M23 walianzisha upya DRC, wateka kijiji

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa (UN), Novemba 2022, waasi wa M23 wameua watu 171 huko Kishishe, wengi wao wakiwa ni vijana na wanaume ambao walituhumiwa kuwa wanamgambo, japokuwa waasi hao wamekanusha kufanya mauaji hayo.

DRC. Kundi la waasi la M23 limekiteka kwa mara nyingine Kijiji cha Kishishe kilichopo Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ambako wanadaiwa kufanya mauaji mwishoni mwa mwaka jana.

Mtandao wa Daily Monitor umeripoti kuwa waasi hao wanaoongozwa na Watutsi, pia wanadaiwa kuungwa mkono na Rwanda kulingana, waliondoka katika kijiji hicho mwanzoni mwa Aprili, wakati huo waliyaachia maeneo mengine katika Mkoa wa Kivu Kaskazini.

Hata hivyo, baada ya miezi sita ya utulivu, mapigano makali yalianza tena mapema Oktoba mwaka huu kati ya waasi na jeshi la DRC, likishirikiana na makundi yanayojiita Wazalendo yenye silaha.

Tangu wakati huo, M23 wameyashikilia kwa mara nyingine maeneo ambayo awali waliyaachia.

 Kwa mujibu wa vyanzo vya habari kutoka Goma ambao ni Mji Mkuu wa Mkoa wa Kivu Kaskazini, Kijiji cha Kishishe wakazi wake wamekimbia na mapigano yameendelea kwa siku mbili, kabla ya jeshi kuingilia kati.

"Wavamizi hao walifanya mashambulizi," amesema ofisa mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe, akiongeza kuwa waasi hao walisaidiwa na Jeshi la Rwanda.

 "Hawa ni Wanyarwanda wanaotushambulia," amesema.

"Kishishe imedhibitiwa na M23 tangu Jumatatu,” amesema mwakilishi wa kutoka moja ya shirika la lisilo la kiserikali katika eneo hilo, taarifa ambazo baadaye zilithibitishwa na vyombo vya usalama.

"M23 wapo Kishishe... Watu wamekimbilia maeneo ya jirani ya Kirima, Mutanda, Kanyabayonga na Kibirizi," amesema ofisa wa kijiji hicho.

"Kuna taharuki Kibirizi, watu waliokimbia makazi yao wanafika kwa wingi", amesema mkazi mmoja.

Amesema wanamgambo wa za Kikosi cha Kidemokrasia cha Ukombozi wa Rwanda (FDLR) waliovaa kiraia pia wamewasili katika mji huo.

Milima inayozunguka Kishishe ni ngome za FDLR, kundi ambalo limeundwa na wanamgambo pamoja na viongozi wa Wahutu kutoka Rwanda.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa (UN), Novemba 2022, waasi wa M23 wameua watu 171 Kishishe, wengi wao wakiwa ni vijana.

Waasi hao wa M23 walidhibitiwa mwaka 2013, hata hivyo Novemba 2021, walianza mashambulizi huko Kivu Kaskazini, eneo linalopakana na nchi za Rwanda na Uganda.