Majaliwa aipongeza GGML kuwainua wanawake, mhitimu FFT aula

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akimkabidhi Meneja (Utawala bora) fedha kutoka GGML, Tatu Tibashengwa cheti cha utambuzi wa mchango wa kampuni hiyo katika ufadhili wa mafunzo ya Mwanamke Kiongozi (Female Futura Tanzania-FFT) mwaka 2023.  Tatu ni mmoja wa wahitimu wa mafunzo hayo yaliyofanyika kwa miezi tisa chini ya uratibu wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE). Wengine waliohitimu kutoka GGML ni Changwa Mjella, Hellen Mallya na Flora Muhochi.

Muktasari:

  • Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ametumia Mahafali ya nane ya Programu ya Mwanamke Kiongozi (Female Future Tanzania) kuipongeza Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) kwa kuwawezesha wanawake.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameipongeza Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) kwa kuwawezesha wanawake walioajiriwa ndani ya kampuni hiyo kujiendeleza kielimu na kuwapa promosheni za nafasi mbalimbali ikiwemo za uongozi pindi wanapohitimu mafunzo au masomo yao.

 Pia, ametoa wito kwa kampuni nyingine kutoa ufadhili wa mafunzo mbalimbali kwa wafanyakazi wanawake ili kuongeza tija katika matumizi ya kidijitali kama ilivyofanya GGML.

Majaliwa ametoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam katika Mahafali ya nane ya Programu ya Mwanamke Kiongozi (Female Future Tanzania) iliyoratibiwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) ambapo jumla ya wahitimu 65 walitunukiwa vyeti wakiwamo wahitimu wanne kutoka GGML.

Mmoja wa wahitimu hao ni Tatu Tibashengwa ambaye alikuwa Msimamizi wa Uthibiti wa Ndani,lakini hivi sasa amepandishwa cheo na kuwa Meneja (Utawala bora) fedha. Wengine waliohitimu kutoka GGML ni Changwa Mjella, Hellen Mallya na Flora Muhochi.

Akizungumzia hatua hiyo, Majaliwa alisema,“nimefurahi kusikia wanawake kadhaa waliohitimu katika program hii wamefanikiwa kupata nafasi za juu za uongozi kama dada yetu wa GGML (Tatu Tibashengwa), hayo ndio mafanikio tunayoyataka.”

Pia, alitoa wito kwa wanawake kujitokeza kwa wingi kushiriki katika programu hiyo kwani imeendelea kuwa na matokeo chanya kwa washiriki na kuleta mabadiliko makubwa kwenye utendaji wao wa kazi na kugusa maisha yao binafsi.

Majaliwa aliwataka wanawake wote na Watanzania kwa ujumla kuendelea kuchangamkia fursa mbalimbali zinazotokana na matumizi ya teknolojia katika kujenga uchumi wa kidijitali.

Kwa upande wake,  Mtendaji Mkuu wa ATE, Suzanne Doran alisema tangu waanze programu hiyo kwa kushirikiana na ESAMI, wamekwishatoa mafunzo kwa wanawake 274 kutoka kampuni 79 wakiwemo Wabunge na wawakilishi 150.

Awali, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya GGML, Terry Strong, Kaimu Meneja Rasilimali Watu, Dominic Marandu alisema tangu mafunzo hayo yalipoanzishwa mwaka 2016, GGML imepeleka jumla ya wafanyakazi wa kike 17 katika program ya kuwapatia mafunzo hayo ya Female Future Tanzania (FFT).

Alisema baadhi ya wahitimu wameteuliwa kwenye nafasi mbalimbali za uongozi ndani na nje ya kampuni hiyo, akiwemo mjumbe wa bodi ya STAMICO, Janeth Luponelo.

“Hivi sasa tupo katika mchakato wa kupendekeza majina ya wafanyakazi wengine wanne wa kike katika program inayofuatia,” alisema. Alisema GGML itaendelea kuongeza ujumuishwaji, usawa na kukubaliana na tofauti mbalimbali zilizopo katika makundi ya kijamii.

Kuhusu promosheni aliyoipata kutoka GGML, Tatu Tibashengwa mbali na kueleza kuipokea kwa furaha, aliishukuru kampuni hiyo kwa kutambua utendaji wake uliotukuka, ufanisi, ujasiri na hata kudumisha dhana ya usawa wa kijinsia mahala pa kazi.

“Ni sehemu ambayo wanawake wengine watavutiwa kufanya kazi na hata wenzangu walioajiriwa ndani ya kampuni, watapata hamasa ya kwamba inawezekana,” alisema.

Alisema ataitumia nafasi hiyo kuwawakilisha wanawake vizuri lakini pia atakuwa tayari kuwapa miongozo wanawake wanaotaka kuwa viongozi kama yeye.