Kim kutembelea kiwanda cha kuunda ndege za kivita Russia

Rais wa Russia, Vladimir Putin akisalimiana na Rais wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un. Picha na Maktaba

Muktasari:

  • Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un amewasili leo katika mji wa Komsomolsk-on-Amur ulioko nje kidogo mashariki mwa Russia Urusi.

Dar es Salaam. Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un amewasili leo katika mji wa Komsomolsk-on-Amur ulioko nje kidogo mashariki mwa Russia, akitarajiwa kukitembelea kiwanda kinachotengeneza ndege za kivita na vifaa vingine nchini humo.

Taarifa kutoka shirika la habari la Urusi TASS, na kuripotiwa na BBC, zimeleza kuwa kiwanda hicho ambacho kiongozi huyo wa Korea Kaskazini anatarajia kukitembelea, ni mahsusi kwa kutengeneza ndege za kisasa za kivita za Rusia.

Taarifa zaidi zinasema kuwa jana Alhamisi Septemba 14, 2023; Kim Un akiwa ameongozana na Rais wa Russia Vladimir Putin, waliofanya ziara kwenye kituo cha safari za anga za mbali cha Vostochny Cosmodrome.

Hata hivyo, nchi za Korea Kusini na Marekani, zimeelezea wasiwasi wao kuhusiana na ziara ya Kiongozi huyo nchini Russia, wakidai lengo lake ni kupanua wigo wa ushirikiano wa kijeshi kati ya nchi hizo mbili na hasa kuweka makubaliano ya ya kubadilishana silaha na teknolojia.

Wasiwasi was Washington na Seoul unakuja kufuatia hisia kuwa Korea Kaskazini huenda ikiipatia silaha Russia, huku na yenyewe ikinufaika kwa kupata teknolojia za hali ya juu zinazohusiana na satelaiti za kijasusi za kijeshi.

Ziara hii ya leo, inakuja huku bila kutarajiwa, kiongozi huyo wa Korea Kaskazini akiongeza muda wa ziara yake nchini Russia bila kutarajiwa.

Katika mazungumzo kati ya viongozi hao wawili, imeelezwa kuwa Rais Putin amekubali mwaliko wa Kim Un kutembelea Korea Kaskazini.

Kiongozi huyo wa Korea Kaskazini alitarajiwa kusimamia maonyesho ya meli za kivita za Russia, na pia kutembelea viwanda kadhaa na kusimama karibu na mji wa mashariki wa Vladivostok akielekea nyumbani kwake.