ICC yatoa waranti kukamatwa Putin kwa makossa ya kivita

Rais wa Russia, Vladimir Putin.

Muktasari:

  • ICC imesema waranti hiyo imetolewa kwa kutuhumiwa kujihusisha na uhamishwaji wa watoto kutoka kwenye maeneo yaliyotekwa nchini Ukraine na kuwapeleka Russia.

Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa kivita (ICC) imetoa waranti ya kukamatwa kwa Rais wa Russia, Vladimir Putin kwa madai ya kutenda makossa ya kivita nchini Ukraine.

Taarifa iliyochapishwa leo Machi 17 kwenye mtandao wa AlJazeera imeinukuu taarifa ya Mahakama hiyo iliyo nchini The Hague ikisema kuwa waranti hiyo imetolewa kwa kutuhumiwa kujihusisha na uhamishwaji wa watoto kutoka kwenye maeneo yaliyotekwa nchini Ukraine na kuwapeleka Russia.

“Kuna sababu za msingi kuamini kwamba Putin anahuisika na jinai kwa makossa yaliyotajwa hapo juu,” imeongeza taarifa ya mahakama hiyo.

ICC pia imetoa waranti ya kukamatwa kwa kamishina wa haki za watoto katika ofisi ya Rais, Maria Alekseyevna Lvova-Belova, kwa makossa hayo hayo.

Hii ni mara ya kwanza kwa ICC kutoa waranti ya kukamatwa kwa Rais aliye madarakani na ambaye nchi yake ni mwanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.