara baada ya baada yakukutana na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Ali Mahaman Lamine Zeine, aliyeteuliwa na wanajeshi kushuka wadhifa huo.

Dar es Salaam. Balozi wa China nchini Niger, Jiang Feng, amesema nchi yake inakusudia kuchukua jukumu la usuluhishi katika mzozo wa kisiasa unaoendelea nchini humo.

 Mwanadiplomasi huyo ameyasema hayo katika mahojiano aliyofanya Jumatatu Septemba 4, 2023 kwenye televisheni ya taifa ya Niger, mara baada ya kukutana na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Ali Mahaman Lamine Zeine, aliyeteuliwa na wanajeshi kushika wadhifa huo.

"Serikali ya China inakusudia kuchukua jukumu la kuwa mpatanishi, kwa ili kutafuta suluhisho la kisiasa la mzozo huu wa Niger," amesema balozi huyo katika mahojiano hayo.

"China inafuata misingi na kanuni ya kutoingilia mambo ya ndani ya nchi nyingine, tunahimiza nchi za Afrika, kutatua matatizo yao kwa njia amani kupitia meza za mazungumzo,” amesema balozi huyo.

Duru za kisiasa zinabainisha kuwa China ni mshirika mkuu wa kiuchumi wa Niger, hasa katika sekta ya nishati.

Nchi hizo mbili zinajenga bomba la mafuta la kilomita 2,000 ambalo ni refu zaidi barani Afrika, linalokusudiwa kusafirisha mafuta ghafi kutoka mashamba ya Agadem (kusini-mashariki mwa Niger) hadi bandari ya Sèmè nchini Benin.

Visima vya mafuta vya Agadem vinatumiwa na kampuni ya mafuta ya China National Petroleum Corporation (CNPC), ambayo pia imejenga kiwanda cha kusafisha mafuta huko Zinder, kusini mwa Niger, chenye uwezo wa kubeba mapipa 20,000 kwa siku na kwamba kampuni hiyo ya China ina asilimia kubwa ya hisa katika kiwanda hicho.

Makampuni ya China pia yanafanya kazi ya ujenzi kwenye bwawa la Kandadji liliko Mto Niger, mradi wa pharaonic wenye thamani ya faranga za CFA bilioni 740 (sawa na euro bilioni 1.1), ulioko magharibi mwa nchi, ambao unapaswa kuzalisha GWh 629 kila mwaka ili kuwezesha Niger kujikomboa kutoka kwa utegemezi wake wa nishati kwa nchi jirani ya Nigeria.

Kufuatia mapinduzi hayo, Nigeria ililazimika kusitisha usambazaji wake wa umeme nchini Niger, kutokana na vikwazo vilivyoamuliwa na Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (Ecowas).