Fangasi wawatesa wanajeshi Israel, mmoja afariki

Muktasari:

  • Taarifa zinaeleza wanajeshi wa IDF wameambukizwa fangasi wakiwa vitani na kusababisha mmoja wao kufariki dunia.

Gaza. Leo ikiwa ni siku ya 81 ya mapambano kati ya Jeshi la Israel (IDF) na kundi la Hamas, imeelezwa mbali ya vifo vya mtutu wa bunduki na makombora, pia fangasi wamekuwa tishio kwenye vita hivyo.

Taarifa za hivi punde kutoka gazeti la Times of Israel zinasema mwanajeshi mmoja wa IDF amefariki dunia kutokana na fangasi huko Gaza.

“Mwanajeshi huyo aliletwa katika kituo cha matibabu Assuta Ashdod wiki mbili zilizopita akiwa na majeraha mabaya kwenye viungo vyake.

“Licha ya matibabu aliyoyapata, majeraha yalionekana kuwa sugu kutibika na baadaye askari huyo akafariki dunia,” imeeleza tovuti hiyo.

Hadi sasa takriban wanajeshi 10 wanaaminika kuambukizwa fangasi na wanaendelea na matibabu nchini kwao Israel.

Mkurugenzi wa zamani wa kitengo cha magonjwa ya kuambukiza cha Sheba Medical Center, ameiambia redio ya Kan leo asubuhi kuwa chanzo cha fangasi hao kinaaminika kuwa udongo wa ardhini ambao umechafuliwa na maji taka.

Maambukizi hayo huyapata kupitia majeraha yanayotokana na wanajeshi wanaopigana huko Gaza.

Jeshi la IDF linachunguza kama maambukizi ya fangasi hao yameanzia kwenye mahandaki ya Hamas wakati wa operesheni ya ardhini ama la.

Katika hatua nyingine, Jumuiya ya Magonjwa ya Kuambukiza ya Israeli inatarajiwa kufanya majadiliano ya dharura wiki ijayo na wataalamu wa magonjwa ya milipuko kutoka IDF na Wizara ya Afya.

Hatua hiyo inakuja kutokana na hali ya wanajeshi kuambukizwa magonjwa wakati wa mapigano ya Gaza.

Mpinzani amlaumu Netanyahu

Wakati hayo yakiendelea kuushangaza umma, televisheni ya Al Jazeera imemnukuu kiongozi wa upinzani wa Israel, Yair Lapid akisema Netanyahu 'hawezi kuendelea' kuwa waziri mkuu wa nchi hiyo.

Kiongozi huyo wa upinzani nchini humo, amesisitiza wito wake wa kumtaka Waziri Mkuu, Benjamin Netanyahu kujiuzulu.

“Kubadilisha waziri mkuu katikati ya vita si vizuri, lakini aliye madarakani ni mbaya zaidi. Hawezi kuendelea,” amesema.

Inaelezwa kuwa Lapid amekataa kujiunga na baraza la mawaziri la vita la Netanyahu mwanzoni mwa vita vya Israel na Hamas na amekuwa mkosoaji wa mara kwa mara wa Serikali ya mrengo mkali wa kulia ya Netanyahu.