Faili la Hamas, Israel latua ICC

Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), Karim Khan.

Muktasari:

  • Hatua hii inakuja baada ya Wakili François Zimeray, raia wa Ufaransa, kutangaza kuwa amewasilisha malalamiko kuhusu uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya binadamu na mauaji ya halaiki katika mahakama hiyo, na kwamba hayo ni madai ya familia tisa za wahanga wa shambulio hilo.

Dar Es Salaam. Ofisi ya Mwendesha Mashitaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), imesema itapitia taarifa zilizowasiliwa kuhusiana na shambulio la Oktoba 7, 2023 lililofanywa na wanamgambo wa Hamas ili kujiridhisha kama uhalifu unaotajwa uko chini ya mamlaka yake.

Pia ICC inataka kujiridhisha kama uhalifu huo pia unaweza kuhusishwa na uchunguzi wake unaoendelea kuhusu hali ya Palestina. Hata hivyo, mahakama hiyo iliyoko Hague, hailazimiki kuishughulikia.

Wakati watu zaidi ya 250 waliuawa katika shambulio la Oktoba 7, mamlaka za Israel zimesema kwa ujumla, zaidi ya watu 1,400, hasa raia, waliuawa katika shambulio hilo.

Aidha, tangu Israel ianze mashambulizi ya kulipa kisasi Ukanda wa Gaza, ripoti ya Ijumaa inaonyesha watu 9,227, wakiwemo watoto 3,826, wameuawa katika mashambulizi ya Israel katika eneo hilo.

Licha ya maombi ya kuchunguza kile kilichofanywa na Hamasi kwa Israel, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC, Karim Khan amesema ofisi yake pia inachunguza mashambulizi ya Israel huko Gaza.

“ICC inachunguza uhalifu ambao unaweza kuwa ulifanywa nchini Israel mnamo Oktoba 7, lakini pia matukio yanayoendelea huko Gaza na Ukingo wa Magharibi ni sehemu ya uchunguzi rasmi wa ICC,” amesema Mwendesha Mashtaka huyo.

Aidha, Mahakama hiyo pia iliombwa na Shirika lisilo la Kiserikali la Reporters Without Borders kufanya uchunguzi kuhusiana na uhalifu wa kivita uliofanywa dhidi ya waandishi wa habari nchini Palestina na Israel.

Hatua hii inakuja baada ya Wakili François Zimeray, raia wa Ufaransa, kutangaza kuwa amewasilisha malalamiko kuhusu uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya binadamu na mauaji ya halaiki katika mahakama hiyo, na kwamba hayo ni madai ya familia tisa za wahanga wa shambulio hilo.

Mtandao wa RFI umeripoti kuwa wakili huyo anadai: “Shambulio lililotekelezwa Oktoba 7 na Hamas nchini Israel, ni utekelezaji wa mradi wa mauaji ya halaiki uliotangazwa na wahusika wa shambulio hilo...ukweli lazima ulindwe, ukatili huu lazima ujulikane na kuandikwa katika kumbukumbu ya pamoja.”

Pia imeelezwa kuwa, Wakili Zimeray amemwomba mwendesha mashtaka wa ICC "kuzingatia ushauri wa kutoa hati ya kimataifa ya kukamatwa kwa viongozi wa Hamas."

Inadaiwa kuwa Wakili huyo amegeukia ICC, kwa sababu ndiyo "mrithi" wa kesi ya Nuremberg. "Hili ndilo jambo bora zaidi ambalo jumuiya ya kimataifa imejenga ili kukabiliana kwa usahihi na ukatili mkubwa."

Chanzo RFI